Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kabla sijaanza kuchangia hoja iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kuunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kufika siku hii muhimu sana kwa Taifa letu kwa Wizara yetu ya Fedha na Mipango. Pia nawashukuru sana viongozi wetu wakuu, Mheshimiwa Rais wetu kwa miongozo yake kwetu ambayo amekuwa akituongoza ili tuweze kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa ni Taifa la kipato cha uchumi wa kati hata kabla ya mwaka 2025. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais katika jambo hili, amesimama imara na tunaliona Taifa letu kweli linasogea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa miongozo yake kwetu, kwa ushauri wake kwetu na kututakia mema katika utekelezaji wa majukumu yetu. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kiongozi wetu wa shughuli za Serikali ndani ya Bunge letu tukufu, naye kwa miongozo yake, yote haya tunayatenda kwa pamoja, namshukuru sana. Kwa pamoja, niwatakie afya njema viongozi wetu wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango kwa kuendelea kufanya kazi hii kwa moyo wake wote kwa kujitolea usiku na mchana. Hakika nasema na Mheshimiwa Waziri naomba nikwambie kwamba najivunia kufanya kazi nawe kama msaidizi wako. Usichoke kunipa miongozo yako, niko tayari kwa muda wowote kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa mijadala ambayo ni yenye afya kabisa ndani ya Bunge lako tukufu. Hii yote haiwezekani, bali ni uongozi wako makini, uongozi wako hodari kabisa ndiyo unasababisha Bunge letu liendelee kuwa na afya. Nakupongeze sana kaka yangu kwa uongozi huu. Endelea kusimama imara na kwa pamoja tutalifikisha Taifa letu kule ambako dira yetu ya maendeleo inatuelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezisema ndani ya Wizara yetu ya Fedha. Nianze na hoja ambayo ilikuwa ni kuhusu malipo ya madeni mbalimbali ambayo Serikali yetu inadaiwa na watoa huduma, watumishi wetu na wazabuni wetu.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge katika hoja hii, wameisema vizuri sana. Nawashukuru kwa kipekee wale waliotuunga mkono kwenye zoezi zima la uhakiki kuhakikisha kwamba kile kinachoenda kulipwa kinalipwa kile ambacho Watanzania walipokea huduma. Nawapongeze sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba, Serikali yetu iko committed kabisa kuhakikisha kwamba madai yote ambayo Serikali inadaiwa na Watanzania na wasiokuwa Watanzania yanalipwa. Nasema hivi kwa sababu, mwaka huu 2017/2018, bajeti kwa ajili ya kulipa madeni haya ilikuwa ni shilingi trilioni moja kamili ndani ya bajeti ambayo Bunge lako tukufu iliipitisha.

Mheshimiwa Spika, ninapoongea leo, tayari tumeshalipa zaidi ya bajeti iliyopitishwa na Bunge lako tukufu. Tulipitisha shilingi trilioni moja na leo tayari tumeshalipa shilingi 1,167,753,620,321. Hii ni dhamira njema ya Serikali yetu kuhakikisha kila kinachohakikiwa katika madeni tunayodaiwa kinalipwa kwa Watanzania na wasiokuwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, hii shilingi trilioni 1.167 ambayo tumeshalipa tayari imelipwa kwa akina nani? Maana imesemwa kwamba Serikali inadharau, walimu hawalipwi, hapana. Tumelipa madeni haya kwa watu wote. Kama tutakumbuka Waheshimiwa Wabunge, mwezi wa pili Serikali yetu ililipa madeni ambayo yameshahakikiwa kwa watumishi peke yao zaidi ya shilingi bilioni 43. Katika hizi shilingi bilioni 43 zililipwa kwa ajili ya watumishi 27,389. Kati ya watumishi 27,389 walimu walikuwa ni 15,919. Hii ni commitment ya hali ya juu sana kwamba yote tuliyoyahakiki, tuna uhakika nayo, yanalipwa kabisa kama inavyotakiwa. Walimu wetu tunawakumbuka, tunatambua mchango wao kwamba bila wao sisi sote tusingekuwa hapa tulipo.

Mheshimiwa Spika, madeni haya ambayo tunayalipa, tunalipa, kama nilivyoanza kusema, baada ya uhakiki kukamilika. Naomba hili liweze kueleweka. Katika hizi trilioni moja ambazo tumeshalipa tayari, ni madeni yaliyohakikiwa hadi Juni, 2016. Tulihakiki, kwa nini tunahakiki?

Mheshimiwa Spika, sisi sote ni Watanzania, tunafahamu tulikotoka, tumepigwa vya kutosha. Haikuwa ajabu kusikia mwalimu anaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 500. Unaweza ukajiuliza, haya ni madai ya nini kwa mtumishi mmoja wa umma kuidai Serikali? Anakwambia ni madai kwa ajili ya likizo yake. Ni likizo gani hiyo mtumishi wa umma ataidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 500? Kwa hiyo, hili liweze kukaa sawa sawa na haya yote tunafanya kwa dhamira njema kama nilivyosema.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 10 cha Sheria ya Bajeti, namba 11 ya mwaka 2015 na kifungu cha 5 cha Sheria ya Fedha za Umma namba 6 ya mwaka 2001, pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2004 vinampa mamlaka Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kusimamia matumizi ya fedha za Umma, ndicho kinachofanyika.

Mheshimiwa Spika, pia vifungu vya 12 na Kifungu cha 68 vya Sheria yetu ya Bajeti, namba 11 ya mwaka 2015 vinampa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kwa taasisi za umma, lakini pia kufanya marejeo ya mapato na matumizi ya taasisi za umma. Kwa hiyo, hiki tunachokifanya kinafanywa kwa msingi imara kabisa wa sheria, hakuna sheria yoyote inayovunjwa katika hili.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, ni commitment ya hali ya juu ya Serikali yetu kuhakikisha kwamba madeni haya yote yanalipwa lakini baada ya uhakiki.

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu pia, Bunge lako tukufu kwamba yapo madeni ambayo ni Juni, 2017. Madeni haya tunaendelea kuyahakiki. Tunataraji uhakiki wa madeni ya mpaka Juni, 2017 yafike mwisho wake, mwisho wa mwezi huu wa sita. Tutakapokuwa tumejiridhisha tayari sasa tutaanza kuyalipa. Kwa hiyo, hii ni sahihi na niwaombe sana watumishi wetu, Maafisa Masuhuli na watu wote walioihudumia Serikali yetu watusaidie sana kwenye zoezi hili.

Mheshimiwa Spika, tunapambana na changamoto kubwa, unakwenda sehemu unakuta hupati zile nyaraka halisi na Maafisa Masuhuli hawataki kushiriki. Watoa huduma ukiwaambia tunaomba nyaraka zako zile original ambazo unasema unaidai Serikali, hawataki kutupatia. Sasa tukibaki tu tunalalamika wakati tunatenda jambo hili kwa ajili ya dhamira njema hatutafika na tutaendelea kulalamika. Nawaomba sana watu wote wanaoidai Serikali yetu waweze kutoa nyaraka hizi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa pia na malalamiko mengine kwenye jambo hili kwamba madeni yaliyolipwa ya watumishi mwezi wa pili, kama nilivyosema yalilipwa kwa kiwango kidogo.

