Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nitumie fursa hii kukushukuru sana wewe kwa kuendesha vizuri mjadala huu wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2018/2019 ni dhahiri kabisa ule usemi wa wazee wetu kwamba zipo kazi hatumwi mtoto, naona tangu jana na kwa sehemu kubwa leo Kiti amekalia mwenye kiti. Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua michango iliyotolewa na Kamati ya bajeti chini ya mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Jitu Soni (Mbunge), pia Wabunge wote kabisa waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 56 wamechangia hoja niliyoiwasilisha na kati ya hao 35 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 21 wamechangia njia ya maandishi. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji (Mbunge), huyu ni Mama mahiri kweli, namshukuru kwa kunisaidia kufafanua hoja nyingi ambazo zimetolewa toka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni mizuri sana, hata ile ambayo ilikuwa inaegemea zaidi kwenye mitandao isiyo na uhakika bado nayo ni michango tu tunaipokea. Nitapenda nitoe ufafanuzi na majibu ya baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote. Kwa wingi wa hoja na pia ukweli kwamba hoja nyingi ni za kutusaidia kuboresha kazi zetu kwa mwaka ujao wa fedha Bunge lako tukufu litakapotupitishia bajeti tuliyoomba, basi nitaomba nitoe ufafanuzi wa hoja chache kwa sababu pia ya muda. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wewe Mheshimiwa Spika kwamba majibu ya hoja zote ambazo zimetolewa hapa na Waheshimiwa Wabunge tutaziwasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba nianze na hoja moja moja. Nilipenda nianze na hoja iliyotolewa mwanzo kabisa wa mjadala kuhusu mashine za EFD kutofanya kazi na kwamba Serikali inapoteza mapato. Kwa umuhimu wake naomba nianze nayo hii.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kuanzia tarehe 11 Mei, 2018 mashine za kielektroniki za kukusanya mapato hazikuwa zinafanya kazi kutokana na hitilafu ya mfumo ambayo ilitokana na kuharibika kwa kifaa ambacho kinatunza na kuchakata taarifa za wafanyabiashara. Hitilafu hiyo ilisababisha wafanyabiashara wakashindwa kutuma taarifa za mauzo yao ya mwisho wa siku tunaziita “z-report” kwenda TRA. Labda tu kwa taarifa ni kwamba hizi mashine za EFD zimetengenezwa kwa namna ambayo kama usipotuma taarifa hizo kwa siku nne mfululizo basi mashine zinagoma kutoa risiti.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutokea tatizo hili wataalam wetu wa Kitengo cha IT cha TRA kimefanyia kazi changamoto hiyo, kwa kweli wamefanya kazi usiku na mchana na hadi sasa bado tunaendelea kulifuatilia jambo hili kwa karibu na mpaka ilipofikia tarehe 1 Juni, 2018 mfumo huu vijana wetu waliweza kuurejesha kwenye hali yake ya kawaida na mfumo ukatengemaa kabisa na kuanza kufanya kazi kama ilivyokuwa awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lilokuja kuibuka ni kwamba aidha kwa kujua au kwa maksudi baadhi ya wafanyabiashara walizima kabisa mashine zao hata baada ya mfumo kuwa umetengemaa, hivyo mashine zikashindwa kupokea majibu ya taarifa kutoka kwenye mfumo wetu pale kwenye saver kuu na mamlaka ya mapato.

Mheshimiwa Spika, wito wangu kwa wafanya biashara ni kwamba warejee kutumia mishine za EFD kikamilifu na kutoa taarifa kwa mawakala wa EFD au TRA pale ambapo mashine zao zinakuwa hazifanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, toka jana nimetoa maagizo kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ahakikishe kwamba maafisa wetu wote wa Mamlaka ya Mapato nchi nzima wanaondoka ofisini na kuwatembelea wafanyabiashara wote wanaopaswa kutumia mashine za kielektroniki ili kuhakikika kwamba zinatumika ipasavyo. Vilevile nimetoa maelekezo kwamba barua zote ambazo zilikuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato kabla ya leo tarehe 4 Juni, 2018 ambazo ziliwaruhusi wafanyabiashara waendelee kufanya mauzo bila kutumia mashine za EFD kwa kisingizio kwamba hizi mashine hazifanyi kazi, mpaka wengine kataratasi wamezifanyia lamination kama vile tatizo hili nimekuwa ni la kudumu, basi nawaambia rasmi kwamba hizo karatasi hazina uhalali kuanzia sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hitilafu yoyote ya kiufundi itolewe upya, Mamlaka ya Mapato na kwa hawa vendors wa hizi machines kwa ajili ya utatuzi wa haraka.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile nawasihi sana wafanyabiashara tunawapenda sana, tunawaomba waingize kumbukumbu za mauzo ambazo walizitunza nje ya mfumo wakati hitilafu ilipotokea, sasa waziingize na niwakumbushe tu kwamba hairuhusiwi kwa mfanyabiashara yoyote kutoa risiti zenye thamani tofauti na kiasi halisi ambacho kimelipwa na mteja. Zipo petrol station unakwenda unanunua mafuta, unakuta wamekata hela uliyotoa, nawakumbusha tena kwamba ni kinyume cha sheria na adhabu kali itatolewa kwa mfanyabiashara yeyote atakayekiuka maelekezo haya.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilihusu Tume ya Mipango na hapa tulishauriwa kwamba irejeshwe, Fungu 66 pia lirejeshwe, na kazi zilizokuwa zinafanywa Tume ya Mipango ziendelee kufanywa chini ya ofisi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hati ya Majukumu ya Mawaziri (The Ministers’ Assignment of Ministerial Functions Notice, 2016) iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mojawapo ya majukumu yaliyokasimiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango ni majukumu ya iliyokuwa Tume ya Mipango, Mheshimiwa Rais amepewa mamlaka haya kwa mujibu wa The Ministers’ Discharge of Ministerial Functions Act Cap. 299 ambayo ilipitishwa na Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba baada ya majukumu kuhamishiwa Wizara ya Fedha na Mipango, tumeendelea kusimamia na kutekeleza majukumu yote ya yaliyokuwa yakitekelezwa na Tume ya Mipango, ndiyo maana tutawasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa Fedha, na shughuli nyingine zote zimendelea kama kawaida. Aidha, ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi, watumishi zaidi ya 50 waliokuwa Tume ya Mipango wamehamishiwa Wizara ya Fedha na Mipango ili kuiwezesha Wizara kuwa na watumishi ambao wana weledi na uzoefu kwenye shughuli ambazo zilikuwa zinatekelezwa na Tume na kulinda institutional memory.

Mheshimiwa Spika, vilevile kama nilivyoeleza kwenye aya ya 3.1.2 ya bajeti ya Wizara ambayo niliwasilisha jana, muundo wa Wizara uko katika hatua ya mwisho ya kuidhinishwa na mamlaka husika na tumefanya mapitio ili kuunda, Division ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa ambayo itaongozwa na Kamishna na itakuwa na kifungu chake kwa ajili ya shughuli za kibajeti.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nilieleze Bunge lako tukufu maana kulikuwa na hoja kwamba sasa hata kazi za mipango hivi hazionekani na Wizara inajielekeza kwenye mambo ya fedha peke yake na kutafuta mapato, hili siyo kweli. Naomba nisisize tena kwamba katika kuandaa bajeti na mipango ya maendeleo bado tunaongozwa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao nimeshika hapa, 2016/2017 mpaka mwaka 2020/2021. Miradi hii inayosemwa kwamba haikuwepo kwenye mipango siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mpango huu, ukianza na ukurasa ule wa 80 miradi hii yote hii imo. Kwanza niseme kuna kuimarisha upatikanaji na uhakika wa nishati ya umeme vijijini na mijini, pia kuna kipengele cha ununuzi wa ndege mpya na kufufua usafiri wa anga. Hali kadhalika ukienda ukurasa unaofuata kitabu hiki kinabainisha wazi kabisa, kwamba lengo letu upande wa nishati ni kuongeza uzalishaji wa umeme, kutoka megawati 2,899.3 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo maji, gesi na kadhalika. Kwa hiyo, hii miradi haikuokotwa, iko kwenye kitabu chetu cha mpango.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kitabu hiki kinabainisha kwamba, moja ya miradi tutakayofanya ni ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge. Kwa hiyo, huu ndiyo mwongozo wetu unaotuelekeza kuandaa Bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja pia kwamba Maafisa wetu wa Mamlaka ya Mapato wanafanya tathmini kwa wafanyabiashara, lakini wanapofanya hivyo wanaweka viwango vya juu kuliko uwezo au faida za biashara husika na kusababisha biashara kufungwa au wafanyabiashara kukwepa kodi. TRA inakokotoa kodi kwa wafanyabiashara kwa kuzingatia taratibu na kanuni ambazo zimebainishwa katika sheria mbalimbali. Kuna Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, Sura ya 332 na Sheria ya Usimamizi na Utawala wa Kodi ya mwaka 2015, Sura ya 438.

Mheshimiwa Spika, pia sheria hizi zimeweka utaratibu wa uwasilishaji wa pingamizi za kodi, kwa wafanyabiashara ambao wanakuwa hawakuridhika na makadirio ya kodi ambayo wanapewa, kwa mujibu wa sheria hizo, pingamizi zinawasilishwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa kwa makadirio ya kodi inayohusika. Sasa utaratibu huu unatoa nafasi kwa Mamlaka ya Mapato kutoa makadirio sahihi kulingana na mapingizi na hoja ambazo zimewasilishwa. Napenda Bunge lako lifahamu kwamba pingamizi za kodi zinashughulikiwa na watumishi wengine tofauti na wale waliohusika na makadirio hayo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo, Serikali inatambua uwepo wa watumishi wake wachache ndani ya Mamlaka ya Mapato ambao wamekuwa wakitoa makadirio ya kodi kinyume cha taratibu zilizowekwa, hawa tumeendelea kuwachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu na za kiutawala. Pia tumeendelea kutoa elimu kwa watumishi wetu kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, maadili na sheria, kanuni na taratibu.

Mheshimiwa Spika, tunayo pia tax payer service charter; hii nayo inatakiwa iwaongoze watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato kuzingatia weledi na kanuni zilizowekwa katika ukadiriaji wa kodi. Ni marufuku kwa watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato kukiuka maelekezo hayo, kama kazi ikikushinda huwezi kufuata taratibu haya tupishe wako Watanzania wengi ambao wanaweza kufanya hizi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mamlaka ya Mapato inawaelimisha wafanyabiashara juu ya mfumo wa kodi, tunawaelewesha pia juu ya taratibu ambazo zinatumika katika ukokotoaji wa kodi na namna ya kuwasilisha haya mapingamizi. Hatua zote hizi tunalenga kuwahakikishia wafanyabiashara kwamba kwa kweli wanastahili wafanye kazi kwa amani, wanafanya kazi nzuri, wanalipia kodi stahiki kwa mujibu wa sheria na siyo vinginevyo, kodi hizo zinatakiwa zichangie mapato ya Serikali kulingana na ukubwa biashara zao.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusu miradi ya PPP kwamba utekelezaji wake unasuasua. Hili kwa kiasi kikubwa bado ni geni sana katika Taifa letu. Tuna shida kubwa ya utaalamu katika eneo hili na hususan katika nyanja za sheria pia katika nyanja za fedha. Kwanza katika kuandaa credible PPPs, kuzi-package na namna ya kuzi-negotiate. Kwa sababu hiyo Serikali inapokea ushauri na tutaendelea kulifanyia kazi eneo hili sababu ni njia bora mbadala badala ya kutegemea mapato madogo ya Serikali peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda niseme kwamba mpaka sasa hivi hatuna Mshauri Elekezi ambaye aliingia mkataba na Serikali kuandaa upembuzi yakinifu kwa utaratibu wa PPP ambaye amesheleweshewa malipo. Kwa hiyo, tutaendelea kuihimiza Serikali nzima na taasisi zake kwamba kabla ya kutangaza zabuni, basi wapatikane wataalam elekezi wa kuandaa miradi ya PPP na kuhakikisha kwamba bajeti inatengwa ya kuweza kugharamia malipo ya wataalam elekezi wa kuandaa maandiko ya miradi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili pia kulikuwa na hoja kwamba kuna mradi wa Mchuchuma na Liganga, reli ya Mtwara, Tanga, Moshi, Arusha ambapo Shirika la Reli yetu liliingia mikataba na wakandarasi kwa ajili ya kuandaa upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa miradi hii, kwa utaratibu wa PPP. Napenda nieleze kwamba miradi hii utaratibu uliofuatwa ni ununuzi wa kawaida (traditional procurement) na siyo utaratibu wa PPP, kazi hii ilikamilika mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina. Ni kweli kabisa ofisi hii ina jukumu kubwa la kusimamia Mashirika ya Umma na hoja kubwa ilikuwa kwamba imepokea asilimia ndogo sana ya bajeti kati ya fedha ambazo ziliidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mwaka huu wa fedha ilitengewa shilingi bilioni 102.23 kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 95 kilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia madai mbalimbali ya Mashirika ya Umma na shilingi bilioni 7.23 kwa ajili ya gharama za uendeshaji wa ofisi.

Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia Aprili, fedha zilizotolewa kwa ajili ya OC ni shilingi bilioni 18.62, ambapo shilingi bilioni 5.35 kilikuwa ni kwa ajili ya madai ya Mashirika mbalimbali na shilingi bilioni 13 kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi ikiwa ni pamoja na kulipa madai ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.

