Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye mapendekezo ya Serikali. Nianze na kuipongeza Serikali kwa kuleta mapendekezo ambayo yanalenga sisi Wabunge tutoe mapendekezo yetu ili bajeti itoke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine Serikali imefanya vizuri sana, kwa mfano, ku-promote viwanda vya ndani na ili uweze ku-promote viwanda vya ndani lazima udhibiti bidhaa zinazotoka nje. Kwa hiyo, kupunguza kodi kwenye baadhi ya bidhaa ambazo tunaweza tukazalisha sisi wenyewe ni mpango mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hata kwenye mafuta ambayo tunaweza tukazalisha, tunalima alizeti na tuna viwanda vya alizeti, ili ku-promote hivi viwanda vifanye kazi vizuri wamepandisha kodi kwenye mafuta yanayotoka nje, hiyo ni sawa, lakini lazima tuhakikishe tunapata soko la uhakika la ndani ili wazalishaji wafanye vizuri. Kwa hiyo, hilo na mimi nakubaliana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu la pili ni bajeti. Bajeti ya mwaka huu 2018/2019 tumeenda na shilingi trilioni 32.5 mwaka jana tulikuwa na shilingi trilioni 31.6. Kuongezeka kwa bajeti ni kitu kizuri sana kwa sababu inalingana na mahitaji ambayo tunayo. Hatuwezi kusema mahitaji ya mwaka jana ni sawa na mahitaji ya mwaka huu. Kila mwaka mahitaji yanaongezeka na bajeti inaongezeka, huo ni mtizamo nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya Serikali kukusanya mapato siyo mibaya isipokuwa kwa sababu tumesema tunataka ku-promote vitu ambavyo tuna uwezo wa kufanya wenyewe ni jambo zuri sana. Kwenye ukusanyaji kwa mfano kuna Electronic Stamping Tax System, kama alivyoongea Mheshimiwa Zungu ni system nzuri sana kwa ajili ya kuongeza mapato ndani ya nchi yetu. Hapo naunga mkono kwa mtazamo wa kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi ni suala zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna issue ambayo Wabunge wengi tunajiuliza, hivi hatuna wataalam pale TRA, vijana wetu ambao wanasoma vyuo vikuu nje wakashindwa kusoma hii system, tukaidhibiti wenyewe, tukaanzisha ndani ya nchi na tukaitumia kukusanya, kwa hiyo, tumeshindwa kabisa? Kwa sababu unapofanya investment ukiona anaweza aka-recover within one year, atapata faida kubwa sana. Kwa mfano, yeye atawekeza kwa thamani ya shilingi bilioni 48 lakini katika hesabu za haraka haraka wamefanya analysis kwa mwaka mmoja anaweza akapata shilingi bilioni 66, tofauti yake ni shilingi bilioni 18 ambayo yote inaenda nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikawa ninajiuliza kama kuna zaidi ya shilingi bilioni 18 ndani ya mwaka mmoja, recoverage ya costs ikafanyika mwaka mmoja, kwa nini tusingesomesha vijana tukachukua hata shilingi bilioni 5 wakaenda kusoma nje wakarudi wakafanya kazi TRA wakakusanya kodi? Hili ni suala la kujiuliza sana. Hivi kuna umuhimu gani kuchukua makampuni ya nje waje wakusanye fedha yetu halafu wapeleke pale, sisi tukawa tumeshindwa. Mwaka wa pili kuna- possibility ya shilingi bilioni 66 zikaenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka siku moja tulifanya semina hapa, vijana wetu MaxMalipo vijana wetu wasomi wa hapa hapa Tanzania siku ile Wabunge tuliwapigia makofi sana pale ukumbuni wali-present issue za kukusanya kodi na wakasema kwamba wako worldwide sasa hivi. Hawa vijana wa MaxMalipo wameshindwa kufanya utafiti wa kukusanya kodi? Labda tuwaite, tuwaulize itakuwaje wameshindwa kufanya makusanyo ya humu