Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, nami kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana na tukajadili mambo ya nchi yetu, lakini jambo lingine niwatakie heri ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Waislam wote Tanzania na duniani kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa kuzungumzia hali ya uvuvi Tanzania katika kitabu cha Wizara ukurasa wa 82 ambapo pana takwimu zimetolewa hapa kwamba Ziwa Victoria kwa mwaka kuna tani 2,143,248; Ziwa Tanganyika tani 295,000; Ziwa Nyasa tani 168,000; Bahari ya Hindi tani 100,000 maji ya Kitaifa ambapo ninavyoamini ni katika ule ukanda unaoanzia Jasini karibu na Kenya mpaka Msimbati ambapo ni kilometa 1,425 na mabwawa madogo madogo yanazalisha tani 30 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi sikubaliani nazo. Haiwezekani ikawa Ziwa Victoria litoe samaki tani 2,143,000 lakini ukanda wote wa bahari wa maji ya Kitaifa utoe tani 100,000 tu! Naomba Waziri atakapokuja atupe takwimu sahihi au labda niwe nimeelewa vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie hali ya uvuvi katika nchi yetu kwa ujumla. Wataalam wanasema if you fail to plan, you plan to fail, hapa ndiyo ninapoona pana tatizo, kwa sababu haiingii akilini kwamba Wizara badala ya kukaa na wavuvi kuwaelimisha elimu ya uvuvi wa kisasa, nyavu zinazotakiwa kisheria, vilevile pia kuwapa elimu ya madhara ya uvuvi haramu sasa kazi yetu imekuwa ni kuanzisha operation. Operation haitengenezi jambo na waswahili wanasema kosa siyo kutenda kosa, kosa ni kurudia kosa.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma kulikuwa na Operation Tokomeza, ikaleta balaa kubwa katika nchi yetu. Wafugaji waliuawa, ng’ombe wakapigwa risasi na hali ikawa mbaya katika nchi. Sasa inakuwaje Waziri Mpina sasa naye badala ya kurekebisha makosa anarudia makosa anatuletea operation! Naona hapa haliko sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, nimtake atakapokuja, hivi katika fikra zake zote kama Waziri aliyeaminiwa na Rais Magufuli, hana plan ya kufanya ni lazima aendeshe kwa operation. Wavuvi hawataki operation, naamini kwamba wavuvi ni watu ambao ni waelewa, wavuvi wamejaribu kuunda vyama vyao vidogovidogo lakini hata katika kanuni ambazo zinaanzishwa za uvuvi hawashirikishwi.

Mheshimiwa Spika, jana tulikuwa na baadhi ya wavuvi hapa, malalamiko yao ni hayo. Wameandika barua tarehe 25 Julai, 2017 wakaambiwa kwamba wataitwa na Waziri, watakaa naye kikao ili warekebishe mambo, matokeo yake mpaka bajeti inaletwa hapa, Waziri hajawaita. Kama hilo halitoshi, katika hiyo Operation Sangara, kuna kitu ambacho mpaka sasa hivi sielewi. Nilisikia kwenye taarifa ya habari kwamba hata mama lishe wanahusishwa na uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, mama lishe kazi yake ananunua samaki, amewapikia chakula wavuvi, mama anaambiwa atoe faini shilingi milioni mbili halafu banda lake la mama lishe linachomwa moto. Najiuliza sasa, huyu Waziri Mpina anayefanya ukatili huu ni kweli amezaliwa na mama? Kwa sababu ni lazima akina mama tuwaonee huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kwa taarifa yako akina mama baada ya kukosa ajira, ndiyo wanaolea familia. Sasa leo matokeo yake mama lishe wanachomewa mabanda yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kuwachomea wavuvi nyavu. Kwetu baharini na hata kwenye maziwa, Tanga kuna dagaa wale wadogo wadogo wanaitwa uono, Mwenyezi Mungu ndiyo alivyowaumba hivyo kama hivi binadamu kuna wengine warefu, wengine wanene, wengine wafupi; uono, dagaa wa Mwanza na dagaa wa Kigoma yale ndiyo maumbile yao. Sasa unapomwambia mvuvi avue na nyavu ya nchi nne au nyavu ya nchi mbili atamvuaje dagaa yule? Hebu watutafutie njia mbadala, mnapowakataza Watanzania wasivue, ujue unahatarisha ajira ya zaidi ya asilimia 36 ya Watanzania ambao utawafanya wasiwe na ajira.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpina atakapokuja hapa ku-wind up atueleze ni nyavu zipi zinazoweza kuvua uono, dagaa wa Mwanza na dagaa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi, Operation Jodari. Hii operesheni katika ukanda wetu wa Pwani imekuwa ni balaa, ni tatizo. Wavuvi wanalishwa samaki wabichi, wavuvi wanalishwa pweza wabichi, sijui kama unamjua pweza alivyo akiwa mbichi anavyokuwa. Mtu analazimishwa amle mbichi, hivi Mheshimiwa Waziri kama ni yeye angeweza kula pweza mbichi? Kwa nini tuwafanyiwe wavuvi ukatili kiasi hiki? Kwa sababu uvuvi unaingiza asilimia mbili ya Pato letu la Taifa. Ilikuwa ni kiasi cha kukaa nao na kuwaelimisha ili tupate mapato mazuri kwa Serikali lakini matokeo yake ni kuwapiga, wengine wanapigwa risasi.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Tongoni Tanga yupo mvuvi amepigwa risasi kwa sababu eti ni mvuvi haramu! Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje atupe njia mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la leseni, leseni kila baada ya miaka miwili inapandishwa bei, kwa nini chombo kimoja kina wavuvi zaidi ya 25 wote wawe na leseni? Ninavyojua mtumbwi ni sawasawa na basi au gari. Anatakiwa kepteni awe na leseni, wale wengine ni kama Wasaidizi wa kuvuta nyavu za jarife na kutupa mishipi, kwa nini kepteni awe na leseni, wavuvi wawe na leseni, chombo kiwe na leseni, samaki walipishwe ushuru, huu ni uonevu. Tunamtaka Waziri aondoe leseni kwa wavuvi, leseni ibaki kwa kepteni peke yake kama ilivyo leseni kwa dereva wa basi, kondakta hana leseni na tanboy vilevile hana leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, tuwape elimu wavuvi wawe wavuvi bora na wa kisasa. Amesema msemaji mmoja hapa kama sikosei Mheshimiwa Bashe kwamba katika Katiba ya CCM Ibara ya 7 inazungumzia majukumu ya CCM ni kulinda haki na kuhakikisha kila mtu anapata haki yake kutokana na kazi anayoifanya. Ninawashauri wavuvi mpo hapa, kama mtaona haki yenu hamuipati tishieni kama vile wenzenu wanavyofanya kurudisha kadi za CCM. Sasa hivi operation zitasimamishwa na ninyi mtabaki salama, lakini mkiendelea kuwa kimya, operation zitaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya mifugo, Tanzania ni ya pili kwa mifugo katika Bara la Afrika, lakini tujiulize ni wananchi wangapi wanakula nyama? Kama hilo halitoshi kwenye suala la upigaji chapa, tunatumia gharama kubwa lakini ni kuharibu ngozi.