Mheshimiwa Spika, ninachojaribu kusema hapa ni kwamba ni kweli fedha zilizotolewa kwa ofisi ya Msajili wa Hazina zinaonekana ni kidogo, lakini ni vizuri Waheshimiwa Wabunge, wakazingatia pia kuwa ulipaji wa madai ya Mashirika ya Umma yanategemea kukamilika kwa uhakiki au mashauriano ya kimahakama. Kwa hiyo, hatuwezi tu kutoa fedha mpaka haya mawili yawe yamekamilika.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusu Deni la Taifa kuongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 1,054.6 na kuongezeka kutoka dola za Kimarekani 1,957 na hivyo kupelekea Serikali kulipa riba kubwa. Hoja hapa ilikuwa kwamba Serikali ina mikakati gani ambayo imepanga kwa ajili ya kupunguza Deni la Taifa.

Mheshimiwa Spika, nisisitize kuwa kwamba ni kweli deni limekuwa linaongezeka mwaka hadi mwaka, nirudie tena kusema deni letu jamani ni himilivu kwa vigezo vyote, tutaendeleaje bila kukopa? Lazima tukope hadi Machi, 2018 deni la Serikali lilifikia bilioni 48,889 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 16.3. Kati ya kiasi hicho deni la ndani lilikuwa bilioni 14,158.6 na deni la nje bilioni 35,729.9. Ongezeko hili lilitokana na mikopo mipya yenye masharti nafuu na ile yenye masharti ya kibiashara. Lakini kikubwa tulitumia fedha hizi kugharamia fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu, mikakati yetu kwanza tunahakikisha kwamba mikopo ambayo inapewa kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu. Mikopo ya kibiashara tunaikopa kwa uangalifu sana, ikiwemo kuhakikisha kwamba hii mikopo ni ile ambayo inakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa letu, ndiyo maana tunapeleka mikopo hii kwa ajili ya kujenga mradi wa umeme unakuwaje na uchumi wa viwanda bila umeme?

Mheshimiwa Spika, tunahitaji kujenga standard gauge railway ili tuweze kunufaika na biashara kwenda nchi jirani, ndiyo umeme utakavyokuwa, mkakati mwingine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ikienda sambamba na kupunguza matumizi yanayoweza kuepukika. Kwa hiyo, niendelee tu kusisitiza kwamba tunao mkakati madhubuti na kila mara tunafanya mapitio ya uhimilivu wa deni kwa kila miezi mitatu na kila mwisho wa mwaka ndiyo tunafanya uchambuzi ambao unahusu eneo lote kwa upana wake, tunafanya pamoja na wenzetu hatufanyi peke yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Nsanzugwanko, kuhusu kujenga ofisi ya Mamlaka ya Mapato Buhigwe, Kasulu na Kakonko, nilitaka nimwambie tu kwamba Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, nia yetu kama Serikali ni kuwapa wananchi wetu huduma kwa urahisi na TRA itajenga ofisi hizo kwa awamu kadri tunavyoendelea kupata mapato na tutatoa kipaumbele kwa maeneo ambayo tayari viwanja vilishapatikana kama ilivyokuwa kwa Kasulu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nimesikia kengele, kama nilivyokwisha kutoa maelezo ni kwamba tutajibu hoja zote hizi kwa maandishi, naomba nisemee moja tu kwamba kwa nini tunaenda kwenye commercial loans badala ya kwenda kwenye concessional loans ambayo itakuwa ni mzigo kwa wananchi. Napenda tu nisisitize kwamba Serikali ilianza kwenda kukopa kwenye masharti ya kibiashara essentially kutokana na kupungua kwa mikopo yenye masharti nafuu na misaada pamoja na nia ya Serikali ya kuongeza ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Spika, hii ni muhimu sana ndugu zangu tuangalie mwenendo wa ulimwengu unavyokwenda, enzi zile ambapo Serikali huko Ulaya zilikuwa zinapenda sana general budget support hakuna tena, tutakaa na reli hii ya kizamani mpaka lini? Tutakaa na umeme wa kubangaiza
mpaka lini ambao una capacity charges za ajabu? Kwa hiyo ni mahitaji yetu haya ya kujenga miundombinu ya msingi kwa ukuaji wa uchumi wetu, ndiyo unaotusukuma tutafute vyanzo mbadala vya mapato.

Mheshimiwa Spika, bado tumeendelea kupata mikopo yenye masharti nafuu kama ile ya Benki ya Dunia, African Development Bank na yote kama nilivyoeleza tunaielekeza kwenye miradi ya maendeleo hatukopi kwa ajili ya kula.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusisitiza tu kwamba ni vizuri Watanzania tukaamka. Maendeleo yana gharama, hakuna maendeleo ya lelemama ya kupata bure. Baadhi ya miradi hii Waheshimiwa Wabunge tunakopa kwa ajili ya vizazi vijavyo, tutatumia reli hii kwa zaidi ya miaka 200 ijayo, lazima tuweze kutoa hiyo sacrifice. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naomba kutoa hoja.