Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kama ambavyo wengine wamesema kwamba nia hii inaweza kuwa njema kabisa, lakini njia za kwenda kufikia kwenye utekelezaji wa hii nia ndiyo ambazo watu wanajaribu kuzisema ili tuweze kurekebisha. Ukienda kwenye Majiji, kati ya vigezo ambavyo vinatakiwa ni pamoja na kuwa na idadi ya watu fulani. Kwa mfano, lazima uwe na watu wasiopungua 500,000 ili uweze kutengeneza jiji kama kigezo. Ukija Jiji la Dodoma hili ambalo sasa hivi tunaenda kuliita jiji ni kati ya Majiji ambayo yanaanza kuongoza kwa vituko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza ndio amemchagua Meya wa Jiji la Dodoma, kitu ambacho hata kisheria hakipo. Kwa utaratibu, Meya huwa anachaguliwa na Madiwani wenzie kutokana na Baraza la Madiwani, lakini hapa tumeona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangaia hata presenter wakati mwenyewe Mheshimiwa anaongea pale, he was not happy, yaani hafurahii kile anachokifanya, ni kama amesukumwa au kuna watu wanamlazimisha kukifanya au kuna kitu wanakitafuta ili kuweza kuwafurahisha watu fulani wakati kimsingi vigezo havijatimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikiliza vizuri hapa Mheshimiwa Mtulia hapa wakati anachangia, wote tungeelekea kwenye mwelekeo ule wa Mheshimiwa Mtulia ili kuweza kupata Jiji bora la kihistoria na la mfano. Viongozi wanafanya jambo la maana, lakini tunakuja hapa ni kupongezana na kusifiana kwenye vitu ambavyo havijafanywa vizuri. Hili siyo jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti ulifanyika, wakasema ili kufanya Dodoma iwe mji au Makao Makuu ya nchi kunatakiwa 40 trillion ili kuliboresha hili jiji na wakashauri kwamba hii transition ifanyike kwa muda wa miaka kumi angalau wafikie milioni nne kutokana na udogo na huu ufinyu wa bajeti yetu.

Sasa ukiangalia sasa hivi hata hawa watumishi…

T A A R I F A . . .

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo unaona hali iliyoko hapa, hata huyo Meya mwenyewe uteuzi wake ulipitia kwa Mheshimiwa Simbachawene wakati huo ni Waziri wa TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona ile namna ya kutaka kubebana bado inaendelea wakati utaratibu haujaandaliwa. Anatakiwa kuwa Meya ambaye anatokana na uteuzi kwenye kata. Diwani wa Kata na sio mtu wa kuteuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona watu wanaoteuliwa, usumbufu wanaotuletea, hata humu ndani ya Bunge, wanaoteuliwa wengi ndiyo ambao wanatuyumbisha kwa sababu wanafanya mambo tofauti na mahitaji ya watu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii nia inaweza kuwa njema lakini njia tunayotaka kutumia kwenda kutekeleza hii nia siyo nzuri. Tulete hiyo sheria ibadilishwe, zifuatwe taratibu zote za kutangazwa kwa Jiji, vinginevyo kule kote ambako wana nia ya kuwa na Majiji na Serikali hii ndiyo ambayo ilisema tunashindwa kuongoza, tunashindwa kupanua maeneo ya kijiografia kwa sababu ya kubana matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuangalie namna ambavyo sisi tunataka kwenda huko mbele, badala yake sasa yote haya yanayotokea ya kuteuliwa tutalazimisha jambo; sasa hivi ukija kuangalia hapa, hata omba omba wanashindwa kutoka Dar es Salaam kurudi Dodoma kwa sababu hapa hapajakaa vizuri bado kwa ajili ya zile kazi zao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia upande wa pili, Watumishi wa Umma wanatakiwa wahamie hapa, lakini huko kuna migogoro. Pamoja na kwamba wake zetu, wengine waume zao ni watumishi wanatakiwa waje kujiunga nao Dodoma, lakini Dodoma bado hapajakaa kuweza kutangazwa kuwa jiji angalau tu kwa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna uhaba wa shule, kuna uhaba wa miundombinu, maji, umeme, vinakatika. Juzi tumetoka kulalamika hapa masuala ya umeme, tunaambiwa transfoma zilizopo haziwezi kuhudumia Dodoma kama Jiji. Haya leo tunataka watumishi wote wa umma wahamie hapa; wale wote wakijazana hapa vyoo vyetu vitaziba. Hali iliyoko Dar es Salaam itakuja kujitokeza na hapa tena. (Kicheko)

Kwa hiyo, kimsingi lazima kwanza tuboreshe, tuhakikishe hapa hakuna haja ya kukimbilia hivi vitu, sisi tunakubali watumie muda mrefu kufanya Dodoma liwe Jiji, ibaki kuwa Makao Makuu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naombe Serikali irudi tena, Mheshimiwa Simbachawene arudi akatafakari, atafute ule utafiti uliofanyika aipelekee Serikali kwamba jamani hebu boresheni kabla hatujaamua kukurupuka na kwenda kutekeleza hili jambo kabla ya wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kujidhalilisha tukianza kujilinganisha na Nigeria, mara sijui Somalia na kwingine kote. Tuangalie kwanza mahitaji ya wakati kabla ya hivyo vitu havijaja mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.