Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri na kazi nzuri inayofanyika katika Wizara.

Mheshimiwa Spika, niongelee kuhusu Ranchi za Taifa. Kumekuwa na malalamiko makubwa ya siku nyingi kuhusu wananchi wanaoishi karibu na Ranchi za Taifa maeneo yaliyogawanywa katika blocks (vitalu) kukosa malisho. Wananchi wanaoishi Misenyi katika Kata ya Kakunyu, Kijiji cha Bubale na vijiji vingine katika kata hiyo maeneo yao yalitwaliwa, watu wakagawiwa blocks na wananchi wazawa/wakazi wakakosa mahali pa kulima na kufugia. Wamesema, wamepiga kelele, wamepaza sauti lakini sauti zao hazisikiki.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amesema wale walioshindwa kuendeleza vitalu walivyopewa watanyang’anywa wapewe wawekezaji wengine wenye ng’ombe wengi. Nauliza swali, vipi sasa hawa wananchi wakulima/wafugaji ambao maeneo yao yalitwaliwa na hawana maeneo? Kwa kuwa kwenye vijiji hivi watu wameongezeka (population), naomba yatengwe maeneo zaidi na haya yarudishwe kwa wananchi wa kawaida ambao ni wakulima/wafugaji.

Mheshimiwa Spika, pili, hawa wafugaji wadogo wadogo wanahitaji kuendelezwa. Waliambiwa wajiunge kwenye vikundi vikundi watapewa maeneo ya kufugia. Napendekeza tusipendelee wawekezaji peke yao, itafutwe namna ya kuwaendeleza wafugaji wadogo wadogo pia kwa kuwapa maeneo ya kufugia, kuwapa elimu juu ya uboreshaji wa malisho na mifugo. Bajeti hii haioneshi ni kwa namna gani inapanga kumuendeleza mfugaji mnyonge.

Mheshimiwa Spika, sababu ya uvuvi uliopitiliza (over fishing), samaki wamepungua sana kwenye Ziwa Victoria. Ili kulipunguzia mzigo Ziwa Victoria, kuongeza samaki na kuwaletea mapato wananchi na hivyo kukuza uchumi ni vizuri wananchi wakaendelea kuhamasishana ili wafuge samaki.

Mkoa wa Kagera watu wengi wameitika/wamehamasika, wamechimba mabwawa na kufuga samaki, tatizo hao samaki hawanenepi hata baada ya miezi nane au kumi bado wanakuwa na uzito mdogo sana. Tatizo ni kuwa wakulima hawajui mbegu bora iko wapi, hakuna Maafisa Ugani wa kuwashauri wafugaji wa samaki na pia chakula sahihi ni shida. Je, ni lini Serikali itatenga pesa za kutosha na kuendeleza ufugaji wa samaki wa mabwawa?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.