Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hii hotuba ya Waziri wa Mipango na Fedha. Kwanza, nashukuru kwa hotuba nzuri ambayo hasa ukiangalia imelenga kuwasaidia sana watu wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mambo mawili ya muhimu ambayo ndiyo kama maneno yangu ya utangulizi. Moja, natambua kwamba Serikali hii ni Serikali ya wanyonge, ni Serikali ambayo ingependa kuendelea kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, wala hilo halina ubishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuulize tu Mheshimiwa Waziri wa Mipango; swali la kwanza ni suala la watumishi waliokuwa wa kiwanda cha MUTEX. Hao watumishi toka waachishwe kazi ni zaidi ya miaka 20. Toka walipoachishwa kazi wamekuwa na madai yao ya kimsingi. Vile vile hawa watumishi wametoka katika mikoa mbalimbali. Wote mnafahamu kwamba fedha hizo zilitengwa, lakini hawajalipwa hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikilisema hili hata nakumbuka mwaka huu mwanzoni Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Musoma. Alipokuja, wananchi wa Musoma walimpokea kwa mabango, akaahidi kwamba atahakikisha wamepata mafao yao. Mheshimiwa Waziri anafahamu, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekwenda kwake mara nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii Serikali ya wanyonge inashindwa nini kumaliza tatizo dogo hili la watumishi ambao waliitumikia Serikali hii kwa uwezo wao wote katika kipindi chao kikubwa, lakini mpaka leo wanataabika wanatolewa kwenye nyumba hata walizokuwa wanaishi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati wa uhitimishaji kusema kweli, hili lazima Mheshimiwa Waziri alitolee maelezo ya kina ambayo wale wananchi labda yanaweza yakawatia moyo, ambayo yataonesha hizo fedha zao kama safari hii wanaweza kuzipata ili waendelee na maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine ni suala la kuwaondoa kazini watumishi hewa. Hakuna mwenye tatizo na hilo, lakini namna ya watumishi wengine jinsi walivyoondolewa. Ukiangalia katika Majimbo yetu mbalimbali, wako baadhi ya watumishi ambao waliondolewa tu kwa sababu ya upotoshwaji. Mfano, kuna mtu ambaye alisoma darasa la saba, baada ya hapo akaajiriwa, akaendelea kujiendeleza, akapata Certificate, akapata Diploma, mwingine mpaka akapata Degree. Wakati ule wanajaza zile taarifa zao binafsi, alipofika kwa Afisa Utumishi pale akaambiwa wewe sasa elimu yako siyo ya darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu, elimu yako siyo ya darasa la saba andika kwamba una elimu ya kidato cha nne. Leo huyo tumemwondoa kazini, tumeacha mtu wa darasa la saba. Hivi kweli ukiangalia tu katika ule utendaji wa kawaida, umemwacha wa darasa la saba halafu umetoa mtu ambaye ni graduate. Hao leo wanahangaika mtaani, hawana pa kwenda, wala hawajui wafanye nini, wala hawajui hatima ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani hii Serikali yetu ambayo ni Serikali sikivu, hebu itoe majibu sahihi na ione namna gani ya kuwasaidia hawa watu ambao wengi wao walipotoshwa. Badala ya kusema kwamba amemaliza darasa la saba akaambiwa kwamba kwa sababu amejiendeleza, basi elimu yake ni zaidi ya darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda na watu wengi kusema kweli tunalizungumzia ni kwamba nchi yetu kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri, uchumi wetu umekua. Tukija kwenye hali halisi katika kuangalia wananchi wa chini, wale wananchi wa kawaida katika maisha yetu ya kawaida, huo uchumi hatuuoni. Hiyo nami nakubaliana kwamba inawezekana uchumi wetu umekua katika zile sekta ambazo haziajiri watu wengi. Sasa kwa sababu hiyo, ndiyo maana kila mara tukiangalia hali ni ngumu. Sasa kwa sababu, sisi Wabunge jukumu letu ni ushauri, nami napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri Mpango, kama ataona ushauri unafaa, basi waweze kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, sifahamu ni kwa nini Watanzania wengi hatupendi kulizungumza hili. Kusema kweli suala la uzazi wa mpango ni suala ambalo halikwepeki kama tunahitaji kukuza uchumi wetu. Kwa sababu, ukiangalia fedha nyingi sasa pamoja na kuzipeleka kwenye huduma za jamii, lakini inaonekana kule nako hatujafanya kitu. Mfano, ukiangalia kwenye afya peke yake zimetoka shilingi bilioni thelathini na kitu, leo tunazungumzia shilingi bilioni mia mbili na kitu, lakini ukienda kule hospitali, bado dawa hazitoshi, bado huduma za afya hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule, mfano kwenye shule moja, katika Kata yangu moja, darasa la kwanza peke yake wanaandikishwa watoto wasiopungua 800. Kwa hiyo, ni kwamba hata kama tutaongeza bajeti, bado maisha yataendelea kuwa magumu kwa sababu fedha nyingi tunaendelea kuzimalizia kwenye huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba hebu tuone namna ya kuli-address. Maana katika nchi nyingine, asilimia kubwa ya watu ni wale wenye manpower ya kufanya kazi, lakini katika Tanzania asilimia 60 wote ni watu ambao ni tegemezi. Kwa hiyo, tunadhani
kwamba bila kuli-address hili litaendelea kutupa tabu na kila siku fedha zitaonekana hazitoshi na uchumi wa nchi bado utaendelea kuwa ambao siyo mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni ushauri, wote tunakubaliana kwamba siyo chini ya 60% ya Watanzania ni wakulima. Kama hivyo ndivyo, nini kifanyike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie yale mazao ambayo kwanza masoko yake yanapatikana. Nami nije na mfano wa zao moja tu la mpunga. Zao hili ukiangalia katika nchi zote zinazotuzunguka, ukienda Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo na Zambia ni watu ambao wanahitaji mchele. Kwenye suala la kilimo cha mpunga kinahitaji maji, mbolea na hakina majira. Sasa kumbe kitu ambacho tungeweza kufanya, tungeweza ku-identify katika mabonde tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewapeleka huko JKT wakawapeleka vijana huko, wale vijana wakafanya kazi, watavuna ule mpunga. Kwa hiyo, tungekuwa na masoko ya uhakika ambayo tunadhani kwamba wale vijana watakuwa wamejipatia ajira na ni kwamba maisha yao yataboreka kuliko hivi ambavyo tunaendelea kuhangaika na bado maisha yetu au maisha ya watu wetu yanaendelea kuwa magumu. Kwa hiyo, kama tutaona ni jambo jema, basi na lenyewe tukilichukua ni imani yangu kwamba litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naona kama bado hatujajipanga vizuri sana ni elimu. Leo ukiangalia kwenye upande wa elimu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nimalizie tu kwa kusema kwamba, naomba mwisho Serikali ione uwezekano wa kulipa wale Wazabuni wote ambao wamei-supply Serikali, wametusaidia, lakini mpaka leo wale watu wanadai na hawajawahi kulipwa. Kwa hiyo, Serikali iweze kuwalipa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante.