Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nianze kwa kuunga mkono hoja. Vile vile napenda kumpongeza Waziri wa Fedha kwamba baada ya kutoka Chuoni kufundisha akaja kwenye siasa. Hotuba aliyoitoa mwaka huu ya utangulizi wa Serikali hii imefanya nini, ameshahitimu siasa. Alimaliza kila kitu katika yale mambo kumi aliyoyasema yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, basi hotuba ya Waziri wa Fedha hakuna hotuba yako imenoga kama ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, upande wangu Utumishi na Utawala Bora kulikuwa na hoja kama tatu nitazieleza kwa kifupi. Kwanza ni suala la ajira, Wabunge wengi wamesimama wametaka kufahamu suala la ajira likoje. Nataka nieleze tu kwamba Serikali kwa makusudi ilisimamisha ajira kwa muda katika kipindi cha kuhakiki watumishi. Maana unaweza ukampa mtu promotion kumbe mfanyakazi yule fake, unaweza kumpa mtu promotion kumbe vyeti vyake sio halali. Ndio maana ikasimamishwa kwanza, ili zoezi la uhakiki likashakamilika zoezi lianze. Zoezi limekamilika, tumewabaini wafanyakazi hewa 19,708, tumewabaini vyeti fake 14,409, tazama pesa kiasi gani tumeokoa. Malengo ya uhakiki makubwa ni mawili:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tuwapate watu wafanye kazi ambayo wanataaluma nayo. Mtu anaingia theatre anapasua watu awe ni mtu ambaye cheti chake kinamruhusu kupasua watu. Tumewabaini watu wanavaa majoho meupe wanaingia walikuwa wanafanya operation sasa hatuwezi kucheza na maisha ya watu. Ndio maana Serikali ikasema kwanza, tuwe na uhakika kila mmoja anafanya kazi ambayo ana taaluma nayo.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine nalo Utawala Bora ni kusimamia rasilimali za umma zitumike vizuri. Unapowalipa wafanyakazi hewa, unapowalipa watu ambao vyeti vyake si sahihi, hayo ni matumizi mabaya ya fedha za umma. Kwa hiyo, nataka niseme baada ya hili zoezi kukamilika tumeshaanza ajira, mpaka Juni, tutakuwa tumeajiri watumishi 22,150 mpaka tarehe 30 ya mwezi huu.

Mheshimiwa Spika, katika hao Walimu ni 7000 tayari process ya ajira inaendelea na Afya 8000. Kwa hiyo, nataka niwaombe Wabunge wenzangu wale ambao tunasimamia ujenzi wa zahanati tusiwe na mashaka, tumalize zahanati hakuna zahanati itakayokamilika ikaacha kufanya kazi eti kwa sababu haina watumishi, tutawaajiri. Hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ilikuwa upande wa mishahara na hili limeongelewa na Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim wa Mtambile, Mheshimiwa Susan Kiwanga wa Mlimba na Ndugu yangu Mheshimiwa Mwita Waitara. Kifupi walisema kwamba, watumishi wa umma hawajaongezewa mishahara kwa muda mrefu sasa na pia hata nyongeza yao ya mwaka (increment) hawapewi. Hali hii inasababisha wanapostaafu kupata mafao kidogo. Maelezo ya Serikali ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, si sahihi kwamba watumishi wa umma hawajaongezewa mishahara kwa muda mrefu kwani nyongeza hiyo haikutolewa kuanzia mwaka 2016/2017. Kama nilivyoeleza kutokana na uamuzi wa Serikali kupitia Muundo wake na kufanya zoezi la uhakiki watumishi. Aidha, hivi sasa Serikali inaboresha utoaji wa huduma ya elimu na afya na kutekeleza miradi maendeleo ambayo itakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla katika siku za baadaye.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uwezo wa kibajeti imekuwa vigumu kugharamia utoaji wa huduma ya elimu na afya, kutekeleza miradi hiyo mikubwa pamoja na kuongeza mishahara kwa wakati mmoja. Uwezo wa bajeti utakapokuwa mzuri Serikali itatoa nyongeza na mishahara kwa watumishi wake.

Mheshimiwa Spika, tulipokuwa Iringa kwenye Sikukuu ya Wafanyakazi, Mheshimiwa Rais alisema hali ya hewa, akiona kwamba hali ya hewa inaruhusu hatangoja kupandisha siku ya sikukuu, hata ngoja kupandisha siku ya mwaka mpya, muda wowote hali itakaporuhusu mishahara itapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitoa nyongeza ya mwaka Annual Salary Increment kwa watumishi wa umma na itaendelea kutoa nyongeza hiyo katika mwaka wa fedha 2018/2019 na miaka mingine kadri ya uwezo wa bajeti utakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho lilihusu upandishaji vyeo. Hili lilitolewa na Mheshimiwa Sophia Mwakagenda na Mheshimiwa Dkt. Prudenciana Kikwembe. Hoja ilikuwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ilizuia stahiki mbalimbali watumishi ikiwemo upandishwaji madaraja kupisha zoezi la uhakiki. Kwa kuwa zoezi limekamilika watumishi wamepandishwa madaraja, kwa tarehe za sasa na sio kwa tarehe walizostahili kupanda madaraja. Hali hiyo inasababisha watumishi kustaafu na kupata mafao kidogo. Serikali iwalipe stahiki zao watumishi kwa vile zoezi la uhakiki limekamilika.

Mheshimiwa Spika, maelezo ya Serikali ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano ilizuia stahiki mbalimbali za watumishi ikiwemo upandishaji madaraja ili kupisha zoezi la uhakiki ambalo lilifanyika kwa manufaa makubwa na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali kwa kuondoka watumishi hewa. kama nilivyosema 19,708, watumishi wenye vyeti fake 14,405. Hata hivyo kwa watumishi hata hivyo kwa watumishi ambao walikuwa na barua ya kupandishwa vyeo, mishahara yao iendelee kubadilishwa katika mifumo shirikishi na taarifa za kumbukumbu za watumishi kila mwezi kwa kuzingatia tarehe walizostahili kadri ya tarehe yao ya kustaafu kazi kwa umri ilivyokaribia.

Mheshimiwa Spika, iwapo kwa bahati mbaya yupo mstaafu ambaye alikuwa na bahati ya kupandishwa cheo lakini mshahara haujabadilika hadi alipostaafu; mstaafu wa namna hii anashauriwa aende kwa aliyekuwa mwajiri wake amjazie fomu maalum ya madai ya malimbikizo ya mishahara inaitwa Mheshimiwa Spika, Salary Arrears Claims Form ili aweze kulipwa madai yake kwa njia za hundi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kama nilivyosema naunga mkono hoja.