Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa mpango mzuri wa maendeleo uliotuletea ikiwemo kuipa kipaumbele Sekta ya Kilimo. Kwenye mpango Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa pembejeo, masoko na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika ukulima wa mbogamboga. Katika kilimo hiki cha mbogamboga sasa hivi vijana wamehamasika sana na wakulima wadogo hujiunga katika vikundi au mmoja mmoja katika kilimo hiki cha mbogamboga. Kwa bahati njema sana mazao ya mbogamboga yanahitajika ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni moja usafiri wa ndani kuhakikisha mazao haya yanafika kwa wakati katika maeneo husika lakini pia usafiri wa nje wakati wanapopata tenda za kusafirisha mazao hayo nje ya nchi kunakuwa na tatizo la usafiri kwa kuzingatia kwamba mazao mengi ya matunda na mbogamboga yanatoka kwenye Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na kwingine. Ni vyema sasa Serikali ikaimarisha Kiwanja cha Ndege cha Songwe ili wakulima na wasindikaji na wazalishaji wa maeneo hayo wapate urahisi wa kusafirisha mazao yao nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika ukulima huu wa mbogamboga napenda niongelee kuhusu suala la vifaa vya kilimo na hususani vifaa vya kilimo vya mbogamboga kama green house. Vifaa hivi vya kilimo vinatozwa VAT vya asilimia 18 na kwa maana hiyo sasa mkulima mdogo au kijana aliyemaliza masomo yake anataka kujiingiza kwenye ukulima huu wa green house, vifaa hivi vinakuwa ni vya bei kubwa sana. Hivyo, anashindwa kuwekeza kwa maana ya vifaa vyenyewe kwamba vifaa vya ujenzi, vifaa vya mipira ya kumwagilia na vinginevyo vinakuwa na gharama kubwa sana ambapo vijana na wakulima wadogo wanashindwa. Naomba Serikali iliangalie hili kwa upana ili kupunguza VAT hii ya asilimia 18 kwa vifaa vya uzalishaji wa matunda green house na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo na vikundi vidogo vidogo vya wakulima imekuwa ni tatizo kupata mikopo kutokana na kwamba hawana dhamana yoyote ambayo itawalinda kupata mikopo hiyo. Naomba sasa Serikali itafute njia bora zaidi na nyepesi zaidi ambayo itakuwa kama ni dhamana kwa vijana wetu na vikundi vyetu vidogo vidogo vya wakulima kuweza kukopesheka. Kwenye sekta hiyo ya kilimo kuna tatizo pia kwenye kodi kubwa VAT ya vifungashio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vMheshimiwa Mwenyekiti,ifungashio vya mazao ya kilimo na mbogamboga imekuwa na VAT kubwa ambapo wakulima wanashindwa sasa kuhimili vile vifungashio vyenye ubora ambavyo vitaweza kusababisha kusafirisha mazao yao nje ya nchi na badala yake wanajikuta mazao yao tunauziana wenyewe hapa ndani ya nchi na tunakosa soko la nje lakini pia tunakosa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mheshimiwa Waziri alizingatie kwenye vifungashio pia vya mazao ya kilimo na mbogamboga. Kwa sababu sasa hivi wawekezaji wetu wa kilimo wanaagiza vifungashio kutoka nje ya nchi na kuviingiza Tanzania. Tufanye mipango sasa vifungashio hivi vizalishwe ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tozo nyingi ambazo zinamfanya mwekezaji kuwa na mlolongo mkubwa wa tozo mbalimbali. Naiomba Serikali sasa iziangalie tozo hizi ziweke mazingira wezeshi itakayomfanya mwekezaji awe analipa eneo moja tu na kumaliza shughuli zake na kuanza kuwekeza, tujenge mazingira wezeshi kwa wawekezaji wetu wa nje na ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapo hapo ssa hivi naigusa sekta ya maziwa. Sekta ya maziwa inatupa lishe lakini pia inatupa afya bora na kwa kuzingatia kwamba maziwa yanapozalishwa yanakuwa na matatizo na mambo madogo madogo ambapo tunahasishwa sasa tunywe maziwa yaliyosindikwa ambayo ndiyo yenye ubora kwa afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hilo kwenye uwekezaji wa sekta ya