Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nami niweze kuchangia mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono mapendekezo haya ya Serikali kwa asilimia mia moja, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na wafanyakazi wake kwa maandalizi mazuri kwa kweli ya hotuba hii. Nina ushauri ambao ningependa kuutoa, lakini kwa sababu tukienda kwa wenzetu hawa wa TRA kwa sababu yote tunayozungumza humu ndani lazima pesa zipatikane, wala siyo vinginevyo, wala sio maneno. Sasa ni namna gani ofisi yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha inaweza ikapata hizi shilingi trilioni 18 ambazo tumeipa jukumu la kuzitafuta TRA. Sasa ni lazima kwanza ile mianya ya upotevu lazima tuizibe. Lakini wafanyakazi wenyewe wa TRA ambao wanafanya kazi nzuri sana, sina mashaka na TRA wanafanya kazi nzuri sana na ndiyo maana mapato kila mwaka kila mwezi yanaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wajibu wetu sasa, Mheshimiwa Waziri hakikisha hakuna shilingi hata moja inayolala nje, pesa ya Serikali hata senti moja inayolala nje, hakikisha kwamba kila shilingi inayokusanywa lazima iingie ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye nidhamu ya matumizi ya fedha, yapo matumizi mengine kwa kweli hayafanani, hayafai. Ili tuwe na pesa nyingi za kutosha ni lazima tunapozipokea, tunapozikusanya, lazima tuwe na nidhamu ya kuzitunza na kuzitumia. Ipo miradi mikubwa, naomba kwa sababu tunacho Kitengo chetu cha TISS kwenye ile miradi mikubwa ili kwenda kui-verify kama kweli hiyo pesa imetumika kama inavyotakiwa. Nashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha watu hawa kwa sababu wapo na kazi yao ni moja ni kuangalia upande wa pili, je, pesa hii imetumika vizuri?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, moja ya eneo ambalo mapato ya Serikali huwezi kuyapima, kuyaona vizuri na eneo hilo kila mwaka tumekuwa tukilalamika na ukiuliza watu wanatupiana mpira ni pale bandarini.

Mheshimiwa Naibu Spika, floor meter watakwambia imepona, lakini ukienda kwenye uhalisia Mheshimiwa Waziri wa Fedha eneo lile ni eneo muhimu kweli kweli kama litasimamiwa, kwa sababu mimi nia yangu ni kupata mapato mengi siyo vinginevyo, tupate mapato mengi ili kusudi pesa hizo ziweze kwenda kusaidia mambo mengine huko.

Sasa pale kwenye floor meter Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu pelekeni timu pale, TISS waingilie kati liko tatizo. Watakwambia wamechelewesha kushusha sijui, kuna linkage sijui, kuna temperature sijui, maneno matupu yale, liko tatizo kubwa sana pesa nyingi zinapotea pale. Ni lazima tufanye utaratibu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pesa hizi ziweze kukusanywa kama inavyotakiwa. Lakini ili tukusanye kama inavyotakiwa lazima pale watu wa TISS waende wakaangalie upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamb la pili nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mwaka jana tulileta mapendekezo kwako kuhusu hii michezo ya kubahatisha.

Mwanzo nafikiri hukuwa unanielewa vizuri, kama nilivyosema mimi nia yangu kwa kweli ni kutafuta namna ya kukusaidia wewe kutafuta vyanzo vingine vya mapato. Hata ukipata shilingi mbili, shilingi tatu, shilingi nne, ukiziongezea kwenye zingine ukakusanya huku na huku chungu chako kitajaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha mwaka jana ulikubali, na nimeambiwa kwamba kutoka kwenye bilioni 27 ambayo zilikuwa zimekadiriwa mpaka juzi hapa mmeweza kupata shilingi bilioni 64. Sasa kama tukisimamia vizuri na yale mapendekezo niliyokuletea kwa nia njema kabisa wala siyo vinginevyo, nia ni kukusanya lile eneo likisimamiwa vizuri eneo lile utatoka kwenye shilingi bilioni 64, shilingi bilioni 70 utakwenda mpaka kwenye shilingi bilioni 100 au zaidi. Lakini ni lazima hayo mapendekezo uyapitie vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ni technical kidogo na mtu anaweza akafikiri kwamba hivi hii Gaming Board ni nini, hivi nayo ina hela? Lakini ukienda Marekani, Las Vegas pale wanaishi lile Jimbo ni kwa sababu ya casino tu. Kwa hiyo, eneo hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana yale mapendekezo ambayo tumekuletea, uyaainishe vizuri ili yaje kwenye Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe tena hapo, michezo hii ili wote tupate kwa maana ya mchezaji, Serikali na Mwekezaji lazima zile asilimia uziweke vizuri. Kwa sababu utakuta kwa mfano, BIKO, TatuMzuka na mwingine Bet hawako kwenye Gross Gaming kwenye GGR, sasa kwa nini unawatenganisha wakati wao wote wanafanya mchezo mmoja. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ili tupate pesa nyingi za kutosha na ziende zikafanye kazi kwenye maeneo yetu hili eneo nalo nafikiri ungelitazama vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la mwisho kabla kengele haijalia. Naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, lakini mimi hasa kwenye hii skipper hii siyo mbaya sana kwa sababu itatupeleka kuzuri. Lakini liko tatizo hebu litazameni vizuri tusije tukafika pahala Mheshimiwa Waziri wa Fedha tukaanza kuulizana maswali kwa sababu tender yake ilitangazwa mwaka 2016, ikagota pahali ikapelekwa kwa AG ndiyo sasa imekuja tena sina tatizo nao, lakini kwa nini ilipelekwa kwa AG, AG alishauri nini lakini uwekezaji wao nani anaujua kweli kama ni shilingi bilioni 44 nani anaujua. Maana yake mtu anaweza akasema mimi niwekeza shilingi bilioni 44 na hapa nikikaa nitakusanya 66 nani anajua kwamba ni kweli uwekezaji wake ni shilingi bilioni 44. Ni jambo jema lakini ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukajiridhisha zaidi ili kusudi yasije yakajitokeza kama yale ya EFDs.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, naunga mkono. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu.