Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na kuwakumbusha Watanzania wote Waislam kwa Wakristo tusome Luka 8:18. Luka 8:18 inaelezea juu ya mambo ya mali, aliyenacho ataongezewa na yule asiyekuwa nacho hata kile kidogo ambacho anahisi anacho na chenyewe atanyang’anywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana sana kusema maneno haya ya utangulizi wa kwenye Biblia kwa sababu ni wazi kabisa sasa hivi Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo inaongoza nchi hii imeamua kusimama kwenye huu mstari Luka 8:18 na nina mifano ya kuhalalisha kwa nini nimeamua kusema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti ya Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango kule ndani hakuna sehemu ambako amekwenda kuonesha kwamba watumishi wote wa kada zote watakwenda kuongezewa mishahara yao. Pamoja na kukamilisha masuala ya uhakiki na walisema kwamba baada ya uhakiki mara moja watakwenda kuboresha mishahara. Juzi hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu amesimama anasema suala la nyongeza ya mishahara itabaki kuwa siri, itafanywa kimya kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize bei za mazao na bidhaa nyingine zinapanda, tumeona kabisa kwamba hata kwenye shule ada zinapanda, lakini watumishi wao hawaongezewi mishahara wakiwemo na watumishi wa Bunge wanaotusaidia hapa ndani mishahara yao haipandishwi sasa hivi kwa mwaka wa pili au wa tatu kwa kisingizo cha uhakiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kabisa wale wachache ambao walikuwa wanatakiwa kupandishiwa mishahara yao walipewa barua za kupandishiwa madaraja wakiwemo Polisi na Wanajeshi. Ukienda Jeshi la Zima Moto ni kilio, wamenyanga’anywa ile mikataba yao ya mwanzo, wiki mbili tatu zilizopita wakati tunakuja kwenye Bunge la Bajeti wamepewa barua nyingine wanaambiwa vile vyeo vyao vya awali vimesahaulika wanaanza kuhesabiwa toka juzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Rais anashangaa, anamwambia hapa Mama Jenista Mhagama kwamba eti anahisi anaajiri vilaza ndiyo maana watu hawafanyi kazi vizuri huko mtaani, hapana na sidhani kama alimjibu. Nataka leo nimwelekeze amwambie Rais hawa watu wamekuwa demotivated kwa sababu hawapati stahiki na mishahara yao, hawafanyi kazi kwa moyo kama ambavyo ikuwa zamani, hili ndiyo tatizo pekee lililopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa mama Jenista kama inawezekana awasiliane na Rais amweleze kwamba hawa watu wamekuwa demotivated wanataka wapandishwe vyeo na mishahara ili waweze kufanya vizuri. Kuna watumishi wa umma wengi wamebaki kwenye vilio sasa, Walimu na wengi waliobakia wanasikiliza Bunge ili tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu yetu ya awali kama Wabunge yalikuwa ni kuisimamia, kuielekeza na kuishauri Serikali, lakini hapa tumeona sasa hivi mtindo huku ndani na hasa zaidi ndugu zetu wa Chama cha Mapinduzi wanavunja sana Kanuni ya 154. Hii kanuni ya 154 inaruhusu kabisa kutoa pongezi za aina yoyote, anayetakiwa kufanya jambo hili kwa niaba ya wote Wabunge ni Mheshimiwa anayekuwepo kwenye Kiti siku hiyo pale. Sasa imekuwa kama utamaduni ili uweze kuonekana utaanza kumsifia Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani wakati sijawa Mbunge nilifikiri hili jambo linakwendaje; unanisifia wee halafu mwishoni unaanza kumwambia lakini hata hivyo rekebisha hii. Twendeni kwenye point tuisimamie na tuishauri Serikali na ndiyo liwe lengo letu wote. Wote tunatamani kupongeza lakini wasiopongeza wanaonekana wabaya kwa sababu wengine wanapongeza na ndiyo tumefikia hapo, hii ni double standard. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa pia niongee leo ni masuala machache kwa ajili tu ya kuishauri kama ambavyo nimeanza toka mwanzo. Nimenukuu hapa Luka 8:18 na ndiko walikosimama Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Twende kwenye gesi Mtwara, mpaka sasa hivi gesi ya Mtwara inatumika kwa asilimia saba tu, wale Wawekezaji wa Maurel and Prom wamekuja kulalamika kwamba wao wanashindwa hata kurudisha mtaji wao kwa sababu gesi ile haitumiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeruka imeachana na gesi ambayo ingekwenda kuwanufaisha watu wa Mtwara, wamekimbilia kufanya mradi wa Stiegler’s Gorge ambao thamani yake halisi mpaka utakapokuja kukamilika haifahamiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna nia ya kupinga huu mradi lakini kwa nini tusikamilishe miradi iliyopo mwanzoni ya kimaendeleo inayoweza kusaidia ili mambo mengine yafanyike. Hiyo pesa inayokwenda Stiegler’s Gorge ingekwenda kutumika kusaidia kwenye miradi ya maji, kujenga zahanati na kufanya shughuli zingine tukaokoa maisha ya watu wetu tukaongeza life span. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli (Standard Gauge). Reli ya Tanzania kulikuwa kuna reli inaitwa Reli ya Kusini ilikuwa inaanzia Mtwara inapita Newala, inakwenda Masasi inanyooka kwenda kule chini. Hii reli ingekuwepo mpaka sasa hivi ingetusaidia kudumisha au

kupata chuma cha kujenga hiyo reli ya standard gauge hapo katikati, kwa sababu Mchuchuma na Liganga uwekezaji wake sasa hivi ungekuwa umeshakwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeachana na hiyo, tunatumia forex nyingi kununua chuma kwa ajili ya kutengeneza reli na tunasema hapo tuna miradi mingine ya kimkakati, huko Stiegler’s Gorge tunakoongelea inatakiwa na kwenyewe ipelekwe chuma, kwa nini Serikali isifikirie kutengeneza Mchuchuma kwanza kwa hizo pesa zote tena kwa haraka tupate chuma yetu wenyewe, nyingine tuiuze nje na nyingine tutumie kwenye miradi yetu ya kipaumbele. Matokeo yake wao wanaamua kuingiza tu (import) ndiyo maana shilingi inashuka kila siku, hii ni biashara ya kawaida kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ambalo kwa kweli hili kwetu ndiyo lenyewe. Hapa nina makaratasi mengi tu na Mheshimiwa Omary Mgumba nimwombe kabisa atuombe radhi watu wa Mtwara kwa sababu Mgumba kilichomleta Mtwara ilikuwa ni biashara ya korosho, walikuwa wanafanya kazi na kampuni moja inaitwa Olam Tanzania Limited, hawa ndiyo walikuwa watu wanaowafanya watu wa Mtwara waendelee kubaki vile wanavyobaki kwenye korosho kwa sababu walikuwa wanajua wananufaika na nini. Ndiyo maana anakuja kutetea, anawatetea ambao walikuwa waajiri wake na hao ndiyo waliotufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya export levy ipo hapa ndani, karatasi hizi ninazo na hizi karatasi nitaku…

T A A R I F A . . .

