Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rukia Ahmed Kassim

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nakushukuru kwa kunipa heshima iliyo kubwa, nakuhaidi kwamba nitaienzi. Baada ya kusema hayo, naipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio chetu Waheshimiwa Wabunge Wanawake (PWPG) pamoja na akinababa ambao walituunga mkono kwa kuondoa VAT kwenye taulo za kike. Sasa watoto wetu watasoma vizuri na utoro shuleni utapungua. Tunaishukuru sana Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo, naanza na kuchangia kwa kusema kwenye pato la Taifa. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kama pato la Taifa limeongezeka kwa asilimia 7.2 kwa mwaka 2018 kutoka asilimia 7.1 mwaka 2017. Pia katika kitabu hicho hicho kasema kama mapato ya ndani yamekua, yamefikia asilimia 15.8 katika mwaka 2018/2019 kutoka asilimia 15.3 kutoka mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa pato la Taifa, pia ni kuongezeka kwa fedha kwa wananchi wetu na wao wakawa nazo mfukoni. Hali ya wananchi wetu ni ngumu sana, maisha yamekuwa magumu kupita maelezo. Sasa tukisema kama pato linaongezeka, lakini maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu, bado naona pato halijaongezeka na hali bado ni ngumu. Kwa hiyo, Serikali ifikirie namna gani ya kuwatoa watu wetu katika umaskini huu uliokithiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake, sijui kama ni kwa mwono wangu mdogo lakini kachangia zaidi, yaani kaelezea zaidi namna ya kuongeza mapato kwa kodi, lakini hakuna mahali nilipopaona ambapo kaonesha namna gani tutafanya biashara ili watu wetu waweze kupata ajira na kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya nchi, maisha ni magumu. Ushahidi wa haya, tuliangalieni Jiji la Dar es Salam lilivyo. Watu wengi wameanza kuhama, kuna baadhi ya matajiri wamefunga milango ya maduka, hawauzi; kodi na tozo zimekuwa ni nyingi. Zamani ilikuwa ukitaka mlango Kariakoo
mpaka umwondoe mtu kwa kumpa pesa, yaani kilemba zaidi ya shilingi milioni 10 au 20, anaondoka anakuachia wewe mlango ufanye biashara. Leo ukienda Kariakoo milango ni bure zaidi ya ile kodi utakayolipa, unachukua wala hakuna mtu wa kumwondoa. Hii yote ni kutokana na ugumu wa maisha na biashara haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani wafanyabiashara walikuwa wanakwenda Zanzibar kuchukua biashara kuleta Bara. Leo hakuna anayekwenda, kodi zimekuwa kubwa, gubu na kero la TRA imekuwa kubwa, wafanyabiashara wanashindwa, wamefunga mikono, wengine wanarudi vijijini, wengine wanahama.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya matajiri sasa hivi wanauza majumba yao, wanafunga biashara Tanzania wanakwenda nchi za Arabuni wanapewa resident permit na wanapewa na nyumba wanaishi huko. Sasa hali ikiendelea hivi, maisha yatazidi kuwa magumu kwa sababu hawa wananchi wadogo wa kipato cha chini wanashindwa kupata ajira. Kwa hiyo, naishauri Serikali tutafute namna gani ya kuwasaidia watu wetu waondokane na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mpango, kasema katika ukurasa wake wa 32, kuwa kuna mikakati ya Serikali ya kuongeza mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na urasimishaji wa majengo na kupima viwanja. Sasa napenda niitanabaishe Serikali, katika kupima viwanja huku ikiwa wataona tutaongeza mapato, tunawaumiza wananchi wetu wa hali ya chini. Kwa sababu kuna watu wameishi katika Vijiji miaka pengine 20 au 30 wamezaliwa hapo, wameishi wamejenga nyumba zao za tope, Serikali inakwenda kupima inawaondoa halafu bila ya kuwalipa.

Mheshimiwa Spika, haya nasema kwa ushahidi hapa Dodoma, Swaswa Ng’ambo kuna watu ambao wamekwenda kupimiwa pale wameambiwa wakahamie Mkalama. Matokeo yake hawalipwi na hivyo viwanja wanavyopewa Mkalama wanaambiwa walipe Sh.200,000.