ndani na wakienda kwenye nchi nyingine wanafanya vizuri na kusifiwa, lazima tuangalie sana. Halafu ule mkataba tumeweka mrefu sana ni mpaka miaka mitano. Tungeweka labda hata miaka mmoja au miwili ili tuangalie matazamio lakini miaka mitano, nadhani hii lazima iangaliwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bajeti tumependekeza vizuri sana, tumesema system siyo mbaya ni nzuri nia ni kudhibiti na tunataka tudhibiti hata uzalishaji wa maji. Tunajua maji ni muhimu, tulikuwa tunafikiria kufanya exemption kwenye product za maji ili watu waweze kupata maji, watumie maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea na Ndugu yangu hapa Mheshimiwa Charles Kitwanga, yeye alishafanya kazi Benki Kuu na utaalamu wa masuala ya electronics, nikamuuliza hivi wewe kama Mbunge mtaalam umeshindwaje ku-advise tuangalie hii system, kweli nimem- challenge hapa. Amefanya kazi BoT karibu miaka kumi na system ya tax collection anaijua. Ameshindwa kunijibu vizuri lakini naendelea kumuuliza lazima Wabunge wataalam watusaidie katika collection ya tax katika nchi hii na tunataka tax revenue iwe juu. Ndiyo maana kuna Wabunge wanachaguliwa wataalam. Kwa hiyo, nimeona hili suala ni la msingi sana nilielezee hapa ili siku nyingine tusianze kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka niipongeze Serikali kwenye mgao wa fedha hasa ile ya vijana na wanawake. Point ambayo nimeipenda pale, ile asilimia 5 kwa vijana na asilimia 5 kwa akina mama Serikali imesema hakuna interest, cha msingi ni usimamizi mzuri, hilo ni jambo zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ni challenge hasa Wizara ya Fedha, ule Mfuko Mkuu fedha yote mtakusanya kutoka Halmashauri, kutoka Serikali za Mitaa, na sehemu zote mtakusanya pale, halafu Halmashauri ikitaka kutumia itaomba kufuatana na mahitaji. Challenge ambayo ipo pale urudishwaji wa fedha unachukua muda mrefu sana. Lazima tuwe makini, Wizara ya Fedha lazima iwe active
katika kurudisha fedha Halmashauri. Tunaweza tukawa tuna system nzuri ya kuweka kwenye akaunti moja lakini Halmashauri inaweza ikatuma maombi ya kupewa fedha ili watumie mkachelewesha. Hili lazima tutoe angalizo kwa Serikali, kwamba kama Halmashauri zimeeomba fedha on time basi wapewe fedha on time. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mufindi kuna fedha ya maji na Waziri wa Maji aliahidi kwamba mwezi Mei angeweza kuipeleka ile fedha. Wameomba kuanzia Machi tunaenda Julai ile fedha hawajapewa mpaka leo. Ni mradi wa maji mmoja tu. Sasa najiuliza kama mradi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri akishirikiana na Engineer ameandika request, vigezo vyote viko pale, tena ni shilingi milioni 270 mpaka leo Juni mradi wa maji kule umesimama Kata ya Mtwango wananchi hawana maji. Kupeleka shilingi milioni 200 ni kazi ya siku moja tu, mimi nikikaa kwenye komputa just a minute nimeshapeleka transfer ya hela zile, lakini mpaka leo hazijapelekwa. Je, tukisema wapeleke shilingi trilioni kadhaa kwenye Halmashauri itachukua muda gani? Hii ni bajeti ya mwaka mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi Wizara ya Fedha ina shilingi trilioni 12 ambazo nyingi ni miradi zinapitia pale. Naomba Serikali, system ni nzuri ndiyo maana naiunga mkono, lakini utendaji kazi lazima tuongeze juhudi, lazima tuende na muda. Bahati mbaya sana sisi huwa hatujali muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.