Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha pamoja na Watendaji wake, Katibu Mkuu pamoja na washirika wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tunalolizungumzia ni muhimu sana na Bunge kama Watanzania lazima tujue safari ya maendeleo inaenda polepole lakini hadi hapo tulipofikia tuko pazuri sana. Leo tunazunguka katika nchi yetu kwa kutumia taxi kwa sababu ya uboreshaji na ukusanyaji mzuri wa mapato yetu. Niwapongeze watu wa TRA kwa kazi kubwa. Nimpongeze Kamishna wa TRA kwa jambo ambalo amelianzisha la kuzunguka na kukutana na walipa kodi wadogo wadogo, ni jambo ambalo tulikuwa hatujawahi kuliona. Leo walipa kodi wetu hawa wanapata elimu nzuri ya kuweza kulipa kodi na kuweza kukusanya mapato mengi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie tu jambo moja. Katika ukurasa wa 69 wa hotuba yake ameeleza mfumo mzuri kwamba fedha zote za Bodi za Mazao zitakusanywa na Mfuko Mkuu wa Serikali, ni jambo jema, atupe commitment itakayokuwa rafiki na time ya kilimo, kwa sababu jambo hili linaenda kwa muda. Wasiwasi mwingi kwa Wabunge ukisikiliza michango yao ni kwamba fedha hizi zikiingia kwenye kapu lile zitapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuhakikishie fedha hizi zitarudi kwa wakulima on time ili tusije tukaachana na muda kwa sababu ukiangalia kwenye pamba au tumbaku yote yanaenda na muda. Mheshimiwa na Wizara yake waangalie ni jinsi gani watakuwa wanarejesha kwenye Bodi husika kulingana na muda wa mahitaji ili tuondokane na hii tabia ya kulaumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba Mheshimiwa Waziri alizungumzia suala zima la kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mazao ya mifugo. Katika kupitia kitabu hiki na Bill itakayokuja kusomwa nimeona kipengele cha soya lakini Tanzania kama nchi cha muhimu ni kupunguza tozo kwenye alizeti, pamba, mahindi na karanga, ndiyo tutaongeza bei kwa wakulima wetu kwa sababu soya hapa nchini haizalishwi sanasana iko Malawi, iko sehemu ndogo sana kule Songea na inazalishwa kwa percent ndogo sana. Wafanyabiashara wadogo wadogo wanachukua mashudu ya alizeti na pamba. Utakapoiweka hivyo bei zetu zitaendelea kuwa nzuri lakini tutachochea uzalishaji mkubwa wa mazao ambayo tunayatumia wenyewe. Naomba na hilo nalo Mheshimiwa Waziri alichukue na alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekaa takribani miezi mitatu, tunaitegemea sana Wizara hii kutukusanyia fedha ili tuzipeleke kwenye maendeleo ya wananchi wetu. Kwa Mkoa wetu wa Simiyu tuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria kuja Mkoa wetu wa Simiyu ikiwepo Bariadi, Itilima, Meatu, Maswa na Busega kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri ndiye mwenye jukumu kubwa la kuhakikisha anazungumza na wadau wetu, naomba afanye hivyo ili fedha zipatikane mradi ule uweze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mifumo ambayo wameipendekeza ni mizuri sana. Mifumo hii ikisimamiwa vizuri inaweza ikaleta tija na tukaondokana na malalamiko ya kila siku. Mifumo hii ya kielektroniki ambayo wanaileta iko vizuri, lakini ziko changamoto ambazo zinajitokeza kila kukicha, wakati mwingine network zinapotea zaidi ya siku mbili, tatu, kwa hiyo, unaweza ukakuta Serikali inapoteza mapato. Mkiweka misingi na mifumo mizuri inaweza ikatusaidia sana tukawa na jambo ambalo linaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila jambo tunalolianzisha tujaribu kulifanyia analysis za kutosha na tuwe na uvumilivu wa kukubali mambo ambayo yanaenda vizuri. Nashauri Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla waendelee kupokea michango mbalimbali ili kushughulikia changamoto zilizopo kwenye maeneo yetu mbalimbali. Lengo ni moja tumekubaliana lazima tuwe na mfumo rafiki utakaosaidia kuleta tija kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ushauri na naomba mliangalie. Tunazo halmashauri zaidi ya mia moja, tunakusanya kodi na kukopesha mikopo midogo midogo. Nashauri jambo hili kwa siku zijazo Waziri ajaribu kulitazama ili fedha hizi ziende kwenye kapu na taasisi moja ili kusudi vijana wetu wawe wanaenda kuzikopa na kufuatiliwa kwa utaratibu mzuri, kuliko hivi sasa fedha hizi zimekuwa nyingi lakini ukiangalia marejesho yake hayana tija. Fedha hizi ni nyingi ikiwa zitakusanywa vizuri na kuwekwa kwenye kapu na taasisi moja ya kifedha, zinaweza kutoa mchango mkubwa sana na kuleta uchumi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo sasa mfano, Wilaya ‘X’ Afisa Maendeleo akihama mkopo ule unafifia na kupotea/kufa lakini kama kuna taasisi ya fedha imekabidhiwa fedha hizi inaweza kujiendesha vizuri na tukawa na fedha nyingi. Pia kwa kufanya hivyo hizi kelele tunazopiga kila siku kwamba halmashauri hazitengi fedha zitaisha kwa sababu halmashauri husika kwa makusanyo itakayokusanya asilimia 10 itachukuliwa itapelekwa kwenye chombo ambacho kimepewa mamlaka na aliyepewa mamlaka haya lazima azikopeshe kwa vijana wetu ili kusudi tuweze kutengeneza uchumi mzuri lakini vilevile tuweze kuwajengea uwezo vijana wetu kwa ajili ya kujipatia kipato na kizazi kinachokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.