Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi yetu kubwa ni kuishauri sana Serikali na kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza yale yote ambayo tunajaribu kuyaona kwa faida ya wananchi wetu. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la utekelezaji wa yale tunayoyaamua ndani ya Bunge, mwaka 2016/2017 na mwaka 2017/2018 nilitoa ushauri kwenye Bunge hili na nikawaambia ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha akajaribu kujikita sana kutoa ushauri pia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa bajeti zetu zote ambazo tunazipitisha ndani ya Bunge zinatekelezwa kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kuamini, utekelezaji wa bajeti kwenye nchi hii sasa hivi imekuwa ni kitendawili. Hoja kubwa hapa ya kutengeneza bajeti hizi ni kwa ajili ya kuinua maisha ya Watanzania, lakini pia Serikali hii inasema kwamba inataka kwenda kwenye uchumi wa kati. Kwenda kwenye uchumi wa kati kunahitaji hatua, huwezi kutoka kwenye ufukara ukaenda kwenye uchumi wa kati, ni lazima uchumi wa kati uwe na hatua zake.

Mheshimiwa Spika, leo huwezi kuamini, Watanzania wanazidi kuwa fukara, wanazidi kurudi nyuma, leo tunakazana tu kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati, kwa sababu tunachokifanya sasa hivi kwenye bajeti hizi tunafanya bajeti ya vitu na siyo kwa ajili ya wananchi wetu na hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili unaweza ukaliangalia katika bajeti zetu zote. Ukiangalia maeneo ambayo wananchi wengi maskini tunatakiwa tuwainue maeneo haya hayapelekewi fedha kabisa. Ukiangalia kwenye kilimo, mifugo pamoja na uvuvi, fedha haziendi kabisa. Ukiangalia kwenye kilimo mwaka 2016/2017, fedha iliyokuwa imetengwa ilitengwa bilioni 101 lakini kati ya bilioni 101 fedha iliyokwenda kuinua kilimo ni shilingi bilioni 3.3 peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018, ilitengwa bilioni 150 lakini fedha iliyokwenda kuinua kilimo imekwenda kupelekwa shilingi bilioni 27.2 peke yake. Sasa tunavyosema kwamba tunataka kuinua uchumi wa Tanzania ni lazima tuzungumzie kwa wananchi hawa ambao ni wavuvi, wafugaji pamoja na wakulima. Tusipoweza kuinua kilimo, tusipoweza kuwainua wavuvi pamoja na wafugaji, tunakoelekea tunatatwanga maji kwenye kinu, tutabaki hapa na tutaendelea kuishangaa Kenya na nchi zingine zinapiga hatua.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema jambo moja, ukiangalia kilimo pamoja na uwekezaji wa bilioni tatu kwa mwaka 2016/2017, lakini mchango wa kilimo kwenye Pato la Taifa ulichangia asilimia 29.2, pamoja na uwekezaji mdogo ambao ulifanyika. Kwa hiyo, kama kweli tutawekeza vizuri kwenye kilimo, hata tungewekeza labda hii fedha bilioni 150 ingetumika yote, inawezekana kilimo kingeweza kuchangia Pato la Taifa hata kwa asilimia 50 au 45. Kwa hiyo tungekuwa tayari tunasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, umeona wavuvi, leo wavuvi katika Taifa hili imekuwa ni janga, wanachomewa nyavu, wanaharibikiwa mambo yao, wanakamatwa, ziko sheria kandamizi ambazo zimetungwa na sasa hivi huwezi kuamini, wavuvi sasa katika Taifa hili hawaonekani kama ni watu muhimu katika kuchangia Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017 kwenye uvuvi peke yake, shughuli za maendeleo, tulitenga shilingi bilioni mbili ili fedha ziende kule lakini miaka miwili yote hakuna hata shilingi iliyopelekwa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mifugo, tulitenga bilioni nne kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha mifugo yetu, pia na kuwawezesha wafugaji wetu lakini hakuna hata shilingi iliyopelekwa kwenye maeneo hayo. Leo tunakaa ndani ya Bunge tunasema tunatengeneza bajeti kwa sababu ya wananchi maskini, hao wananchi maskini tunaowasema ni watu gani?

