Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu kwa ajili ya hoja ya Serikali iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, tunajadili Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/2019, lakini pia tunajadili Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, nitaanza kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi. Kwanza niipongeze Serikali kwa kutenga asilimia 37 ya bajeti yote kwa shughuli za maendeleo. Kufanya hivi ni kuendana na mpango wetu wa miaka mitano ambao tulishaupitisha hapo awali wa kwamba tutakuwa katika kila bajeti ya kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya maendeleo kati ya asilimia 30 na asilimia 40. Kwa hiyo, bajeti hii imeweza kukidhi matakwa hayo ya mpango wa miaka 5 tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kupongeza kwa sababu Serikali imefanya jambo kubwa lifuatalo, pengine wenzangu hawajaliona au wameliona; ni kwamba fedha za ndani ambazo Serikali imeweza kuchangia, kwa mwaka uliopita, mwaka 2017/2018 ambayo ilikuwa ni asilimia 38, kwa fedha za ndani zilikuwa asilimia 75 na fedha za nje zilikuwa asilimia 25. Mwaka huu Serikali imeamua kuongeza mchango wa fedha za ndani na kupunguza mchango wa fedha za nje, kwamba kwa mwaka huu wa fedha mchango wa fedha za ndani ni asilimia 82 wakati mchango wa fedha za nje ni asilimia 18. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itaweza kwenda kutusaidia kuondoa tatizo kubwa sana ambalo limekuwa likisababisha budget performance kuwa siyo nzuri kwa sababu ya kulegalega kwa utoaji wa fedha za nje. kwa mfano, katika mwaka ulioisha wakati utekelezaji kwa upande wa fedha za ndani ulikuwa asilimia 85, fedha za nje zilikuwa asilimia 15 tu peke yake; lakini kwa mwendo huu tunaoenda nao pengine tutafika mahali.

Mheshimiwa Spika, nataka kuishauri Serikali twende hivi, ikiwezekana tufike mahali ambapo fedha zote za maendeleo zitatokana na fedha za ndani na fedha za nje ziwe ni fedha za ziada, tutaweza kwenda kwa kasi na kuweza kutekeleza vizuri zaidi malengo yetu katika miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda labda ningesema jambo moja tu kwamba ingekuwa wadau wa fedha za nje (wachangiaji kutoka nje) nao wangechangia asilimia 85 kama tulivyochangia sisi kwa fedha za ndani, budget performance kwa kufikia mwezi Aprili mwaka huu ingekuwa ni asilimia 73. Mahali ambapo hata sisi wenyewe kama tungechangia asilimia 100 na wafadhili wangechangia asilimia 100 kwa mwezi Aprili tungekuwa tumefikisha asilimia 85.4 na kwa hiyo kuwa na mwelekeo wa kuweza kupata matokeo mazuri zaidi ya kibajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu hali ya uchumi na mpango wa maendeleo wa Taifa tumefanya vizuri sana, kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Serikali. tuna mafanikio ya kiuchumi kwa upande wa uchumi wa Taifa kwa vigezo vya uchumi wa Taifa kwa jumla, lakini pia kwa ongezeko la Pato la Taifa na udhibiti wa mfumuko wa bei. Si tu kwa ndani lakini pia hata katika eneo la Afrika na Kusini mwa Sahara, miongoni mwa nchi za SADC na nchi za Afrika Mashariki, takwimu zinajieleza, kwa sababu ya muda siwezi kusoma takwimu hizo, lakini tumefanya vizuri sana kiwango cha kuweza kujipigia Makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kufanya vizuri huko kumeelezwa kwenye taarifa hiyo hiyo kwamba kumetokana na jitihada za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, lakini pia kuongezeka kwa uzalishaji wa baadhi ya madini na pia kuimarika kwa sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, napenda hapa niwapongeze wachapa kazi wote wa Tanzania, walipa kodi wote, wizara kwa niaba ya Serikali nzima pamoja na uongozi wa juu wa Serikali wakiongozwa na Jemedari Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Tanzania akisaidiwa na wasaidizi wake wa karibu kabisa Makamu wa Rais mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pengine tungeweza kuona namna ambavyo tunaweza kufanya vizuri hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ili tuweze kufanya vizuri zaidi kipo kitu kimoja ambacho ni nyenzo hatujakitumia sawasawa na hiki siyo fedha, mali wala mtaji mwingine wowote ule isipokuwa tu lugha ya Kiswahili. Pengine wengine wakinisikia nikisema Kiswahili wanaweza wasielewe, lakini watafiti duniani kupitia The World Economic Forum wamesema hivi, kwanza wamesema speaking more than one language can boost economic growth. Pia wamesema multi lingualism can fuel exports increase salaries and help innovation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki tuna shida kidogo kwenye mkataba wenyewe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kiswahili hakipewi umuhimu. Kwenye kifungu cha 137 cha Mkataba wa Afrika Mashariki imeandikwa hivi Article 137, official language.

137._ (1) The official language of the community shall be English,

(2) Kiswahili shall be developed as a lingua franca of the community.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu moja kwa moja hapa kupitia Serikali tushauri ili katika uwanja ule wa Afrika Mashariki na Kiswahili kitumika kama official language. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sababu ya msingi ya kusema hivyo ni kwamba nyaraka muhimu ambazo zinatoa mwelekeo wa kimaendeleo na kuweza kuzungumzia mipango mbalimbali ya Afrika Mashariki kama mkataba wenyewe, lakini vision ya East Africa ya mwaka 2050, pia mipango kama development strategy, protocols zote pamoja na facts and figures na mambo ya ripoti za kila mwaka zote zipo kwa Kiingereza.

Mheshimiwa Spika, tunaweza kushindwa kuwafanya Watanzania walio wengi kushiriki katika ushindani huo kwa sababu ya kikwazo cha lugha. Hii inawezekana kwa sababu duniani huko ziko taasisi nyingine zinazounganisha au zinazojumuisha nchi nyingine nyingi zaidi SADC, European Union, COMESA CARICOM, ikiwemo na nyingine nyingi. Hata Umoja wa Mataifa wenyewe una lugha sita rasmi, UN ina six official languages ikiwemo Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Ki-Russia na Ki-Spanish. Hii inawezesha kwanza ushiriki wa watu wote wanaohusika katika muunganiko huo na kuwawezesha kuweza kuelewa mipango mbalimbali na kuweza kulinganisha mipango ya nchi zao na ile ya nchi hizo za mijumuiko katika hizo forums.

Mheshimiwa Spika, nirudi tena upande wa Tanzania, tunao mpango wetu wa muda mrefu unaitwa The Long Term Perceptive Plan (LTTP) wa mwaka 2011/2012 mpaka mwaka 2025/2026. Kwenye kipengele cha institutional framework Serikali ilipangiwa jukumu la kutawanya nyaraka zote za maendeleo kwenda mpaka kwa wananchi. Vision yenyewe huo mpango wenyewe wa muda mrefu lakini mipango ya miaka mitano yote huu wa kwanza na huu wa pili na wa tatu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Namalizia kwa kusema kwamba mipango yote hii Serikali iweze kutekeleza kwanza kwa kuitafsiri nayo iwe ya Kiswahili, halafu iweze kuitawanya na kuipeleka kule kwa wananchi ambao ndio watekelezaji wa hii mipango, tutaweza kuona namna ambavyo tunaweza kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.