Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru lakini nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha tunaendelea na mjadala wa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapa pole ndugu zangu wa Ikungi kwa kufiwa na Katibu wao wa Wilaya wa Chama cha Mapinduzi. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuipongeza Wizara ya Nishati, ama hakika ndugu zetu hawa wa Wizara ya Nishati wanaonesha vision na mission ya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, kwa kweli niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kabisa na kwa mara ya kwanza naona wameweka fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya asilimia 66.7, ni fedha nyingi sana haijawahi kutokea. Humo ndani wameelekeza vizuri, iko miradi mikubwa ambayo imeelekezwa kupewa fedha nyingi ikiwemo Stiegler’s Gorge lakini pia na mradi wa REA, ni jambo jema sana. Kote huku tunalenga kuwa na umeme wa uhakika. Eneo hili tuna kila sababu ya kumsifu sana na kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na Naibu wake waweze kufikia malengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu, siku zote lazima tuiweke hofu hii kwamba fedha hizi hazifiki kwa wakati. Tunataka tuiombe Serikali tusiwe watu wa kulalamika kila siku fedha hazifiki, mikakati yote iliyowekwa hii haiwezi kutekelezeka kama fedha hazijaenda. Niiombe sana Serikali ihakikishe inawapa fedha ili hii mikakati waliyoiweka ya kuhakikisha tunapata umeme wa uhakika tuweze kupata huo umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee eneo hili la Stiegler’s Gorge. Wako watu wametolea mfano kwamba eneo hili wanakata miti ambapo unafananisha sasa ukataji wa eneo lile la miti na kilometa za mraba za Dar es Salaam yaani unafananisha na Jiji la Dar es Salaam. Ndugu zangu, Selous ina kilometa za mraba zaidi ya 50,000, Dar es Salaam ina kilometa za mraba 1,300, maana yake Dar es Salaam pale Selous inaweza ikaingia mara 35 mpaka 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilieleze jambo hili vizuri, Watanzania wanahitaji kuelezwa vizuri na ukweli. Tukisema zaidi ya Dar es Salaam kwamba tunaangalia ile miti lazima uangalie value ya mradi na ile miti inayokatwa, lakini lazima uangalie multiplying effect ya ule mradi, tunatarajia huu mradi utusaidie nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga reli kwa kiwango cha standard gauge, reli hii inatarajiwa kuwa na umeme wa kutosha, utatoka wapi? Malengo haya yaliyowekwa na Wizara ya kuhakikisha kwamba tunapata megawatt 2,100 maana yake yatatusaidia sasa hata miradi mingine ambayo inatarajia kuhitaji umeme iweze kutekelezeka, ikiwemo reli. Pia tunahitaji kuwa na viwanda vya kutosha vinahitaji umeme, Stiegler’s Gorge inaweza ikawa ndiyo suluhu ya hiyo miradi ambayo tunatarajia iweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunalalamika juu ya kutokuwepo kwa umeme wa uhakika. Pale Singida Mjini tunayo sub-station nadhani ina megawatt zaidi ya 600 lakini hata pale ilipo kuna mtaa unaitwa Kimpungua, wananchi hawana umeme. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, maeneo haya ambayo yako mjini na wako tayari kulipia gharama za umeme, maeneo haya madogo madogo ni vizuri sana Wizara ikawa makini kuhakikisha watu wanapata umeme lakini viko vijiji karibu 13 na mitaa 13 yote haina umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri wameomba fedha kwa ajili ya usambazaji wa umeme mijini, wameomba, hawana fedha. Sasa kama wameomba fedha maana yake sisi tutaendelea kusubiri maombi ya fedha, yanaweza yakakubalia au yakakataliwa ni lazima tuwe na mkakati madhubuti. Hatuhitaji kusubiri fedha zinazokuja sisi tunao umeme wa kutosha ni kuwaongezea tu bajeti ndugu zetu wa TANESCO pale wahakikishe kwamba vijiji vile na mitaa wanaweza kupata ule umeme wala hakutakuwa na tatizo lolote Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengine, Singida tumejaaliwa na rasilimali ya umeme wa jua, rasilimali nyingine ya upepo, nashukuru Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri kwenye kitabu chake na ziko fedha wametenga