Mheshimiwa Spika, kitendo cha kununua ndege tano kwa wakati mmoja tafsiri yake ni kwamba tunakwenda kuinua uchumi wa watu asilimia tano tu, kwa sababu katika nchi hii watu wenye uwezo wa kupanda ndege ni asilimia tano peke yake. Tunatumia mamilioni ya fedha kupeleka kule tunawaacha Watanzania maskini ambao tulipaswa kuwainua ili waweze kujenga nchi na kuhakikisha kwamba uchumi unaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitaka kukuonesha hali halisi ilyopo, ukiangalia kwenye nchi yetu kila mwaka wanafunzi wanaohitimu elimu ya juu ni karibuni 800,000 kati ya watu 800,000 wanaopata ajira ambazo ni rasmi wanapata watu 40,000 peke yake. Kwa hiyo, kuna wananchi ambao ni wasomi 760,000 hawapati ajira kabisa na wanategemea ajira hii ambayo siyo ramsi, kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi, lakini hakuna fedha inayokwenda kule.

Mheshimiwa Spika, hii tafsiri yake ni kwamba hatujajiandaa kuondoa umaskini wa Watanzania badala yake tunaendekeza maneno ndani ya Bunge hili. Hakuna mtu yeyote, wanayemdanganya, wamepewa madaraka makubwa na wananchi wa Tanzania, nia na madhumuni wakiwa na matumaini kwamba wangeweza kuwafikisha wanapohitaji. Leo Watanzania kila maeneo wanalia, tunataka tuseme, ni lazima wabadilike! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu pekee unayeweza kujenga nchi sasa hivi ni wewe kwa sababu Muhimili wako ndiyo unaosimamia Serikali, Mhimili wako ndiyo unaoweza kutoa maagizo na kuhakikisha kwamba Serikali inafanya kazi vizuri, lakini kama na wewe utashindwa kuhakikisha kwamba unasimama kama kiongozi wa Mhimili na kuhakikisha kwamba unakemea bajeti hizi, kama kweli bajeti zinakuja tunatekeleza kwa asilimia 18, tunatekeleza kwa asilimia 20, tunatekeleza kwa asilimia sifuri, tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania hawa.

Mheshimiwa Spika, tunaomba tutekeleze wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kuhakikisha kwamba Serikali hii inatekeleza wajibu wake kama ambavyo tunapitisha bajeti humu ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia sana barabara. Ukiangalia mtandao wa barabara katika nchi hii ni karibuni kilometa 86,472, kati ya kilometa hizi mtandao wa barabara ambao sasa hivi uko kwa lami karibuni ni asilimia 9.7 peke yake. Kwa hiyo, hata kwenye barabara pia bado tuko nyuma sana, tafsiri yake ni kwamba tuna safari ndefu ya kujenga uchumi wa nchi kwa sababu hatutakwenda kwenye viwanda kama hata barabara hatuna. Kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaonesha ni namna gani tunaweza tukajenga uchumi huu kwa vitendo na siyo kwa maigizo kama ambavyo yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunazungumzia pia madini. Tunasema, ooh! Sasa hivi tunataka tujikite kwenye madini, yatachangia Pato la Taifa, madini yanawezaje yakachangia Pato la Taifa kama uwekezaji unakuwa kidogo kiasi hiki! Ukienda kuangalia kwenye madini mwaka jana STAMICO tuliwatengea shilingi bilioni 20.9, fedha ambayo tuliwapelekea STAMICO tuliwapelekea bilioni 2.8 peke yake ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 10 tu ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, tunawezaje tukahakikisha kwamba tunapata mapato mengi kwenye madini wakati hatuwekezi. Kwa hiyo, yako mambo mengi ambayo ni lazima pia tusimame tuangalie, kama Taifa ni namna gani tunaweza tukajenga Taifa hili kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie la mwisho kabisa ni kampuni ya jotoardhi. Kampuni ya jotoardhi ukisoma kwenye ukurasa wa 24, ukiangalia Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema, kati ya shilingi bilioni 409 zilipelekwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba umeme vijijini pamoja na jotoardhi. Hata hivyo, ukiangalia hapa mwaka jana fedha iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya joto ardhi ilikuwa bilioni 21, lakini fedha iliyopelekwa ilikuwa ni Sh.53,715,000/= ambayo ilikuwa ni sawasawa na asilimia 0.24 ndiyo iliyokwenda kwenye jotoardhi. Katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri anaonesha kwamba fedha nyingi ilipelekewa kitu ambacho hakikufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusisubiri miujiza, ni lazima tutekeleze bajeti zetu tunazozipanga ndani ya Bunge zikatekelezwe huko na watu wote wanamlaumu Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Tunaomba abadilike na kama ameshindwa, atuachie nafasi ili tuweze kusogeza Taifa hili mbele.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naikataa hoja.