Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Ninaamini nina dakika kumi.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu mkubwa sana katika sekta ya uvuvi pamoja na mifugo, ndiyo maana ameiweka Wizara hii ili tuweze kupata nafasi kubwa sana katika kujadili changamoto zote zinazogusa sekta hii. Kwa hiyo ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa kwamba pasipokuwa na changamoto, hakuna mafanikio. Kwa hiyo, ninaamini kwa changamoto zote zinazojitokeza katika sekta ya uvuvi pamoja na mifugo ndiko tunakoelekea kwenye mafanikio. Ninaomba sana Wizara ipokee changamoto hizo na izifanyie kazi kwa sababu ndiyo hasa ilikuwa kusudio la Mheshimiwa Rais ili kuweza kuwasaidia wale wananchi ambao wanaguswa na sekta hii.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Singida tuna ufugaji. Kwanza ni wafugaji lakini pia wakulima, tumekuwa na ufugaji mzuri na ukulima bila migogoro kwa muda mrefu sana. Migogoro huwa inakuja pale wageni wanapokuja kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo wenyewe hatukuwa tumekusudia kwa ajili ya kulisha mifugo lakini Serikali za Mkoa, Vijiji na Wilaya wemekuwa wakijadili na kuingia muafaka.

Mheshimimiwa Spika, kuna jambo ambalo Mheshimiwa Waziri katika taarifa yako, sielewi kama kweli unaona ufugaji wa kuku ambao hasa uko katika Mkoa wa Singida ni sehemu mojawapo ya kuwaondolea umaskini Watanzania, pia ni kipato kinachotokana na ufugaji wa kuku, sijaona kama umetilia mkazo. Singida kuku ni chanzo cha kipato, lakini bado ni chakula na ni utamaduni wetu. Hata mtoto mdogo ukienda kumtembelea shangazi, anakupatia kuku kwa ajili ya kwenda kumfuga, kumuendeleza. Ni utamaduni wetu mgeni akifika ni lazima kwanza mboga ya haraka ni kuku. Waziri unatakiwa sasa uwatoe wananchi wa Mkoa wa Singida kwenye utamaduni kwamba ni ukarimu tu, iwe ni biashara tena biashara yenye tija kwa wananchi wa Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wataalam walioko kule uwape maelekezo kama ambavyo mnaweza kutoa maelekezo kwenye mazao mengine, pia kwenye ufugaji wa kuku utoe maelekezo wataalam waende wakawasaidie na kutoa dawa, wafuatiliwe ili kuweza kukuza ufugaji wa kuku wa Singida ambao ni watamu sana wote mnafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka kwenye eneo hilo niende kwenye uvuvi. Na sisi pia tuna uvuvi Singida, ukienda Ziwa Singidani na Kindai. Pia nataka nizungumzie Kitangiri. Kwanza nataka ieleweke na Waziri utakaposimama hapo useme, Wilaya ya Iramba ndiyo yenye Ziwa Kitangiri, useme hapa leo ili wananchi wote wasikie, kwa sababu Kitangiri tunaita Kiteka, wavuvi wanaovua pale wanaotoka upande wa Meatu, kwanza Serikali ya Halmashauri ya Meatu haitendei haki Serikali ya Halmashauri ya Iramba.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Iramba inapofunga ziwa lile kwa ajili ya kuhakikisha vifaranga wale wanakua, Meatu hawafungi na wakati haiko kwao! Ushuru wanapokea wao, hela zile haziji Iramba, kwa hiyo tunawadhulumu na hatuwatendei haki wananchi wa Iramba na Meatu wanakaribisha watu kutoka maeneo mengine. Wanapokea ushuru, unanufaisha Halmashauri ya Meatu. Sawa, sikatai lakini ninaomba taratibu zifuatwe. Iramba inaposema tunafunga ziwa hili, Meatu pia watangaze, wafunge! Pia ninaomba sana boti iletwe kwa ajili ya kufuatilia wale wavuvi haramu ambao hawana leseni na vibali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna mkondo wa maji ambao umekuwa ukipitisha maji kwenda Kitangiri. Kata za Igunga wamekuwa wakilima kwenye mkondo ule kiasi kwamba inatishia Kitangiri kuondoka. Mheshimiwa Waziri naomba utakapoongea hapo utuambie unatulindia vipi Kiteka yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikimaliza Mkoa wa Singida mimi naomba niseme hivi, kuna suala la operation linaloendelea. Mheshimiwa Mpina una baba zako, una wadogo zako, una kaka zako, wote wako kwenye uvuvi, hata kama hujazaliwa nao kumbuka kila mtoto au kila mwanaume au kila mwanamke ni mtoto wa mwanamke aliyezaliwa na wanawake kama sisi. Ni hakika wale wavuvi hawatendewi haki. Mnapokamata zile nyavu unazichoma, kumbuka ameacha familia nyuma inamtegemea, kumbuka ana wazazi wake wanamtegemea, kwa nini usiende na utaratibu mzuri? Nyang’anya zile nyavu lakini lete mbadala wape nyavu nyingine, hata kama watalipia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwa kweli siungi mkono hiyo operation ni uchungu kwa sababu na mimi nina ndugu zangu wako kule. Kwa hiyo, naomba mnapochoma yale sijui makokoro, sijui kitu gani, naomba peleka nyavu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ameongea hapa Mbunge mmoja kwamba wasomi mliopo huko msifanye kazi kama watu ambao hamkwenda shule. Mheshimiwa Rais amewaweka hapo ili muwasaidie Watanzania na ili msaidie sekta hiyo. Kwa kweli hatuungi mkono uvuvi haramu, lakini ile operation namna mnavyoiendesha kwa kweli haitendi haki kama binadamu wengine. Kwa hiyo, suala hilo naomba sana liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna jambo lingine hili la kuwabandika ng’ombe moto. Jamani, chuma cha moto kwenda kumbandua ng’ombe na kumfanya awe na kidonda. Mimi nimekutana na ng’ombe ana kidonda hakiponi. Naomba mtafute namna ya kuweka chapa wale ng’ombe. Jamani, kwanza tunaharibu ile ngozi halafu ng’ombe anakonda. Naomba sana Mheshimiwa Mpina, wataalam wapo na mmesoma kwa kweli, tafuteni namna ya kutia chapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli, tunajua tunataka tudhibiti ng’ombe wanaotoka katika nchi jirani, lakini kwani mtu akisajili ng’ombe wake akasema Mheshimiwa Mlata ana ng’ombe 100, kesho mkimkuta ana ng’ombe 200 si atajieleza kawapata wapi? Tafuteni namna, basi wawekeeni hata vidani, wawekeeni kitu chochote wale ng’ombe jamani, tusiwatese jamani. Kwa hiyo, hilo mimi nilikuwa naomba liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, sisi tulikuwa tunapokea ng’ombe kutoka Meatu, Maswa, wanakuja pale Singida kupakia. Mabehewa yalikuwa yanapakia kupitia hii reli ya hapa Manyoni, lakini siku hizi usafirishaji wa ng’ombe umekuwa ni mgumu kwa sababu ile treni haiendi tena. Sasa sifahamu mna mawasiliano gani na sekta ya uchukuzi ili kuwapunguzia ng’ombe msafara mrefu, wengine wanafia njiani kwa sababu ile reli ilikuwa inarahisisha sana yale mabehewa kupakia ng’ombe wengi lakini na sisi Singida tulikuwa tunaweza kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, boresheni ranchi zenu, ukienda Kongwa kwa Mheshimiwa Spika, yale majani yanaota mpaka yanakauka, hakuna chochote kinachopatikana. Wekeni utaratibu mtu akiingiza ng’ombe mmoja mwambie kiasi fulani, mtu alete ng’ombe wake, alishe, kusanya hela, muwekee maji pale, alipie kama kuna matibabu, hebu fanyeni biashara kisomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.