Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Waziri, Naibu Waziri na Mkurugenzi wa TPDC kwa kukubali ushauri wangu wakati tunapitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kuna ushauri niliutoa nawashukuru mmetusaidia hususani kwa wananchi wangu pale Kilangala kuweza kunufaika na mkuza. Mheshimiwa Waziri nakuomba tu kwamba yale tuliyoyaanza na Mkurugenzi wa TPDC nafikiri ananisikia basi tuyamalizie ili kile tulichokubaliana wananchi sasa wakione ili wapate moyo ule ambao walikuwa nao siku ile tulipokuwa tunakubaliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja mbili ama tatu, kwanza nataka nihoji Wizara. Mwaka 2013, Rais wa Marekani Barack Obama alikuja Tanzania na kuzindua Initiative iliyoitwa Power Africa. Sababu iliyofanya aje kuzindua Power Africa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo wananchi wengi hawapati huduma za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambazo ziko Sub- Saharan Africa, asilimia 76 ya wananchi tunaoishi katika Jangwa la Sahara hatupati umeme na Power Africa ilikuja kuzinduliwa Tanzania, ilikuwa ni mpango wa miaka mitano chini ya ufadhili wa African Development Bank na partners wengine. Sasa miaka mitano imefika, tunaomba ndani ya Bunge iletwe tathmini ama Waziri wakati anajibu atuambie tathmini ya programu ya Power Africa imeishia wapi? Je, fedha ambazo zilikuwa zimeahidiwa zimepatikana ama hazijapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu taarifa tulizonazo Mheshimiwa Waziri Power Africa alipoondoka Rais Kikwete na Power Africa imeondoka Tanzania. Ndiyo taarifa tulizo nazo na imeondoka kwa sababu tumefeli kwenye Diplomasia ya Kiuchumi. Wafadhili waliokuwa wanafadhili miradi ile ya Power Africa wengi wao wame-withdraw fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hili siyo sahihi wakati Waziri anakuja kuhitimisha aje atueleze kwa sababu takwimu tunazo. Wamarekani ndiyo walikuwa wachangiaji pamoja na partners wao, wao sasa hivi hawatoi fedha na tunajua sababu kubwa na ugomvi mkubwa wa Marekani na Serikali iliyopo sasa madarakani ni hii Sheria ya Mtandao, sheria hizi ambazo zinakinzana kabisa na demokrasia ya wakati huu. Sasa fedha hizi kama kweli zilikuwa zinakwenda au zimetolewa basi tunahitaji tathmini ya Power Africa imeishia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie suala la gesi. Gesi imegundulika maeneo ya Kusini mwa Tanzania lakini kiwango ambacho kimepatikana ni kikubwa mno. Nashauri kama inawezekana hatuna hata sababu ya kwenda kwenye Stiegler’s Gorge, hatuna. Kwa kiwango cha gesi tulichonacho unaweza kupatikana umeme wa kutosha tukatumia kwenye viwanda na kwenye majumba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya Qatar inatumia gesi. Rasilimali kubwa iliyofanya Qatar leo wafike pale walipofikia ni gesi. Mheshimiwa Rais Kikwete wakati yuko Mtwara anatushawishi wananchi wa Kusini tukubali mradi wa bomba la gesi alisema Tanzania itabadilika itakuwa Qatar ya Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Kikwete alikuwa Rais aliyetokana na Chama cha Mapinduzi ambaye ndiye aliyetuahidi kwamba tutakuwa Qatar ya Afrika. Rais John Magufuli naye ni Rais anayetokana na Chama cha Mapinduzi amekuja anaachana na ule mradi wa bomba la gesi, anaachana na miradi yote ya gesi, je, mmeshatufikisha kwenye Qatar ya Afrika? Kama tumefika kwenye ile level ya kuitwa Qatar ya Afrika basi tuelezeni. Tunachokishuhudia ni umeme shida na kiwango cha upatikanaji wa umeme vijijini bado ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna biashara ya gesi ambayo nimemwona Waziri juzi anaizungumzia kwamba inataka kuanza Mtwara na Dar es Salaam, ni biashara nzuri sana. Mwaka jana hapa tulitenga fedha kwenye bajeti kwamba pamoja na maeneo mengine ambayo gesi itasambazwa majumbani ni Lindi. Nakumbuka ilitengwa shilingi bilioni moja kwenye bajeti iliyopita kwa ajili ya kutengeneza miundombinu Lindi. Leo Waziri anakwenda kuzindua anaanza kusema kwamba Dar es Salaam na Mtwara wataanza kutumia gesi majumbani mbona Lindi haipo? Lindi tuna gesi ya kutosha lakini sijaona imetajwa. Sasa Waziri hebu atueleze kwamba wametutoa au sisi tutakuwa watu wa kufuatia baadaye? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu suala la REA. Mheshimiwa Waziri wakandarasi wengi wa REA wanalalamika kwamba Waziri amekuwa kama anawafanyia harassment. Leo Waziri anasema mnakwenda kuzindua mradi, vifaa wanatakiwa waende wakavichukue TANESCO, wakaviazime, wakati mwingine kuna miradi mnaizindua haijakamili ili mradi tu ionekane kwamba REA inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna tatizo Wizara ya Fedha ambako Bunge zima tunajua kwamba mambo ya nchi hii hayaendi kwa sababu tatizo liko Hazina na Wizara ya Fedha. Hakuna Mbunge ambaye hajui, hakuna mwananchi ambaye hajui kwamba kama Waziri Mpango ndiyo Waziri wa Fedha na ataendelea kuwepo katika miaka mitano yote ya Rais Magufuli, nchi hii haitakwenda kwa sababu ameshindwa kumshauri Rais. Mimi leo ukiniambia nitaje Waziri aliyefeli zaidi nchi hii ni Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Philip Mpango, hili halifichiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara ya Kilimo wamelalamika fedha, kwenye Wizara ya Maji wamelalamika fedha, TAMISEMI wamelalamika fedha, kwenye umeme tunajua Waziri hasemi tu kwa sababu ya uwajibikaji wa pamoja lakini naye pia shida yake ni fedha. Ndiyo maana wakandarasi wamesaini mikataba zaidi ya miezi tisa mpaka sasa hamjawapa fedha.