Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

 

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa tijihada kubwa inayofanyika katika kutatua changamoto za Watanzania katika sekta mbalimbali za huduma za jamii ambazo fedha zote zilizotolewa zinatoka katika Mfuko wa Hazina.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa ni kinara wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania kwa kuboresha huduma za kijamii kwa kuongeza mapato na udhibiti wake kwa kiwango cha kuridhisha. Mheshimiwa Rais amekuwa makini kwa kuteua wasaidizi wake makini kama Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu watatu, Kamishna Mkuu wa TRA na watendaji wote walioko chini ya Wizara hii ya Fedha kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kusimamia kikamilifu na juhudi kubwa katika kupanga na kutekeleza. Pamoja na pongezi, nina mambo machache kama changamoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja, ununuzi wa pamoja (bulk procurement), Serikali itafute uwezekano wa kuwa na matenki ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya usalama wa nchi (national reserve) kuliko kutegemea matenki ya makampuni binafsi. Mafuta hayo yanaweza kuhifadhiwa na taasisi ya Serikali kama GPSA.

Mheshimiwa Spika, pili, ni mafunzo kwa watendaji wa fani ya ununuzi na ugavi. Kuwe na bajeti ya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa Serikali na taasisi zake katika fani ya ununuzi na mikataba (procurement and contract management course) kwa kuzingatia kwamba asilimia 90 ya matumizi ya Serikali ni manunuzi ya umma. Hivyo basi, watendaji wa fani hii wawe na weledi na uadilifu wa kutosha kwa kuwapatia mafunzo ya ndani na nchi na nje kwa kushirikiana na PCCB katika kutoa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, tatu, ni kuhusu miradi kwa njia ya ubia (PPP). Kwa kuwa nchi yetu kwa sasa ina uhitaji mkubwa wa kufanya miradi mikubwa ya miundombinu ya aina mbalimbali kama barabara kubwa za kisasa, madaraja makubwa, vivuko, shopping malls, airport, hotel za kitalii, hospitali, viwanja vya michezo, viwanda, kilimo cha kisasa cha umwagiliaji na kdhalika, miundombinu hii inahitaji miradi ya ubia baina ya Serikali na makampuni binafsi ili kwa pamoja miradi hiyo iweze kuchochea uchumi wa nchi na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, bado kuna upungufu wa watalaam wa fani ya PPP na mikataba. Hivyo kuna uhitaji wa vijana wetu kwenda nje ya nchi kujifunza fani hiyo (PPP, Procurement and Contract Management) kwa kuzingatia nchi zilizobobea kwa miradi ya PPP kama China na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nne, Maofisa wa Kodi TRA wanaofanya tathmini kwa wajasiriamali au wafanyabiashara wa ngazi zote kwa kukadiria bidhaa/biashara kwa kiwango cha juu sana kuliko faida ya biashara husika, TRA iangalie uwezekano wa kufanya tathmini kwa kuzingatia uhalisia wa biashara husika.

Mheshimiwa Spika, tano, vyanzo vipya vya mapato; TRA kupitia Wizara hii iangalie vyanzo vipya vya mapato hata kwa kwenda kujifunza kwa wenzetu nje ya nchi ili kuongeza wigo zaidi wa kuongeza mapato ya nchi. Ukiangalia nchi yetu inapokea meli nyingi zinazoingia hapa nchini. Mfano, ndege, magari makubwa, viwanda na mitambo mikubwa ambayo hutoa hewa chafu (air pollution). Eneo hili linaweza kuwa chanzo cha mapato kipya kwa kutoza kodi (carbon tax) kwa kuzingatia nchi kadhaa duniani, kutumia utaratibu wa kutoza kodi eneo hili. Nchi kama India, South Africa na kadhalika hutumia aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, nashauri pia Serikali iwekeze kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji kwa mtazamo wa matokeo makubwa kwa muda mfupi, kwa kuzingatia mazao ya muda mfupi yenye kuleta tija. Kwa mfano, mazao ya mafuta ya alizeti, ufuta, pamba na mazao ya mahindi, ngano, maua, mchele na kadhalika. Maeneo kama haya yakifanyiwa uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi itaweza kuchochea uchumi wa watu binafsi na Serikali. Pia itasaidia kuongeza mapato kwa kuzingatia mahitaji ya mafuta ya kula duniani ni makubwa sana; hata mahitaji ya ngano, mahindi, mchele na kadhalika ni makubwa pia.

Mheshimiwa Spika, pongezi kubwa kwa Wizara na TRA. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.