Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uti wa mgongo, hii ina maana kuwa kilimo ni kila kitu na ni uhai wa Watanzania. Hivyo eneo hili linataka litiliwe maanani na kupewa kipaumbele kwani Watanzania walio wengi ni wakulima. Kwa kweli Watanzania wanahitaji yafuatayo katika kilimo ili kiwe kilimo bora na chenye tija:-
(i) Pembejeo na trekta ili wapate kilimo bora chenye tija;
(ii) Mbolea nzuri;
(iii) Wataalam au Mabwana Shamba ambao watawaelimisha kulima kilimo bora chenye kuleta tija;
(iv) Zana hizi zifike kwa wakati ili waendane na mipango ya kilimo;
(v) Pia wanahitaji miundombinu ya kuweza kulima kilimo cha umwagiliaji. Hili ni suala la kutilia maanani na kukipa kipaumbele kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima hivyo wanatarajia Wizara hii iwawezeshe ili wawe na kilimo endelevu chenye manufaa;
(vi) Madawa ya kuondolea maradhi mimea na mazao;
(vii) Kupata masoko ya uhakika nchini; na
(viii) Kutatua migogoro iliyopo baina ya wakulima na wafugaji kwa kuwapatia ardhi ya kutosha kila mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ufugaji, hii pia ni sekta muhimu sana na yenye kuleta tija. Hivyo wafugaji waelimishwe namna ya kushughulikia mifugo yao kuanzia kuwalisha, kuwatunza. Hivyo sekta hii inahitaji utaalam wa kuweza kushughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii inatupatia kitoweo cha nyama, hivyo mifugo hii inasaidia sana Watanzania. Naomba maeneo yafuatayo yaimarishwe:-
(i) Kupewa shamba la mifugo;
(ii) Madawa ya mifugo;
(iii) Viwanda vya kusindikia nyama na maziwa;
(iv) Kutengwa maeneo maalum ya malisho ya mifugo na kilimo;
(v) Kufanya utafiti wa kutosha ili tuwe na ufugaji wenye tija;
(vi) Vitendea kazi vya utafiti;
(vii) Serikali kuruhusu uzalishaji kwa Kiwanda cha Maziwa ambacho kitanunua maziwa kutoka kwa wafugaji;
(viii) Upanuzi wa mapori ya akiba; na
(ix) Kutoruhusu uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapoimarisha maeneo haya ya ufugaji na kilimo, nchi yetu itachukua hata nafasi ya pili au ya kwanza kwa kilimo bora na ufugaji wa kisasa na kuleta pato zuri la Taifa letu na hata migogoro itaondoka kati ya wakulima na wafugaji na tutakuwa na kilimo cha biashara chenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya uvuvi ni muhimu sana na ni sekta ambayo tukiendeleza italeta tija kwa Taifa na pato zuri sana, ila sekta hii inasumbuliwa na changamoto zifuatazo:-
(a) Uvuvi haramu wa mabomu na nyavu ndogondogo. Mabomu haya huharibu mazalia ya samaki (matumbawe);
(b) Wavuvi kutopata vyombo imara vya kuvulia (zana za kisasa za kuvulia);
(c) Viwanda vya kusindikia na kuhifadhi samaki;
(d) Boti bora za kuvulia;
(e) Kudhalilishwa kwa wavuvi wadogo kwa kuchomewa moto nyavu zao;
(f) Kukosekana kwa elimu ya uvuvi. Watu wengi wanavua kwa mazoea tu;
(g) Jambo lingine la muhimu ni kuanzisha bandari ya uvuvi kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi; na
(h) Kukosekana kwa soko ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tunaiomba Serikali itatue changamoto hizi katika sekta hii ili kukuza pato la Taifa. Tunamwomba Waziri achukue mawazo haya kwa ajili ya kuliokoa Taifa letu la Tanzania tuwe na kilimo, ufugaji na uvuvi bora wenye tija na Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia iangalie kwa jicho pevu sekta hii kwa kuilipia zile shilingi bilioni mbili kama Mahakama ilivyotoa amri kuhusu meli ya uvuvi maarufu kama “kesi ya samaki wa Magufuli” iliyokuwa ikiwakabili wavuvi raia wa China wamiliki wa meli ya uvuvi ya TAWARIQ.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila la kheri, Mungu ibariki Tanzania.