Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Mawaziri pamoja na taasisi zilizopo chini yake. Pia nitoe pongezi za pekee na niseme labda ni shukrani kwa Wakala wa Misitu Tanzania kwa sababu mara ya kwanza nilipoingia hapa Bungeni nilizungumza sana juu ya umuhimu wa Wakala wa Misitu kukutana na wadau wa sekta ya misitu hasa walioko katika Jimbo la Mafinga Mjini na Wilaya ya Mufindi. Nawapongeza kwa sababu mwaka jana kabla ya msimu tumefanya kikao na mwaka huu alikuja Mtendaji Mkuu Profesa, tarehe 30 Aprili. Tumesikilizana na wadau, naamini Wakala wamechukua mawazo yao na watayafanyia kazi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kufanya kazi kwamba tunapotoa ushauri kwa Serikali ikiuchukua na kuufanyia kazi inakuwa ni kwa manufaa yetu sisi na wananchi wetu kwa ujumla wake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nizungumzie changamoto chache ambazo ziko kwenye sekta ya mazao ya misitu. Moja, tulipokutana na wadau walizungumzia lile suala ambapo ukishafanya malipo ili uingie msituni kuvuna unapewa siku zisizozidi 30 uwe umeshamaliza kuvuna na zile siku 30 zinahesabia Jumamosi na Jumapili. Sasa nitoe mfano, kama huo mwezi tarehe 1 imeanza ni Jumamosi maana yake kuna siku takribani 10 zitakuwa Jumamosi na Jumapili. Maana yake ni kwamba huyu mdau anakuwa ana siku 20 tu, zile 30 zinakuwa ni kwa maneno. Kwa hiyo, niiombe Serikali hususani Wakala wa Misitu, hebu tuangalie, mtu akishalipia zile tunazoita siku 30 basi ziwe siku 30 za kikazi, tusijumuishe Jumamosi na Jumapili na pia tuondoe kama hapo katikati kutakuwa na siku za sikukuu ili kumpa huyu mtu nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi na kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni changamoto katika check points. Watu wa mazao ya misitu hususani mbao, nguzo na mirunda kuna zaidi ya check point karibu 10 na nitazitaja kwa haraka. Kwa mfano, mtu akitoka kule Mufindi anakutana check point Mtiri, Makwave, Lungemba, Tanangozi pale kwenye kaburi la Kiyeyeu, Igumbilo, Ruaha Mbuyuni, Sangasanga pale kwenye njiapanda ya kwenda Mzumbe, Chalinze, Vigwaza na Kiluvya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi tunapoelekea uchumi wa viwanda watu wanaosafirisha mazao ya misitu hususani mbao, mirunda na nguzo hawaruhusiwi kusafiri mara baada ya saa 12.00 jioni. Sasa imagine mtu anatoka Mafinga anakwenda Mwanza atatumia wiki nzima kufika Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa kuwa tayari tuna check point na kuna magari yanafanya patrol hebu turuhusu watu wasafiri usiku, kwa sababu tuna slow down speed ya kukuza uchumi katika Taifa. Sehemu ya kutumia siku mbili, kwa mfano, mtu akitoka Mafinga kufika Dar es Salaam sanasana ni siku moja lakini analazimika kutumia siku tatu. Maana yake ni nini? Kwanza umeongeza gharama za uendeshaji kwa mwenye gari na matokeo yake yule mtu ataziongeza zile gharama kwa mwenye mzigo matokeo yake mlaji wa mwisho atajikuta anapata mzigo kwa bei kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, kwa kuwa tuna check point na tuna magari ambayo yanafanya patrol hebu turuhusu hili kusudi tukimbize uchumi. Kwa sababu hawa watu, kwa mfano, wenye magari wanaosafirisha mizigo hii wanajaza mafuta; maana yake ni kwamba kama akienda akirudi mara nyingi tayari pia Serikali itakuwa imepata fuel levy. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kulitazama suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo napenda kulizungumzia pia ni kwenye sekta hii ya misitu. Pale Mufindi, Mafinga kulikuwa na majengo ambayo yalikuwa ni madarasa, ofisi za walimu na mabweni kwa ajili ya chuo kidogo cha masuala ya mazao ya misitu. Sisi watu wa Mafinga, Mufindi na Nyanda za Juu Kusini tunaomba tuwe na chuo ambacho kitafundisha masuala haya ya mazao ya misitu. Kwa nini nasema hivi? Sisi ndiyo wenye msitu mkubwa Afrika ya Mashariki na Kati maana yake ni kwamba hata mazoezi kwa vitendo lakini pia hata wale