Hivi jamani tujiulize Mama Lishe anapika chakula ile hela hata ya ugali wake na watoto wake hapati au anajitwika beseni la ndizi anapita akiuza, ikifika jioni hata hela ya kula hana. Serikali inamlazimisha atoe Sh.200,000/=, atazipatia wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa napenda niiulize Serikali, wale wananchi tunaowahamisha sasa Ng’ambo tunawalazimisha wakanunue viwanja Mkalama, kama mtu kashindwa ina maana nyumba yake itavunjwa na yeye hatalipwa na atakosa pa kukaa? Tunawatia watu wetu umaskini. Serikali lazima iangalie, tusiwafanye watu kuichukia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kutokana na mambo tunayoyafanya sisi viongozi. Naishauri Serikali watu hawa walipwe na huko wanakopewa viwanja wapewe bure, siyo waambiwe wanunue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, nataka kuzungumzia kuhusu BoT. BoT wanasajili Benki ambazo hazina sifa. Kuna Benki zimefunguliwa kwa mfano, FBNE. Benki hii ilifilisiwa tokea mwezi Agosti, 2017. Sasa najiuliza, hivi BoT mlivyoisajili hii Benki hamkujua kama haina viwango? Haikidhi haja? Benki hii imefilisiwa, kuna watu wamefanya kazi miaka 40, kachukua pesa zake za gratuity kaziweka katika benki ile, matokeo yake Benki imekuja kufilisiwa anaambiwa mtu huyu atalipwa; maana yake imewekwa ufilisi chini ya Benki ya Amana. Wamelipwa shilingi milioni 1.5, wameanza kulipwa Novemba, 2017. Wameambiwa kama watalipwa tena ni baada ya kuuzwa mali za ile Benki. Hapo mwanzo walipoisajili Benki hawakujua kama haina vigezo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, BoT waache kusajili Benki ambazo hazina viwango. Benki zilizoshindwa kufanya kazi zifungwe. Tusiwatie umaskini wananchi wetu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa atuambie watu walioweka pesa zao FBNE, watu wale hawana makosa, ni maskini wa Mungu, sisi ndio tuliwahamasisha waweke fedha zao benki. Kwa hiyo, tuambiwe lini watalipwa pesa zao? Kama hatukuambiwa, tunashawishi watu, tunazuia shilingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpango, hiyo mipango yake yote aipange, atuambie lini watu hawa watalipwa fedha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nijielekeze kwenye Zimamoto. inavyoonekana Serikali imeshindwa kusimamia vifaa vya umeme nchini; havina viwango, ni vibovu. Kila siku yanatokea maafa ya moto, ukiuliza unaambiwa ni fault ya umeme. Inakuaje hata nchini viingizwe vifaa ambavyo havina sifa? Vibovu! Tunawatia watu hasara, tunawatia umaskini. Maafa ya moto yamekuwa makubwa. Juzi Kariakoo imeungua nyumba siku tatu imeshindikana kuzimwa. Kwanza hatuna vifaa. Serikali iagize vifaa vya Zimamoto, halafu tuongeze magari ya Zimamoto. Katika Wilaya zetu hakuna Ofisi za Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kwanza ihakikishe vifaa vya umeme vinavyoingia nchini viangaliwe, viwe vina viwango na pia tuhakikishe tunaagiza magari ya Zimamoto ambayo yatasaidia kuzima moto, tena tuagize na vifaa vya kisasa. Maafa ya moto yamezidi, kuna mashule yameungua, juzi Buguruni zimeungua nyumba zaidi ya nne, sijui tano; Kariakoo moto umeshindikana kuzimwa siku tatu; Zanzibar kila siku moto unatokea. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuhakikishie jambo hili analifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nijielekeze sasa kwenye huduma za afya. Mheshimiwa Waziri Mpango wanawake tunakufa bila ya kiasi. Tunakufa kutokana na Vituo vya Afya kutokuwa na Wodi ya Mama na Mtoto, hatuna Wodi ya Wazazi. Naomba Serikali ihakikishe kila Wilaya kuwe na hospitali ambayo itakuwa na Wodi ya Wazazi, chumba cha upasuaji pamoja na chumba cha mama na mtoto.

Mheshimiwa Spika, ahsante.