Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uhai na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu na kuweza kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.

Pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika kwa kuanzisha Kamati hii, lakini pia utaratibu wa kuwasilisha taarifa hii mara mbili kwa mwaka, kwa sababu imekuwa na mchango mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu kwamba sheria ndizo ambazo Bunge tunashiriki kwa kiasi kikubwa katika kuzitunga, lakini kanuni zinatungwa na Mawaziri na zinaanza kutumika sisi tunakuja baadae kuziona. Kwa hiyo, ukiangalia kwa kiasi kikubwa sheria nyingi kwa kuwa, zinakuwa zimepitia kwa wadau wengi unaweza ukakuta hata kama kunakuwa na mapungufu yanakuwa ni machache sana. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuandaa kanuni si vibaya tukashirikisha wadau mbalimbali, ili na wenyewe wakatia mchango wao na wakaweza kutusaidia katika kuziboresha kanuni zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Sheria yetu ya Madini ambayo tuliipitisha mwaka jana na pia tukawa na kanuni zake; Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi. Sasa katika kanuni ukiangalia suala la local content na suala zima la indigineous bank na ndigineous company, ukiangalia pale unakuta kunakuwa na matatizo makubwa sana. Nia ya sheria ni nzuri, lakini inavyokuja kanuni unakuta sasa ile nia nzuri inapotea. Lengo la kuhakikisha kwamba, tunakuwa na local content siyo kwa vile ambavyo imetafsiriwa katika kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema kwamba, kampuni ya madini itawekeza akaunti zake katika indigenous bank na ukatoa tafsiri ya indigenous bank ambayo inaitoa CRDB, inaitoa NMB na naitoa NBC, benki zinazobaki kwa kweli, hazina uwezo hata hizo kampuni zikisema yanataka kukopa, lakini hata uwezo wake ule wa kuhimili kwa sababu baada ya hapo zitabaki labda Mwanga Community Bank, Mufindi Community Bank au labda Azania, ndizo ambazo utazikuta zinaendana na yale masharti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa kanuni ikitoka inachukua muda mrefu sana kuja kurekebisha, mimi nadhani ni vizuri sana Waheshimiwa Mawaziri wanapozitunga zile kanuni hata wakaishurikisha Kamati ya Sheria Ndogo wakazipitia kabla ya kuzitangaza katika Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kabisa kwamba zitakuwa ni kanuni nzuri sana kwa sababu hatutegemei kanuni izizidi sheria, lazima sheria iwe juu ya kanuni. Kwa hiyo, hilo lilikuwa ni pendekezo langu la kwanza, kwamba Waheshimiwa Mawaziri wanapotunga kanuni, wala sio vibaya waka-share na Kamati Ndogo, lakini pia wakawashirikisha wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachia suala la benki, mfano indigenous company, Shirika kama PUMA Serikali ina hisa 50%. Ndiyo kusema PUMA ikinufaika na Serikali imenufaika na wananchi wananufaika, kwa sababu Serikali inasimama kwa niaba ya Watanzania. Sasa kwa kanuni ile sasa inaitoa PUMA kufanya kazi na migodi ya dhahabu au na migodi mingine, kwa sababu PUMA sasa inakuwa sio indigenous company kwa sababu share za Serikali au share za Watanzania kupitia Serikali ni 50% tu. Kwa hiyo, niombe wakati tunavyotunga kanuni, nia ni nzuri, lakini tuwe tunaangalia hivi tunavyosema indigenous company au indigenous bank ni zipi tunazozikusudia na kama sisi tutanufaikaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kiasi kikubwa kampuni zetu, sekta binafsi katika nchi yetu ni change, kwa hiyo tunategemea pale ambapo Serikali ipo, imeingia ubia, ndio wananchi wapo, Serikali ikinufaika Wananchi tumenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo pia nilitaka nilichangie, tumesikia kwamba kumekuwa na matatizo ya uandishi katika baadhi ya kanuni na wakati mwingine hata sheria ndogo zinazotungwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hata hivyo wakati mwingine makosa yale yanajitokeza kutokana na uchache wa rasilimali watu katika ofisi zetu na wakati mwingine na wingi wa kazi uliopo. Mfano kama sasa hivi unakuta tuna Halmashauri 185, useme tu nusu yake wamepeleka Sheria zao Ndogo TAMISEMI na zinahitajika kwa haraka, umepeleka Sheria Ndogo 80 au 90, watumishi waliopo je, wanaendana na kazi iliyopo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nayo tuhakikishe kwamba, tunaijengea uwezo kwa maana ya kwamba, watumishi, rasilimali watu, lakini pia na kuziwezesha kwa sababu tunazo sekta zinazoibukia, masuala ya gesi na oil. Wengi wa wanasheria wetu wamesoma, lakini wanasoma mambo hayo hayakuwepo, lazima tuwajengee uwezo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.