Mheshimiwa Spika, madeni haya yaliyolipwa ndiyo yaliyogundulika ni halali kulingana na nyaraka zote zilizohitajika. Hatukatai yalikuwa submitted madeni ya shilingi bilioni 66.92, yaliyokuwa halali ni shilingi bilioni 43.39 na Serikali ikasema kwa yule ambaye anaona hajalipwa na ana nyaraka halali, azilete sisi tutazipokea, tuhakiki, tukijiridhisha na madeni yote haya ya shilingi bilioni 66 kama yatagundulika ni halali, basi Serikali yetu itaweza kuyalipa.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niseme jambo ambalo limesemwa kwa kiwango kikubwa linalohusiana na malipo haya, kwamba, katika Wizara ambazo zinavunja sheria za nchi yetu ni Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa tumelisikiliza, lakini tunapenda kuwaambia kwa ujasiri wa hali ya juu, katika Wizara tunazofuata sheria ni Wizara ya Fedha na Mipango. Hatuko tayari kuona tunavunja aidha, Katiba yetu wala sheria zetu ambazo Bunge lako tukufu limetunga. Nasema haya kwa sababu yalisemwa pia kwamba pesa za Mifuko Maalum zinakusanywa na zinawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kazi hazifanyiki.

Mheshimiwa Spika, tunasema kwa ujasiri mkubwa Wizara ya Fedha kwamba jambo hili halipo. Kwa sababu katika mtiririko wa makusanyo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania zipo aina mbili za makusanyo. Makusanyo ambayo siyo ya mifuko maalum na makusanyo ya mifuko maalum. Makusanyo ambayo siyo ya mifuko maalum yanaingia katika Revenue Collection Deposit Account ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Pesa hizi zikishaingia hapa, ndiyo zinakwenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini vyanzo vyenye mapato maalum vinaingia katika mfuko maalum ambao huu unakusanya pesa zote hizi zenye vyanzo maalum inaitwa ni Fuel Levy Collection Deposit Account na jina lake linajieleza.

Mheshimiwa Spika, katika hizo, ziko fedha za Mfuko wa Reli, zina akaunti yake. Zikishaingia katika Deposit Account zinakwenda kwenye mfuko specific. Fedha za Mfuko wa Barabara zikishaingia kwenye Deposit Account hiyo zinakwenda kwenye Account ya Mfuko wa Barabara na fedha za Mfuko wa Umeme Vijijini zikishaingia katika Deposit Account hiyo zinakwenda kwenye Account ya REA.

Mheshimiwa Spika, nini kinafanyika na inaonekana kwamba, tunazuia fedha hizi kama Wizara ya Fedha? Wakati tunajadili bajeti za Wizara mbalimbali, tulisikia Waheshimiwa Wabunge wakilalamika ndani ya Bunge lako tukufu kwamba fedha nyingi za maji zimepelekwa, lakini ukifuatilia miradi ya maji, hakuna miradi inayofanya kazi. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Jemedari wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, tumesema hili hatutaki litokee. Hatutaki liweze kutokea. Tutafuatilia kuanzia mwanzo wa miradi hiyo, tutajiridhisha na mchakato mzima mpaka tutakapopeleka pesa. Watakapoanza kutekeleza miradi hiyo, kama Wizara tuliopewa mamlaka ya kufuatilia makusanyo na matumizi ya fedha za Serikali, tutakwenda kwenye miradi kukagua na kujiridhisha kama kweli pesa hiyo inafanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndipo tulipo na siku zote Waheshimiwa Wabunge niwaambie, kwenye transformation yako machungu ndani yake, lakini machungu yenye dhamira ya dhati ya kwamba tukimaliza hapa, tutakwenda kwa mfumo sahihi wa kuhakikisha kwamba sasa Taifa linakimbia na pesa za Watanzania masikini zinatumika kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki tukifanyacho ni jambo ambalo limesemwa hata kwenye vitabu vitukufu vya dini zetu. Kwa wale Waislamu naomba mwende kwenye Surat Israa, naomba msome. Mheshimiwa Khatib kwa hili naomba nisikilize, katika Surat Israa nenda aya ya 27, aya ya 28, aya ya 30 inasema nini katika mapato na matumizi ya pesa za mtu yeyote na za Serikali yetu. Ndicho tunachokifanya.

Mheshimiwa Spika, mwisho wa aya hii ya 30 ya Surat Israa, ndugu zangu, Mwenyezi Mungu anatuambia kwamba hicho mnachokifanya muwe na hofu kwa Mungu kwa sababu wanaofanya ubadhirifu hao ni marafiki wa shetani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kuwa marafiki wa shetani. Serikali ya Awamu ya Tano inataka kutenda kwa ajili ya Mungu. Tutafanya kazi hiyo, niwaombe sana tushirikiane kuhakikisha hili linafanya kazi na Taifa letu linapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naona na Mheshimiwa Khatib kapiga makofi, naamini hiyo, imeingia vizuri. Anasema imekuja vizuri kwa hiyo, ndiyo maana kapiga makofi. Tunafanya hayo kwa utukufu wa Mungu aliyetuamini na kutuweka kwenye mjengo huu, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kulisemea, nalo ni kuhusu Serikali yetu kuchukua vyanzo vya mapato vya Halmashauri zetu. Naomba nitumie neno alilolitumia mtani wangu Mheshimiwa Msigwa kwamba tumezi-ground Halmashauri, hapana, siyo sahihi hata kidogo. Nasema hili kwa sababu moja kubwa, nimesema dhamira ya Serikali kwenye kusimamia mapato na matumizi ya Serikali yetu, jambo tunalolifanya kwenye property tax nilieleza Bunge lililopita nikasema, tulileta mabadiliko ya sheria tukabalidisha wote kwa pamoja hapa ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, tulichokibadilisha, tukasema, pesa hizi zitakusanywa halafu zitarejeshwa kwenye Halmashauri zetu kulingana na bajeti za Halmashauri husika. Hicho kipengele cha mwishio naona kinasumbua sana; “kulingana na bajeti za Halmashauri husika,” ndicho tunachokifanya Serikali ya Awamu ya Tano. Tunakusanya na tunapeleka katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliambie Bunge lako tukufu, tumepitisha bajeti hapa ya Wizara ya Afya, kila Mbunge alisimama ana zaidi ya vituo viwili au vitatu kwenye Jimbo lake. Hizo ndiyo pesa zinazokusanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi sote ni mashahidi, mvua imenyesha ya kutosha, ikaharibu miundombinu, sasa hivi kila Mheshimiwa Mbunge jimboni kwake wakandarasi wameshafika wanarekebisha miundombinu iliyoharibika. Ndiyo bajeti tunayoirejesha Halmashauri hii, haiwezi kusema kwamba zinaweza kutoka sehemu nyingine, hapana.

Mheshimiwa Spika, wapo wanaobeza elimu bure, hapana. Ndiyo bajeti tunayoikusanya, tunarejesha na inamfikia kila mtoto wa maskini wa Taifa hili. Hilo ndilo jambo la msingi na hii ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano. Tunatenda kwa vitendo na wananchi wanaona haya tunayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo ndilo jambo la msingi, hii ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano tunatenda kwa vitendo na wananchi wanayaona haya tunayoyafanya.

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe jambo moja, Mamlaka ya Mapato Tanzania ndiyo mamlaka pekee kisheria ambayo imepewa jukumu la kusimamia sheria zote za kodi zilizoainishwa katika jedwali la kwanza la Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili sheria hii inabainisha katika Ibara ya 5(1)(a) kuwa TRA itakadiria, itakusanya na kuhasibu mapato husika, ndicho ambacho Serikali yetu ya Awamu ya Tano inafanya. Kwa mujibu wa Ibara ya 5(1)(c) cha Sheria Mamlaka ya Mapato kinatuambia Mamlaka ya Mapato inawajibika kusimamia makusanyo ya tozo na maduhuli yote ya Serikali yanayokusanywa na Wizara pamoja na Idara mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba turejee historia ya Chenge One na mapendekezo yake. Nini Chenge One ilisema? Tunachofanya kama Serikali tunatekeleza haya yote ambayo Bunge lako liliagiza Serikali yetu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu sana. Kwa hiyo tumeanza kutekeleza hatua kwa hatua kuhakikisha hili linafanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba Bunge lako Tukufu liliridhia marekebisho madogo ya sheria ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Chenge One, hivyo hatupaswi Waheshimiwa Wabunge kujitoa katika suala hili kwa kuwa mapendekezo ya awali ni ya Bunge tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunachokifanya ni kutekeleza tu yale ambayo Bunge hili lilipitisha.

