Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukushukuru wewe kunipa nafasi hii jioni ya leo. Kwanza kabisa, nianze kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla pamoja na Naibu wake rafiki yangu Mheshimiwa Hasunga. Niseme Wizara hii ni nzito na usitegemee hata siku moja kupongezwa sana kwa sababu, inagusa watu wengi na mambo mengi. Kwa hiyo, niwapongeze kwa hapo mlipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumza habari ya vivutio vilivyopo katika Wilaya ya Kilolo. Wilaya ya Kilolo ni moja ya wilaya ambayo ina vivutio vingi sana vya maliasili ambavyo naweza kusema vimesahaulika. Moja ya vivutio ni ile sehemu ambayo Wajerumani na Wahehe walipigania pale, ni sehemu ambayo ina sifa kubwa na mpaka kusababisha jeshi letu barracks yao kuitwa jina lile, Lugalo, lile jina linatoka pale. Ile sehemu kuna makaburi ya mtu anaitwa Zelewsky au Nyundo, ambaye aliuwawa pale na Wahehe lakini kivutio kile kimesahaulika kabisa na sidhani kama kuna Waziri yeyote ambaye alishafika pale. Ushauri wangu ni kwamba, hebu tuanze kufufua vivutio hivyo kwa sababu wenzetu wa Ujerumani wanapita kila mwaka pale wanaangalia na wanapiga picha wanaondoka, hatupati kitu. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa hebu tupite pale tuangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nashukuru ndugu yangu Mheshimiwa Chumi amejaribu kuligusia, ni suala la Gereza ambalo liko kule Kilolo linaitwa Kihesa Mgagao. Ile sehemu ni nyeti sana, ni sehemu ambayo walikaa Wapigania Uhuru. Chumba alicholala Mzee Mandela kipo mpaka leo, Sisulu kuna chumba alicholala kiko pale mpaka leo, lakini cha ajabu sijui nani aliyetoa ushauri, tumeenda kufungua magereza. Leo wenzetu wa South Africa wamekuja, kuna makaburi pale, kuna familia wameacha, kuna watoto mpaka leo wameachwa pale, wanataka kuja kuangalia sehemu ile lakini hawaruhusiwi kuingia na wako tayari hata kutoa misaada mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gereza liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, ningeshauri mshisirikiane Wizara ya Mambo ya Ndani na Maliasili, ili kugeuza kile kiwe kivutio. Bahati nzuri na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje yupo leo, tufanye kivutio na wewe unatoka Iringa, ambacho tutaingiza pesa nyingi tu kama mali ya kale. Kwa hiyo, niombe hilo lifanyike na ningeomba Mheshimiwa Waziri aweze kufika pale. Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla bahati nzuri tunalima jirani kule Kilolo na yeye ni mkulima wa Kilolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la fuvu la kichwa cha Mkwawa. Ni sehemu ambayo kwa kweli sasa hivi mnaleta migogoro tu kwenye familia ile kwa sababu hakitunzwi vile kinavyotakiwa. Mmeleta mgogoro kati ya ma- chief na wananchi na Serikali yenu ambayo ni Wizara ya Maliasili. Kwa hiyo, ningeomba vitu kama vile ni vitu ambavyo havitokei kihistoria na identity ya sisi watu wa Iringa ni pamoja na vitu kama vile. Kwa hiyo, naomba mtutendee haki, tuangalie jinsi gani tunaweza tukafanya kikawa kivutio na Serikali ikaingiza fedha lakini kwa sasa hivi mmekitelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabila langu ni Mzungwa, natoka kwenye Milima ya Udzungwa ambayo ni Kilolo, Iringa, lakini leo hii unaposema Udzungwa mtu yeyote anayejua anajua ni Morogoro kiasi kwamba sisi watu wa Kilolo au Udzungwa tunapopata miradi inaonekana kama ni hisani siyo haki yetu. Bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla bado alikuwa yuko masomoni, lakini wanaojua Udzungwa ilipokuwa inaanza waliweka makao makuu Morogoro kwa sababu ilikuwa hamna njia ya kupita kwa kupitia njia ya Iringa lakini leo hii inaonekana beneficiary ni watu wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba aidha, sisi watu wa Iringa mtuhamishie Morogoro au tunufaike na mbuga hizo ikiwa ni pamoja na kutengenezewe barabara na miundombinu mingine. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, wewe ni msikivu sana hebu lifanyie kazi hilo. Itakuwa siyo vizuri tutakapokuja kwenye bajeti ijayo, tukazungumzia kitu kilekile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Mbuga za Udzungwa kuna Vijiji vya Ruaha Mbuyuni, Mahenge na Mgowelo, kuna shida kubwa sana ya wanyamapori. Tembo wamekuwa wakiuwa sana binadamu lakini kile kifuta jasho kimepitwa na wakati. Mimi ningefikiria hebu tushauriane kwanza tuongeze kifuta jasho lakini ulinzi ule shirikishi kati ya wananchi na Afisa Wanyamapori uwe karibu. Nimshukuru sana Mhifadhi Mkuu wa Kikosi cha Ujangili cha Mkoa wa Iringa jinsi ambavyo amekuwa akitupa ushirikiano. Kwa hiyo, niombe tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la Ruaha National Park, niishukuru sana Serikali kwa kuamua kuboresha mbuga ile kwa kupeleka barabara ya lami na pia kwa Serikali kuamua kununua ndege. Kwa kawaida huwezi kuona faida ya ndege zile usipochanganya na utalii. Sasa hivi utalii utapanda kwa sababu watalii wengi watafika kwa sababu wanaweza kufika na ndege zipo na uwanja wetu wa Nduli Airport utakuwa umeboreshwa, kwa hiyo, tutapata wageni wengi. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa kununua ndege zile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya wafugaji na hifadhi. Watu wengi wamelalamika, bahati nzuri nilishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya, migogoro hiyo ipo siyo ya kuibeza. Changamoto ninayoiona mgogoro ule anaachiwa Maliasili peke yake wakati ukiangalia ni mgogoro mtambuka Wizara zinatakiwa zishirikiane, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ardhi na Wizara ya TAMISEMI. Kwa sababu wanyama ni wa Maliasili, ardhi iko chini ya Wizara ya Ardhi na wale binadamu pale wako chini ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wangeshirikiana, wakajiuliza ni kwa nini wafugaji wanaingia kwenye hifadhi, ukiweza kujiuliza hilo swali mgogoro wote utakwisha. Kama mnataka kujua tatizo hili likoje, nafikiri mkakae pamoja na ikiwezekana tuunde mfuko wa pamoja wa hizi Wizara nne tuweze kutenga fedha na kufanya utafiti wa kina na kutoa elimu ya kutosha. Ni kweli wafugaji wanapata shida lakini kuna mambo ambayo yanasababisha mojawapo ni upimaji wa ardhi, watu wameshalalamika kwamba tuangalie, je, ni kweli Wizara ya Maliasili imeingia ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kulaumu Wizara wala Waziri ni vijana wenyewe wana matatizo, hasa hawa ambao wako kwenye hifadhi wa kikosi maalum kile cha kuzuia ujangili. Wanafanya kazi yao vizuri lakini inafikia mahali wanapitiliza, wanaweza wakaenda nje ya mipaka yao ya kazi. Kwa hiyo, nafikiri tukiunda tume ya pamoja au mfuko wa pamoja wa hizi Wizara nne tunaweza tukatatua tatizo hili ambalo linawasumbua wenzetu wafugaji, wamekuwa wakilia kwa muda mrefu bila suluhisho. Kwa hiyo, tuwasikilize kwa sababu ni wenzetu na mifugo ni yetu, wanyama ni wetu, hatutaki kuona wanyama wale wanapata matatizo kwa sababu tunahitaji hifadhi na fedha za kigeni, lakini hatupendi pia kuona wafugaji na mifugo yao wanapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wale ambao wamelalamika kwamba mifugo yao imeuzwa, tuwasikilize. Kwa kupitia tume hiyo, tutakuwa tumetatua. Niiombe tu Serikali iwasikilize ili tuweze kutatua tatizo hili. Kwa sababu mimi najua Rais wetu ambaye yupo sasa hivi ni Rais wa wanyonge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo, niunge mkono hoja hii.