Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi lakini kwanza niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jiji la Tanga ambao nitaanza kwanza kwa kuwazungumzia katika suala zima la bomba la mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hilo nisije nikasahau kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kuzungumza katika Bunge lako hili.

Mheshimwa Mwenyekiti, Tanga itakuwa ndiyo last destination ya bomba la mafuta na patakuwa na refinery nyingi ambapo itakuwa ndiyo mitambo ya kuingiza kwenye meli, mitambo ya kusafisha crude oil na mambo mengine. Kwa hiyo, kama walivyosema wasemaji wengine niishauri Serikali kwamba pale ambapo mradi utakuwa umepita kipaumbele cha kwanza katika ajira wapewe watu wa eneo hilo. Kwa hiyo, nawaombea watu wa Tanga wale ambao wana taaluma mbalimbali wapewe kipaumbele cha kwanza katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nizungumzie suala zima la umeme wa REA. Sisi ambao tuko kwenye Majiji umeme wa REA sasa umekuwa kama unatugeuka kwa sababu tuliambiwa kwanza hakutarukwa kijiji hata kimoja lakini pia shule zote za msingi na sekondari ambazo hazina umeme watawekewa umeme wa REA. Nitaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze mpaka sasa hivi ni shule ngapi za msingi zimewekewa umeme wa REA na shule ngapi za sekondari zimewekewa umeme wa REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, kwenye umeme wa REA, kuna baadhi ya vijiji waliomba umeme wa TANESCO baada ya kuja hii neema ya MCC ambayo ilileta REA I, II na III wakaomba sasa waingizwe katika mradi ule ambao utakapokuwa umefanya wiring unalipia Sh.27,000. Hata hivyo, TANESCO inawalazimisha walipe gharama ile ile ya TANESCO ya Sh.370,000. Mfano upo katika Jiji langu la Tanga kwenye Kata za Kiomoni kwa maeneo ya Pande Mavumbi, Pande Muheza, Pande Marembwe, vilevile katika Kata ya Pongwe maeneo ya Kinangwe na Kisimatui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, hata kwenye Kata ya Kirare kule kunakozalishwa sana muhogo, maeneo ya Mapojoni na maeneo ya Mtakuja, bado umeme wa REA huko haujafika lakini wananchi pia wamekuwa na huko wanakizungumkuti wakiuliza wanaambiwa kwa sababu mmekuwa Jiji ninyi hampaswi kupata umeme wa REA. Kuna kitu kipya sasa hivi pia nimeambiwa kinaitwa para urban, kwamba kuna kitengo kipya kinaanzishwa, huu itakuwa kama ni ujanja wa kuwakwepa wananchi. Kama tumeamua kuwasaidia wananchi tusianze kuleta visingizio vidogo vidogo tuwapelekeeni umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiambiana hapa kwamba asilimia 75 ya Watanzania wanaishi vijijini lakini tangu tupate Uhuru mpaka leo ni asilimia 10 tu ya Watanzania wanaofaidi umeme. Sasa kwa nini tunataka wazalishaji wawe wa vijijini lakini tukifika kwenye umeme tunaanza kupanga mipango tofauti. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuhakikishie ni kweli vijiji havitarukwa au lah! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya vijiji walipelekewa nguzo chache. Wanakijiji wako 1,000 wanaomba nguzo1,000 wanapelekewa nguzo 500 au nguzo 400, wengine wanakosa kupelekewa huduma ya umeme. Wako tayari kulipia kama vile ambavyo unalipa umeme
TANESCO lakini unasubiri miezi sita, hata kwenye REA watu wapo tayari kulipia lakini hawapatiwi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ichukue utaratibu wa kuandaa kampuni ya TANESCO iwe kama vile kampuni za simu, pawe na ushindani kwa sababu disadvantage of monopoly kwa TANESCO ndiyo inawafanya wajione kwamba wao wako zaidi. Tuanzishe kampuni za umeme kama kampuni za simu iwe mwananchi ana uhuru wa kuchagua kampuni anayotaka. Simu leo wanashindana kupunguza bei ya muda wa maongezi kusudi wapate wateja. Kama kungekuwa na shirika lingine la umeme Tanzania, Waziri nakuhakikishia TANESCO labda ingebaki na Taasisi za Serikali, kwa sababu kuna usumbufu, kuna urasimu, na rushwa imejaa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua, ufisadi wote unaopita Tanzania TANESCO hawatoki. Mheshimiwa Waziri tunaomba hili uliweke sawa. Kwenye umeme wa REA tunataka wananchi wetu wapate umeme wa vijijini na kama ni Sh.27,000 mtu akishafanya wiring iwe Sh.27,000 kweli, siyo Serikali inatangaza Sh.27,000 akifika TANESCO anaambiwa aaah, hizo ni kauli za wanasiasa tu, hili jambo linaichafua Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la bei ya umeme. Bei ya umeme ndiyo inayosababisha watu watumie mkaa kwa wingi, ndiyo inayosababisha watu watafute vishoka kwa ajili ya kuwaunganishia umeme. Sasa tushushe bei ya umeme ili wananchi wetu wafaidi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Afrika Mashariki na Kati …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)