Mheshimiwa Spika, naomba kusema pia kidogo katika dhamira ile ya kuhakikisha tunawafikia Watanzania kule walipo baada ya kukusanya mwezi wa Aprili, 2018 na Waheshimiwa Wabunge walikuwepo wakati tunazindua mkakati kwa ajili kuongeza mapato katika Halmashauri zetu. Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwepo, Halmashauri nyingi za Mkoa wa Dar es Salaam zilipata pesa za kutosha siku ile wakati tunazidua mkakati huu, dhamira ni nini? Ni kuhakikisha kila taasisi ndani ya Serikali yetu wanakuwa ni wabunifu kuhakikisha tunatafuta vyanzo vya mapato. Kwa hiyo, tutengeneze tuongee na Wakurugenzi wetu kwenye Halmashauri zetu. Tuweze kuandika miradi bunifu kwa ajili ya kuongeza mapato ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ina pesa, tatizo siyo pesa tatizo tunakwenda kuzitumiaje, hilo ndilo jambo la msingi sana. Halmashauri nyingi zimepata fedha hizi kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi itakayoongeza mapato kwenye Halmashauri husika. Niwaombe sana kwa pamoja tushirikiane katika jambo hili ili tuweze kufikisha huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne ambalo ningependa kulitolea ufafanuzi katika mchango wangu, ni hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Kombo aliyohoji pamoja na Wabunge wengine waliohoji kuhusu majukumu ya Tume ya Pamoja na Fedha. Waliohoji kwa nini wanapewa bajeti?

Mheshimiwa Spika, napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba majukumu ya Tume hii ya Pamoja ya Fedha yapo kwa mujibu wa Katiba, ambayo nayo ni pamoja na kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na au yanayohusu utekelezaji wa mambo ya Muungano. Ndani ya wiki iliyopita nilijibu swali kuhusu Tume hii ya Pamoja ya Fedha, nikasema tayari nini Tume ya Pamoja na Fedha imefanya katika kipindi chake uhai wake. Imefanya mambo makubwa ifanya study za kutosha na sasa katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 Tume ya Pamoja ya Fedha pamoja na mambo mengine inakwenda kupanga na kufanya mapitio ya study ya usimamizi wa Deni la Taifa kwa ajili ya kuhuisha taarifa kufanya mapitio na takwimu zilizotumika katika study za awali iliyowasilishwa Serikalini.

Mheshimiwa Spika, Tume hii pia itaendelea kufanya uchambuzi wa mapato na matumizi na utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa lengo la kuwa na kanzidata ya taarifa sahihi za fedha zinazohusu mambo ya Muungano. Vilevile Tume imepanga kufanya kazi nyingine zikiwemo kutoa elimu kwa wadau wa Tume hii kuhusu uhusiano wa kifedha baina ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hili la kutoa elimu ni muhimu sana ili kwa pamoja tuweze kuelewa ni nini tunafanya hata ule mjadala niliyosema wiki iliyopita mbele ya Bunge lako tukufu naamini tukishapata elimu ya kutosha mjadala ule utafikia maafikiano mazuri na tutaenda kutekeleza majukumu haya Kikatiba kama yalivyopitishwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulisemea nalo ilikuwa hoja ya kwamba kwa nini bidhaa zinazoingia Tanzania Bara kutoka nje ya nchi kupitia Zanzibar zinatozwa kodi mara mbili. Napenda kuliambia Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna bidhaa inayotozwa kodi mara mbili. Bidhaa tunachokifanya ni kufanya assessment (uthamini) upya wa bidhaa iliyopitia Zanzibar kutoka nchi jirani na katika hili iliunganishwa kwamba bidhaa kutoka Zanzibar haziruhusiwi kuuzwa Tanzania Bara, hakuna zuio hilo.