maziwa nako pia kuna mlolongo mkubwa wa kulipa vitu mbalimbali kama hiyo mambo ya fire, VAT na vinginevyo ni vingi sana mpaka wazalishaji wa maziwa wanashindwa sasa kuhimili vile vikwazo vidogo, naomba hizi changamoto ndogo ndogo Serikali iziangalie kwa hawa wawekezaji wa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye sekta hiyo ya maziwa ukiondoa hayo mlolongo wa mambo hayo mambo yanatakiwa kulipa, kwenye kuwekeza maziwa, maziwa yanayozalishwa kwa muda mfupi hayatozwi VAT lakini ukizalisha maziwa ya muda mrefu yanatozwa VAT. Kwa maana hiyo sasa wawekezaji wanawekeza kwenya maziwa ambayo ya muda mfupi ambayo hayatozi VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema sasa tukaliangalia hili ili wawekezaji wetu wawekeze maziwa muda mrefu ili waweze kusafirisha nje ya nchi kwa sababu yatakuwa yanadumu kwa muda mrefu na tutapunguza lile tatizo la sisi kuagiza maziwa kutoka nje na kuyaingiza ndani ya nchi kwa sababu ya kwetu sisi ni ya muda mfupi yake yanatoka nje ya muda mrefu, hili nafikiri tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya maji kwa kuwa tuliomba tuongezewe Sh.50 kwenye lita ya mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Maji, nashauri Serikali kama hili haliwezekani tutafute njia mpya njia mbadala ya kuongezea huu Mfuko wa Maji ili tuweze kutatua matatizo ya maji ndani ya nchi yetu. Kilio kikubwa kimekuwa kwenye maji na tumeweka kwenye mpango kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji tutahitaji maji, tutahitaji mabwawa, tutahitaji visima. Kwa hivyo ni vyema pia tukaliangalia ili kuongeza kwenye Mfuko wa Maji ili tuweze kujenga hayo mabwawa, visima na miundombinu mingine ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya uvuvi, ni vyema pia Serikali ikaiangalia kwa upana wake sekta ya uvuvi. Sekta ya uvuvi ni eneo moja ambalo litaipatia Tanzania fedha za kigeni, litaipatia ajira vijana wetu pia tutapata lishe bora kwa kula samaki ambapo watakuwa wengi tunawavua hapa nchini. Pia tujikite katika uwekezaji, naomba Serikali, hii bandari ya uvuvi ipewe kipaumbele ili imalizike na baada ya kumalizika kwa bandari ya uvuvi, Serikali sasa tumeshajikita katika kununua ndege sasa tujikite tena pia Serikali kwenye kununua meli ya uvuvi. Naipongeza Serikali kwa hilo, tumenunua ndege sasa tujikite tena tujipange, tujifunge mkanda, tununue meli ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la umeme. Umeme ni uchumi, umeme ni siasa na umeme ni usalama. Huduma hii ya umeme katika bajeti ya mwaka jana tulizungumzia kuhusu suala la umeme Zanzibar baina ya ZECO na Shirika la Umeme TANESCO. Tunaomba sasa huu mchakato umalizike kwa kuwa mtumiaji wa umeme wa Zazibar inabidi alipe VAT mara mbili kwa sababu tukinunua umeme tunalipa VAT, mtumiaji mdogo analipwa VAT sasa ni vyema sasa VAT hii iwekewe mikakati iwe inalipwa sehemu moja tu ili kumpunguzia mzigo mwananchi mdogo ili asielemewe na mzigo na kwa sababu hii ndio maana kumekuwa na malimbikizo makubwa sana ya umeme kule Zanzibar kwa sababu suala hili bado halijapita ufumbuzi wapi VAT hii ilipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye huduma za mama, afya na mtoto; naipongeza Serikali kwa kulipa kipaumbele suala la afya ya mama na mtoto. Pia naiomba Serikali kila kwenye kituo cha afya basi iweke chumba cha kujifungulia mama na mtoto na chumba pia cha kupumzika baada ya kujifungua ili kuweka usalama wa mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kusamehe kodi mbalimbali za kilimo ikiwemo mambo ya ngozi na mambo mengine ya kilimo. Hapa naipongeza Serikali sana kwa kuliona hili, lakini pia nataka Serikali itupie macho katika haya mambo niliyoainisha kwenye sekta ya maziwa, sekta ya mbogamboga na sekta nyingine za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.