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini muda wangu umeutunza. Nataka tu nikwambie wakati tukiwa Wabunge wageni kabisa mwaka juzi, Mheshimiwa alinikutanisha na Meneja Mkuu wa Olam duniani, sijui alimtoa wapi tukakutana hapo nje, sasa ndiyo anaoendelea kuwatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya export levy ninayo hapa na nitampa pale Waziri, nataka nisome tu mistari michache nikueleze. Wanasema hivi changamoto hii ilipata utatuzi kupitia maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika tarehe 12 mpaka 14 Aprili, 1994, Mkoani Mtwara katika Wilaya ya Masasi. Mkutano huu pamoja na mambo mengine uliazimia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa walisema kuweka mikakati ya kuwa na utafiti endelevu wa zao la korosho. Pia kuwa na usimamizi wa uratibu mzuri wa tasnia ya korosho nchini; kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora na kuendeleza ubanguaji wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali inakuja hapa pesa zetu sisi tunadai ili tukafanye mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikuwa Attorney General, kwa hiyo naamini kabisa unafahamu na ndiyo maana ulisema historia hii unaifahamu. Ahsante sana Mheshimiwa Chenge kwa kunisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya tafiti ambazo zipo, nilimshauri mwaka jana hapa Waziri wa Viwanda kwamba tunaomba tufanye utafiti na jana tumekaa hapa na wadau wanaozalisha pombe na vitu vingine wanalalamika upatikanaji wa alcohol. Nilikwambia mabaki yanayobaki kwenye korosho na ndiyo maazimio yao pale ikiwemo pamoja na zile kitu kwetu tunaita kochoko inapatikana kule ndani nipah, ukiamua kuitengeneza vizuri unapata ethanol, methanol na vitu vingine mle ndani ili kuwaongezea wakulima wale kipato. Huu utafiti ulikuwa unafanyika Naliendele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za kuondoa hiyo export levy ya kwanza kabisa inasema upotevu mkubwa wa idadi ya mikorosho nchini Tanzania. Hapa karibuni tumeona Serikali inawasisitiza mikoa mingine waanze kulima korosho wakimemo Tumbi, Mkuranga Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Dodoma Mpwapwa, Tabora, Singida na mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niwaambie Watanzania hawa ambao wanaingizwa huu mkenge, zao la korosho sisi ndiyo limetufanya wakazi wa Mikoa ya Kusini tuwe maskini, lakini tulikuwa tunavumilia, tukagundua kwamba tunahitaji pesa ili tuweze kuliendeleza. Serikali ya

Chama cha Mapinduzi inakwenda kutoa mtaji wetu wa kuendeleza zao hili, sasa wanataka kuingiza mkenge Watanzania wasiohusika na jambo hili. Hili jambo ni la Wamakonde watuachie wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hili tunalosema, wazee wetu akina Mzee Nandonde wakati huo walikuwa wanaomba Kusini basi tutengwe na Tanzania iliyobaki ambayo tunafikiri maendeleo yao yanakwenda kwa kasi, tuishie kuna sehemu moja hapo panaitwa Kinyonga, Kilwa. Kule tunajitosheleza, tuna gesi na korosho zetu tutajua wenyewe namna ya kujiendesha pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pesa ya export levy ilikuwa na mgawanyo wake maalum ambao upo kisheria, asilimia 35 inakwenda Serikalini na asilimia 65 ilikuwa na matumizi yake, karatasi hii hapa inayoonesha matumizi mbalimbali ya pesa hiyo asilimia 65, mpaka sasa hivi Serikali wametoa bilioni 10 katika bilioni 211 tunazoidai Serikali hii. Tunataka Mheshimiwa Dkt. Mpango akija pale atueleze hiyo balance inayobakia yote wamepeleka wapi na kufanyia nini wakati wenyewe tunaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tunakoelekea sasa ni kubaya na ndiyo maana hapa juzi Mheshimiwa Bwege alisema tunakwenda kuandamana na tunakwenda kuandamana kweli. Nitaongoza maandamano Jimbo la Ndanda la kudai haki na stahiki yetu kwa sababu tunadhulumiwa na tunaonewa. Kila kidogo tunachojaribu kukikusanya kwa nguvu zetu Serikali inakwenda inapora, wanaleta sheria hapa wanataka watudhulumu. Basi kwanza walete pesa tuliyonayo, halafu baada ya hapo wao walete huo utaratibu wao wa kutaka kubadilisha hii sheria ili tuone mwisho wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii document nitaipa hapo Kamati yako. Kati ya mambo ambayo yatakwenda kufeli huko mbele ni pamoja na taasisi itapoteza wafanyakazi Watafiti waliobobea kwenye utafiti wa zao la korosho.

Tanzania ambako tunazalisha maeneo mengi, kati ya hao watafiti pale Naliendele Chuoni wameajiriwa wafanyakazi 126 kati ya hao wafanyakazi 71 wameajiriwa kwenye programu ya utafiti wa korosho ambapo mishahara yao inatokana na cashewnut levy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hapa Mheshimiwa Mgumba anakuja anasimama anataka kutetea wanaomtuma anataka kutuaminisha kwamba… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)