Mheshimiwa Spika, bidhaa zote zinazozalishwa Zanzibar zinaruhusiwa kuuzwa Tanzania Bara lakini zifuate mfumo wa kiforodha. Hilo ni jambo la muhimu sana lazima tuhakikishe nini kinaingia na kimetoka wapi. Katika moja kwa nini Serikali yetu inafanya hivyo, tunafanya haya kwa sababu jambo kubwa tuko kwenye soko huria na tunahitaji kuweka mazingira mazuri, mazingira sawa sawa, mazingira, sawia ya kufanya biashara kati ya Tanzania yetu yote. Tunahitaji fair and competitive environment kwa ajili ya ufanyaji wa biashara. Tunataka haya siyo kwamba tunahitaji maana yake ilisemwa kwamba mfumo huu umeletwa ili kuiua bandari ya Zanzibar hapana! Tunachokihitaji ni hii fare and competitive environment ya kufanya biashara. Mtu awe na choice yeye mwenyewe, kwa nini apitie bandari ya Zanzibar na asipitie Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, hilo ni jambo la msingi lakini tukifanya upande mmoja kodi inayotozwa kwamba ni ndogo kulinganisha na upande wa pili halafu bidhaa zinazopita kodi ndogo ziingie upande wa pili. Hapa hakuna fare and competitive environment kwenye jambo hilo, kwa hiyo, hapo tutakuwa tume-declare moja kwa moja kwamba tulichokifanya ni kuilinda bandari ya Zanzibar na kuja kuiua bandari ya Dar es Salaam si sahihi hata kidogo. Yeyote atakayekwenda tufanye tu assessment ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, katika hili naomba niseme jambo moja, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa sasa inatumia mfumo wa TANCIS. Ndugu zetu wa ZRB wanatumia mfumo wa ASYCUDA na Serikali zetu mbili kwa sababu lengo letu ni kulinda muungano wetu kuhakikisha muungano huu unakwenda sawia tuko kwenye majadiliano na majadiliano haya muda mfupi tutafika conclusion kuhakikisha Watanzania wote wanafaidika na Utanzania wao katika jambo hili. Niombe sana liweze kueleweka hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jambo lililohusiana na jambo hili pia ilikuwa ni magari yanayotoka Zanzibar kuja huku Tanzania Bara. Tukichukulia nilikoanzia mifumo yetu ya kodi haiko sawia kinachotendeka sasa maana yake tuliambiwa hapa na niombe Waheshimiwa Wabunge tuwe tunasema ukweli ili tuweze kuwaongoza wananchi waliotuamini katika njia sahihi. Nalisema hili kwa sababu magari yote yanayotoka katika nchi za SADC, magari yote yanayotoka katika nchi za East Africa na magari yote Zanzibar ambayo ni Tanzania wote wanapewa muda wa miezi mitatu wanapoingia nchini. Tunafanya hayo ili kujiridhisha ili kujiridhisha gari hili kweli linaingia Tanzania Bara kwa ajili ya matumizi au kwa ajili ya biashara. Maana yake mtu anaweza akapitisha Zanzibar gari kwa sababu kodi yao iko chini kutokana na mfumo wao, ikija huku tutaua soko la huku hatutakuwa na fair competition kwenye soko letu.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge sote kwa pamoja tushirikiane dhamira ni njema, dhamira yetu ni moja kuwatumikia Watanzania maskini na hakuna maendeleo bila kodi lazima kodi zikusanywe na kwa hilo tutasimama imara kuzisimamia kuhakikisha kodi zote zinakusanywa kulingana na sheria zetu ambazo Serikali yetu imezipitisha.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo napenda kulisemea ni kuhusu TRA kuwa Mawakala wakukusanya nimeligusia. Naamini hii ni kengele ya pili naomba nirejee kusema nakushukuru sana kunipa nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu kidogo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili na Waheshimiwa Wabunge tushirikiane tushikamane tumpe moyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ili kazi yake iweze kuwa rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo napenda kurejea naunga mkono hoja hii, ahsante sana.