zaidi ya shilingi bilioni 888 kwa ajili ya umeme wa jua, niwaombe sana eneo hili sasa waliangalie na ni vizuri tukaharakisha, mchakato ufanyike mapema kwani jambo hili halijaanza leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunao upepo, nashukuru Waziri ametambua. Kwenye kitabu ukurasa wa 32 kama sikosei ametambua kwamba tunao upepo ambapo tunaweza kupata mradi wa umeme wa upepo na ametambua kampuni moja ya Wind East Africa, walikuja na kampuni nyingine ya Power Project, eneo kubwa sana la Singida ukiacha Kisaki, Mungumaji tunaenda mpaka Unyambo kule Kisasida kote kule kunafaa kwa mradi wa umeme wa upepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niiombe Serikali eneo dogo hapa, kampuni hii tumekuwa nayo zaidi ya miaka 10 sasa lakini hakuna utekelezaji, sijajua kulikuwa na mazingira gani, lakini Waziri ameeleza vizuri kwamba mchakato wa kusaini ile Power Purchasing Agreement umefikia hatua ya mwisho, well and good lakini muwape time-frame, wakimaliza huo mchakato tuwape time-frame ni lini wataanza sasa kuhakikisha mradi huu unafanyika. Kama jambo hili linashindikana niiombe Wizara itangaze rasilimali hii hadharani. Wako wawekezaji wengi watatusaidia na watahakikisha tunapata umeme, zaidi ya hii megawatt tuliyoizungumza hapa 100 tunaweza kupata hata megawatt 200 na tukaondokana na tatizo la umeme Mkoa wa Singida. Niiombe sana Serikali, tunayo maeneo mengi tunahitaji kuwa na uwekezaji wa viwanda, hatuwezi kuwa na uwekezaji wa viwanda kama hatuna umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaliwa kuwa na rasilimali kama hii, liwe eneo muhimu sana. Naomba Waziri atakapokuja ku-wind up ni vizuri tukawapa timeframe hawa wawekezaji tulionao kwa muda mrefu na sasa hivi wananchi wanalalamika sana, tufikie mahali tuweke rasilimali hii hadharani kila mtu mwenye uwezo wa kuwekeza kwenye eneo hili aje awekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo lingine, Watanzania hawa tunaowapelekea umeme hasa vijijini uwezo wao wa ku-afford unit 350 ni mdogo sana. Unit moja ina takriban 350, kesho tutakwama kwenye hili. Nataka niiombe Serikali, tunapoweka mkakati wa kuhakisha watu wanapata umeme kwenye vijiji vyote basi tuweke na mkakati wa kupunguza gharama hii, kwa sababu watakuwa watu wengi ambao wanatumia umeme. Tukipunguza gharama hii itatusaidia pia watu waache kutumia mkaa kwa wingi, tutaanza kutumia umeme kwenye shughuli zetu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri tuweke mkakati wa kupunguza hii gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wanapohitaji kuingiza umeme, tumepunguza gharama za uingizaji umeme. Kwa mjini tumeweka Sh.321,000 bado ni fedha nyingi sana, akiweka nguzo moja tu anaenda Sh.515,000 lakini vijijini tumeweka Sh.177,000, kwa nini tusiwaweke wote sawa kwa sababu wote wanatumia umeme sawa, wote wafanane kwa nini itofautiane? Kama inatofautiana, kwa nini tuweke kipaumbele kwenye REA tukaacha hapa kwenye maeneo ya miji, maeneo ya miji hayana umeme, tumewekeza kwenye maeneo ya vijijini. Niiombe Serikali iliangalie eneo hili itasaidia wananchi wengi kupata umeme na wanaweza kutumia ule umeme kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vision hii ya Wizara itatufikisha mahali ambapo lengo ama utekelezaji wa Ilani yetu ya uwepo wa viwanda vya kutosha na watu kuweza kutumia umeme kwa uhakika itatusaidia sana. Tumepitia bajeti nyingi hapa lakini mkakati kwenye bajeti hii ukiusoma vizuri na watu wakipewa fedha utatufikisha mahali ambapo tunapahitaji. Tuna kila sababu ya kuwaaunga mkono watu wa Wizara hii ili waweze kutusaidia sisi kuweza kupata umeme wa uhakika na wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kuendelea kuishukuru Serikali, mambo mengi tumekuwa tukiyasema hapa, nimuombe Waziri tunaposhauri ni vizuri mkayasema hapahapa msisubiri Rais aseme. Tulishauri kwenye maji hapa kesho Rais akatolea majibu lakini sisi hatukuweza kusema. Sasa niwaombe tuwe tunamaliza humu humu tusisubiri Rais alione hili, Rais wetu anafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naiunga mkono bajeti.