Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii inaonekana ndiyo Wizara ambayo itakuwa ngumu safari hii kwenye Bunge letu. Namuomba ndugu yangu Mheshimiwa Mpina ambaye anatoka eneo la wafugaji wa ng’ombe, tunaotoka maeneo ya ufugaji tunaomba hizi ranchi kwa mara ya kwanza ziruhusiwe wananchi wetu waweke ng’ombe mle, walipie officially Serikalini ili Serikali na Wizara yake ipate pesa badala ya sasa hivi pesa hizo zinaenda kwa watunzaji wa hifadhi hizo. (Makofi)

Mheshmiwa Spika, leo tunahangaika watu wanachukua ng’ombe kutoka Usukumani kwenda mpaka Lindi, lakini tuna Ranchi ya Mwabuki ambayo inaweza kuchukua ng’ombe zaidi ya 500,000 mpaka milioni moja. Wizara kama itaruhusu ng’ombe laki tano au milioni moja wakakaa pale Mwabuki, kutajengwa automatically viwanda vya maziwa, vitajengwa viwanda vya nyama bila hata shuruti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ranchi hiyo haina ng’ombe zaidi ya 500. Kuna fisi, kuna nguruwe, hakuna kitu chochote. Ingekuwa vizuri Wizara ikaanza kuchukua action.

Mheshimiwa Spika, tuna pori ambalo linatokea Kahama mpaka Kigoma, Mheshimiwa Dotto alikuwa analia sana mara nyingi maana yake amepakana nalo. Pori hilo lina urefu wa kilometa 400, upana kilometa 250. Halina wanyama, siyo National Park kwamba watalii wanaenda, kwa nini Serikali isitoe hata asilimia kumi ikaruhusu watu wakaweka ng’ombe zao na wakalipia officially Serikalini na ikapata mapato na wananchi wetu wakapata malisho.

Mheshimiwa Spika, nawalaumu sana wataalam wa mazingira, ni kweli wanatupotosha na ni waongo. Ng’ombe hali miti wala hali udongo, ng’ombe anakula nyasi. Ng’ombe akila nyasi kwenye pori wakati wa kiangazi moto unapokuja unainusuru ile miti. Wataalam wanatuletea maneno ya Ulaya ya uongo kwamba ng’ombe akiingia kwenye lile pori ataharibu, ataharibu nini.

Mheshimiwa Spika, pori lile ni nusu ya nchi ya Uganda. Ni kweli ng’ombe waliopo pale wanaweza kudhuru nini? Leo wako ng’ombe pale wanatozwa pesa na watu wanapata pesa hakuna kitu chochote. Ni vizuri Mheshimiwa Mpina Serikali yako ili ipate pesa, ruhusu watu wachunge officially, uwatoze pesa officially, lakini wananchi wetu watapata manufaa na maendeleo pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda kwenye suala la uvuvi. Mimi kwangu sina ziwa wala mto lakini makao yangu ni Mwanza. Ukweli hali inayoendelea kule Kanda ya Ziwa ni hatari na sijawahi kuiona kwa zaidi ya miaka 30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mji wa Mwanza, ukiondoa kilimo, ukaondoa na dhahabu kinachofuata ni samaki. Leo hali iliyopo kule ni hofu, sijawahi kuiona kwenye maisha yangu. Mwananchi wa kawaida anakatazwa kubeba samaki kwenye pikipiki anakimbizwa, kwenye baiskeli anakimbizwa, matokeo yake haijulikani hasa samaki wanatakiwa kupigwa marufuku au inatakiwa nini. Kama kuna tamko la Serikali, basi Serikali itamke kwamba imesitisha ulaji wa samaki kwa muda hadi hapo itakavyojulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wavuvi hawa wanaosemwa, kweli siungi mkono uvuvi haramu lakini hawezi akakosea mtu mmoja tukaamua kwenda kupiga watu wetu kwa model hiyo, kwa kweli nakataa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lawama kubwa naitupa kwa wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nchi zinazoongoza duniani sasa hivi kwa uuzaji wa samaki, siyo nchi zenye maziwa wala bahari, nchi ya Thailand ndiyo inazoongoza kwa samaki, Serikali inatoa vifaranga milioni 200 kila mwezi, inawapa raia wake wafuge ama kwenye malambo, mabeseni, ndoo, baada ya miaka miwili, samaki walio nchi kavu ni wengi kuliko waliopo ziwani. Kwa matokeo hayo, Mheshimiwa Mpina na wataalam wake ambao tunawaita wachawi wa kizungu, maana wasomi wenzetu tunawaita wachawi wa kizungu, wenyeji wanaitwa wachawi wa kienyeji ni kweli!

Mheshimiwa Spika, viongozi wetu ambao ni wasomi, msomi kugeuka kuwa mgambo kwenda kupiga raia inahuzunisha sana. Kazi hiyo ilitakiwa ifanywe na mtu ambaye hana degree, siyo kama Maprofesa alionao nao Mheshimiwa Mpina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kama wataalam wasingetengeneza mayai ya kizungu, leo mayai ya kienyeji yangekuwa shilingi 5,000. Wataalam wasingetengeneza kuku wa kizungu, leo kuku wa kienyeji angekuwa shilingi 50,000. Wenzetu wasomi wao walikaa wakafikiri, badala ya kugombana na wananchi wakaja na solution, solution hiyo ndiyo inayotufanya leo hatujaamka kwenda kugombana na wananchi wanaofuga kuku na mayai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wazalishe samaki, warudishe mbegu za samaki kila mwezi ziwani, wawagawie na wananchi mbegu za samaki bila kupeleka maneno yao ya mazingira, bila kupeleka maneno yao ya uongo ya mazingira, uongo mtupu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mpina ajaribu kupunguza jazba. Ni kweli wananchi kule hawana nyavu. Nyavu zinazotengenezwa zinatoka Kiwanda cha Sunflag, kiwanda hiki kinatengeneza vyandarua hata kama tutaficha, lakini kweli nyavu hizo zinaweza kuvua samaki? Vyandarua haviwezi kuvua samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Mpina, asituone Wabunge kama ni watu wabaya, wote tunategemea samaki, tuna biashara zetu kule ambazo siyo samaki lakini zina uhusiano na samaki, hatuwezi kukataa, maeneo yetu yote yale yanahusika na samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwangu Kahama samaki wanaliwa. Population ya watu imeongezeka, ulaji wa samaki umeongezeka, haiwezekani wataalam wetu, watu waliosoma kwa gharama kubwa wanang’ang’ana tu kupiga watu badala ya kung’ang’ana kutafuta ufumbuzi! Kama ndugu zetu wazungu walivyoleta ufumbuzi wa kutengeneza mayai, wakatengeneza na kuku wa kizungu, leo hatuna mgogoro unachagua mwenyewe unachotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kweli leo Maprofesa wazima wanaungana kwenda kupiga watu! Uzuri na Mheshimiwa Profesa Kabudi kama yuko hapa ingekuwa ni wanasheria au madaktari wangesimamishwa kwa ajili ya degree zao lakini sijui kwa degree zingine kwamba sheria inasemaje kama mtu aliyesoma anapoharibu heshima ya degree hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo yote naomba vilevile kwa Mawaziri ambao tunaendelea na migogoro mingi hapa, kwa zile sheria ambazo Mawaziri wanaziona kama zina matatizo, wazilete tena sheria hizo Bungeni zifanyiwe marekebisho kama Mheshimiwa Rais anavyofanya. Mheshimiwa Rais juzi alifanya mabadiliko akaleta Sheria ya Madini, amesema iletwe Sheria ya Mafuta ifanyiwe mabadiliko, Mheshimiwa Luhaga Mpina na Mawaziri wengine ambao wanaona kuna matatizo, leteni sheria hizo hapa zifanyiwe mabadiliko ili kuondoa ugomvi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.