Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Niseme kwamba ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo na wakati Kamati zinapangwa watu tuliopangwa Sheria Ndogo tulionekana kama vile watoto yatima kwa sababu inaonekana kama madaraja ya Kamati. Nimhakikishie Mheshimiwa Spika anayepanga Kamati kwamba nimepata nafasi ya kujifunza vitu vingi sana na ninamshukuru sana na kama Mungu atajalia niendelee kupangwa Kamati hii milele na milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili wamezungumza Wabunge hapa, la kwanza ambalo ni muhimu kwa Serikali, taasisi na vyombo mbalimbali kujua kwa mujibu wa Katiba na ninataka nirudie ili lieleweke. Bunge ndiyo lina jukumu la kutunga sheria kwa mujibu wa Ibara ya 64 ya Katiba. Kwa sababu Bunge tunakutana mara nne kwa mwaka na kwa sababu tuna majukumu mengine mengi zaidi ya kutunga sheria ndiyo maana Ibara ya 97(5) ya Katiba tumefanya delegation kwa mamlaka mbalimbali kutunga sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni muhimu Mawaziri, Halmashauri na Mahakama zetu kupitia Chief Justice zifahamu kwamba kazi hii tumeishusha. Vilevile kupitia Kamati hii ndogo baada ya hizo sheria ndogo kuwa gazetted tuna wajibu wa kuja kuziangalia kama zimeenda kinyume tuna wajibu na haki ya kuzirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana mkaelewa kwamba sheria hizi ndogo zinapuuzwa kwa sababu ya jina lake sheria ndogo. Sheria hizi ndogo ndiyo zinagusa maisha ya wananchi wetu mmoja mmoja kule chini kila siku. Kwa hiyo, kama kuna kanuni, by law, miongozo, kanuni za mahakama, amri, taarifa na tangazo maalum lolote lile linalohusu watanzania, wawekezaji na taasisi mbalimbali hizo zote ni sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana watu walikuwa wanasema ooh, mnaenda kutunga sheria za mbuzi na ng’ombe sijui, hapana. Ndiyo maana ningependa hicho kitu kinachoitwa semina hata Wabunge wapewe kwa sababu kazi tunayoifanya hapa tunafanya nusu, halafu ile nusu nyingine wanaenda kufanya watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza Mwenyekiti wetu wa kamati hapa kwamba kuna tatizo la Mawaziri wakipewa dhamana ya kwenda kutengeneza sheria ndogo wanatengeneza sheria ndogo ambazo zinakinzana na sheria mama. Juzi nimeshtuka sana wakati Kamati ya Katiba na Sheria ilipoleta suala la kuanzishwa mahakama (mobile courts) Waziri akalazimika kuliondoa kwa sababu Kamati ilikuwa haiungi mkono. Waziri anakuja anasema kwamba eti kifungu cha 4 cha JALA na kifungu cha 10 cha Magistrates’ Courts Act kinampa mamlaka Jaji Mkuu kuunda mahakama, jambo ambalo ni la uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 4 cha JALA kama ambavyo nimesema Jaji Mkuu ana uwezo wa kutengeneza rules za jinsi mahakama zinavyotakiwa ziendeshwe, lakini siyo kuunda chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Magistrates’ Court Act, JALA na Sheria ya Tafsiri inayotoa tafsiri ya Magistrate hakuna popote ambapo Jaji Mkuu amepewa ruhusa ya kuunda mahakama nyingine, lakini ana uwezo wa kusema hii Mahakama ya Wilaya ikajisogeze iende sehemu fulani ambayo haina Mahakama ya Wilaya ili wananchi wasogezewe huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira kama haya tukahoji hizi shilingi bilioni 48 mmezitumia mkanunua hayo mabasi kwa ajili ya mobile courts/special courts zinaenda kufanya nini? Tunajibiwa eti Jaji Mkuu anaweza kuunda mahakama mpya. Sasa vitu kama hivi vinatisha na vinaogopesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza Mheshimiwa Aida hapa, Sheria Ndogo za BASATA. Mwenyekiti wangu wa Kamati yaani ingekuwa ni amri yangu azimio hili la leo liseme kanuni hizi zisiende kutekelezwa mpaka Waziri alete marekebisho mengine. Kanuni hizi zinaua wasanii wetu, kanuni hizi hazijengi wasanii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, naomba nikisome kifungu cha 64 na Wabunge mnisikilize, kinasema; makosa na adhabu; haya makosa yote ninayosoma hapa ndiyo msanii anaweza akatozwa yote siyo moja moja.

Moja, Msajiliwa wa Baraza au mtu yeyote atakayebainika kuvunja au kukiuka masharti ya kifungu chochote cha kanuni hizi atakuwa anafanya kosa na atachukuliwa hatua zifuatazo;-

(i) Atatozwa faini ya papo kwa papo isiyopungua shilingi milioni moja;

(ii) Kufungiwa kazi husika na kutozwa faini ya papo kwa papo isiyopungua shilingi milioni tatu;

(iii) Kufutiwa usajili;

(iv) Kufungiwa kujishughulisha na kazi za sanaa kwa kipindi kisichopungua miezi sita;

(v) Kuzuiwa kujishughulisha na kazi za sanaa maisha kwa kubainika kulingana na ukubwa wa kosa;

(vi) Kutozwa faini na adhabu yoyote stahiki wakati wa utendaji wa kosa husika;

(vii) Kufungiwa kujishughulisha na kazi za sanaa kwa kipindi kisichopungua miezi sita; na

(viii) Kuzuiwa kujishughulisha na kazi za sanaa maisha kwa kubainika kulingana na ukubwa wa kosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sub-section 2 inasema adhabu zilizotajwa hapo juu katika kanuni ya 64(1) zinaweza kutolewa moja moja au kwa pamoja kulingana na uzito wa kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria zisipungua milioni moja, mbili na tatu. Ukiangalia sheria inayoanzisha BASATA hapa inawapa majukumu mengi ya kuweza kutafutia wasanii masoko, kuwajenga wasanii na kuwapa mafunzo, hawatekelezi kanuni hizi ila wameona wasanii wawili/watatu maskini wa Mungu wametoka, wanataka kuminya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisisitize Mwenyekiti wetu ukija ku-wind up, namshukuru Mheshimiwa Mwakyembe alikuja akawa na busara ya hali ya juu akasema kamati ninaomba hii kitu niondoke nayo nikairudie upya niiangalie, ni busara ya hali ya juu na kwa sababu ya busara hii azimio letu pamoja na mambo mengine lielekeze hizi kanuni batili zisitumike mpaka pale ambapo zitaletwa mpya na kamati ijiridhishe kwamba imeendana na hizi sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana.