Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu, lakini pili niendelee kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na timu yake ndani ya Wizara na taasisi zao. Kipekee kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwamba wanafika sana kwenye Kamati yetu na kwa kweli kwa upande huo wanajitahidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako makosa ambayo sasa Wizara inataka kuanza kufanya. Kosa la kwanza ambalo Wizara inataka kufanya ni kuua Ofisi ya Mipango. Mheshimiwa Waziri wa Fedha kabla hajawa, alikuwa kwenye Tume ya Mipango, lakini sasa kwa kuwa ameingia yeye sasa, anatumia cheo hicho kuua Ofisi ya Mipango. Tungependa kuona kwamba Ofisi ya Mipango yenye Fungu Namba 66 inarejeshwa. Hatuwezi kukubali kuwa chini yako, chini ya Fungu Namba 50 kwa sababu mikakati mingi inakufa sasa. Kwa hiyo, hilo ni namba moja ambalo kwa kweli tungeomba lirejeshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili kwa uendelevu wa ukosefu wa mipango, hata mfano ukiangalia fedha tunazozipeleka kwenye Bodi ya Mikopo, ushauri wetu tungependa aidha, waanzishe mfuko wa elimu ya kusomesha vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwenye tangazo juzi kwamba vijana wetu wa diploma hawapati fedha za mikopo. Sasa haya ni mambo ambayo hayakubaliki, mtu anatangazaje na sisi tumeshajitoa kwenye fedha na vijana wanajua tayari watapata fedha? Sasa hii ni ukosefu wa planning unit ambapo kila mtu mwenye taasisi anaamua kusema mwenyewe. Kwa hiyo, tunaomba hilo nalo liweze kurudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Wizara ya Fedha kuna mahali wanaanza kukiuka kufuata sheria. Sheria tumezitunga wenyewe. Tuna sheria za mifuko ambapo mifuko mingine iko ring-fenced ambapo sasa mna- temper nazo zile fedha. Mfano iko Mifuko ya REA, Maji, TANROADS na Reli. Hiyo Mheshimiwa Waziri hamwendi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapenda kuona kwamba mnaenda vizuri zaidi, zile fedha ziheshimiwe, ziweze kwenda kama zilivyotarajiwa. Miradi mingi ambayo wakandarasi tumewa-commit mikataba, kazi hazianzi. Miezi tisa mtu ana mkataba lakini haanzi. Kwa hiyo, tunapenda hapo muweze ku-improve. Ipo mingine ambayo tumeiweka tu kimatamko; mfano, asilimia 15 ya refund za watu wa viwanda vya sukari mnashindwa kuwapa, wanadai mpaka shilingi bilioni 30 zinaenda mpaka shilingi bilioni 40. Sasa ni vizuri nazo muweze kuona.

Mheshimiwa Spika, tunazo fedha karibu shilingi bilion 600 kwenye kampuni za madini nazo hamjaweza kuwapa refund yao. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri aweze kujipanga namna ya kuwarudishia angalau kila mwezi.

Mheshimiwa Spika, tuna huu ugonjwa wa uhakiki. Naipongeza Wizara ya Fedha kuhakiki kulipa fedha ambazo zimetumia, lakini hebu wapeni uwezo hizi Wizara. Mlitoa mfano siku moja kwenye Kamati, tukasema Wizara ya Maji imeleta certificate za shilingi bilioni 109 lakini mmejiridhisha kwamba shilingi bilioni 17 tu ndizo zinatakiwa kulipwa.

Je, swali hapo kama Wizara ya Maji inaweza ikaleta vitu ambavyo karibu shilingi bilioni 92 ni fake; je, hiyo Wizara kwa nini hamjaivunja? Kwa hiyo, ni vizuri uhakiki uweze kuwa empowered kwenye Wizara zote ili hiki kipengele cha kujifichia cha uhakiki kiweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako madeni mengine ni halali. Yako madeni ya TANESCO na Maji, nayo mnahakiki. TANESCO wakileta bili ya umeme unahikiki nini? Je, zile Wizara nazo haziaminiki? Kwa hiyo, hapo napo muweze ku-improve vizuri ili muweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, fedha za kulipa wakandarasi, hili ni jambo lime-stuck uchumi. Wewe unataka makusanyo lakini ume-stuck uchumi. Wakandarasi hawapati hela, walio-supply hawapati hela, kila kitu kime-stuck. Sasa hayo mapato wewe unayapata wapi? Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli Wizara hii iweze ku-improve mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuimarisha Ofisi ya TR. Ofisi ya TR inasimamia karibu shilingi trilioni 47 ya investment. Investment kubwa iko pale, lakini hamuipi wataalam, hamuwapi empowerment, bajeti mnayowapa ni ndogo, sasa hata kutoa ripoti ya mwaka kwa Ofisi ya TR inakuwa ni shida. Wapeni fedha ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalo bomu lingine la mwisho. Hizi fedha za CDG mmesumbua Maafisa Mipango, Wabunge na Madiwani, fedha haziendi. Fedha za Maendeleo ya mwaka 2017/2018 hamjapeleka hata hela yoyote na huu ni mwezi wa sita unaisha. Kwa hiyo, ukisimama hapa utuambie, u-declare kwamba mwaka 2017/2018 kwenye Halmashauri zetu hakuna fedha ya maendeleo iliyoenda. Hili ni bomu kwetu sisi tuliochaguliwa. Tumeahidi tunaenda kuboresha zahanati hamna, shule, hamna; sasa tunaenda vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba hizo fedha hata kama zikitolewa, hata kama mkizitoa mwezi huu, basi tunaomba hizo fedha zitumike na mzidai zirudi baada ya mwaka. Mzipe grace period ya miezi sita ziendelee kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo ushauri wangu. Naunga mkono hoja.