ambao watakuwa wamejifunza iwe rasmi au kwa mafunzo ya muda mfupi watatumika katika viwanda mbalimbali ambavyo wawekezaji wamewekeza katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kikao cha wadau tulizungumzia umuhimu wa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo kuhakikishiwa malighafi. Wawekezaji hawa wanachukua mikopo iwe ya ndani ya nchi, nje ya nchi, benki za ndani au kwa namna nyingine yoyote wenye mabenki wanasita kuwapa mikopo kwa sababu hana guarantee ya kupata material. Kwa hiyo, niombe Wakala wa Misitu, kama walivyosema katika ukurasa wa 38, Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba ameunda kikosi kazi ambacho kitapitia hali ya upatikanaji wa material katika Kiwanda cha Mgololo. Hawa wawekezaji kuanzia Mgololo, Sao Hill na wawekezaji wengine siwezi kuwataja kwa majina pale Mafinga Mjini wanahitaji kuwa guaranteed kupata material ili kusudi waweze kuwa na uhakika wa kuchukua mikopo ambapo kweli wenye mabenki wataweza kuwadhamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, hawa wawekezaji, nisome kipengele kimoja katika Biblia, 1 Timotheo 5:8 inasema, mtu yeyote asiyewatunza na kuwathamini wale wa nyumbani kwake hasa, ameikana imani tena ni mbaya kuliko asiyeamini. Sasa mimi wa nyumbani kwangu ni nani? Mimi wangu ni pamoja na wapiga kura lakini na hawa wawekezaji ambao wakiwa guaranteed material mimi siasa zangu zinakuwa nyepesi kwa sababu ni kazi sana kuongozo mwenye njaa lakini hawa watu wakiwa na material maana yake watu wangu watapata vibarua, watapata kazi, watapata kipato chao na watakuwa na mchango wa uchumi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa kuhusu TANAPA kutozwa kodi. Mara kadha hata Mheshimiwa Rais amesema na mimi nilikuwa wa kwanza kusema humu ndani, nchi yetu ina vivutio vingi, lakini hata makampuni ya soda, jiulize Coca Cola, Pepsi kila siku wanatangaza, nani asiyeijua Coca Cola au Pespi? Kila mtu anaijua. Kwa hiyo, mimi nashauri hizi gharama ambazo mnaikata TANAPA bora mngewaachia kwa kiwango fulani ili kuwaongezea nguvu TANAPA na Ngorongoro ya kujitangaza na pia kuiwezesha TTB ili kusudi vivutio hivi viweze kweli kuleta watu. Biashara yoyote ni matangazo, sasa utatangaza wakati bajeti yenyewe ni ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, katika Mkoa wa Iringa kuna maeneo mengi ambapo wapigania uhuru akiwemo Mandela na Sam Nujoma wamepita. Niiombe Serikali, kwa mfano, kuana eneo la Kihesa Mgagao, sisi tumelifanya gereza lakini kumbe lile eneo tungelifanya la makumbusho hata watu wengi kutoka Kusini mwa Afrika wangeweza kwenda pale na kuona kwamba, ala, kumbe Mandela alipita hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo Sam Nujoma alitumia jina kama Sam Mwakangale ili aweze kupata passport ya Kitanzania kuendesha harakati zake za uhuru wa Namibia. Hebu tuyang’amue hayo maeneo nayo tuongeze katika sekta yetu ya utalii, yatatupa mapato kuliko ambavyo tumeyafanya yapo chini. Hizi Serengeti na kadhalika pamoja na kuwa tunazitangaza lakini tuyatambue maeneo hayo tuwekeze katika utangazaji ili kusudi mapato yaweze kuongezeka katika utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, niishauri Serikali, hebu ijaribu kufikiria kuhusu single entry. Single entry inaumiza wadau ambao wako kandokando ya mbuga za wanyama. Hawa ni part na parcel wa kunufaika na mbuga lakini kutokana na single entry matokeo yake watu hawa wanakuwa idle, vijiji havizalishi na hatimaye wanajiingiza katika shughuli ambazo si salama na ni illegal katika mustakabali mzima wa sekta yetu ya maliasili na utalii. Kwa hiyo, hebu Serikali ijiridhishe, mimi naamini ina mbinu za kutosha kuweza kudhibiti ile sababu iliyosababisha kuwepo na single entry ili kufanya pia vijiji vinavyozunguka mbuga viweze kuwekeza navyo viweze kupata watalii lakini pia watalii waweze ku-enjoy mbuga zetu na tamaduni za wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nashukuru sana.