Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Wapo wazungumzaji wamenitangulia wamechukua baadhi ya hoja zangu, lakini naweza nikaongezea kidogo. Nianzie pale alipoishia mzee wangu, Mheshimiwa Bulembo.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Bunge, Wabunge walio wengi ni Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, pia Serikali inayoongoza ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Wakati wa utengenezaji wa bajeti viko vitu vinaangaliwa, inaangaliwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, inaangaliwa hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge lako, lakini pia unaangaliwa Mpango wa Miaka Mitano wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, jana nimeangalia kwa makini sana, nimeipitia kwa mara ya kwanza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nimeona kumbe ilani imeandika vizuri sana juu ya uendelezaji wa sekta ya uvuvi na mifugo. Jana hiyo hiyo nikapitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, lakini pia nikasikiliza na clip ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge lako mwezi Novemba, 2015.

Mheshimiwa Spika, yaliyoandikwa kwenye Ilani ya CCM, yaliyoandikwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na aliyoyasema Mheshimiwa Rais, hayajatekelezwa yote kwenye sekta ya uvuvi na mifugo. Hayajatekelezwa! Bajeti imepata asilimia sifuri ya maendeleo kwa mwaka 2017 au mwaka huu tulionao, 2018. Maana yake ni kwamba sekta ya uvuvi na sekta ya mifugo ndiyo basi tena, imekwenda kuzimu. Waswahili wanasema imekwenda kuzimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna ukanda wa bahari wa kilometa1,400 kuanzia Mtwara mpaka unafika Tanga. Kwa maajabu makubwa kabisa, ni Tanzania pekee ambako wavuvi ndio maskini. Katika maeneo nchi tulizopakana nazo, ukienda katika visiwa vya Mauritius, ukienda Seychelles na maeneo mengine, Zanzibar tu inawezekana huu umaskini wa Zanzibar labda tumewaambukiza sisi. Hata maeneo ya Comoro, wale wavuvi sio masikini kama wavuvi wa Tanzania. Leo wavuvi wa Tanzania ndio wamekuwa na laana ya kuwa maskini jambo ambalo kwa kweli linasababishwa na usimamizi mbovu na sera mbovu za chama kinachoongoza, lazima tuseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nimekutana na wavuvi kutoka upande wa Kanda wa Ziwa, wana malalamiko makubwa. Wanalalamika kwamba sasa hivi wamezuiwa kabisa kuvua. Hoja iliyoletwa mezani kwako ya kuunda Tume, naomba sana uiunge mkono. Kuna haja ya kubwa sana ya kuchunguza. Najua umeunda Tume ya Kuchunguza Uvuvi. Kuna haja kubwa sana ya kuangalia operesheni inayofanywa kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maftaha amezungumzia hapa kwamba kule Mtwara kuna kijana amepigwa risasi. Kwa bahati mbaya yule kijana mimi namfahamu, amepigwa risasi ya kisogoni na hawa watu ambao wanasema wanapambana na uvuvi haramu. Nataka nikuhakikishie uvuvi wa mabomu haupo Mtwara, haupo Lindi, sasa hivi watu wameacha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani tulikuwa hatupati samaki, nami niliwaambia, nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Nilimwambia Mheshimiwa Mpina, kama kuna jambo mlitusaidia na wananchi wameelewa, wameacha kupiga mabomu, niliwaambia kwenye Kamati. Wakati fulani nilimwambia Mheshimiwa Ulega alikuwa Mjumbe mwenzetu wa Kamati. Nilisema operation hizi za kwenda kupambana na uvuvi haramu, msipokuwa makini, mnakwenda kuua Watanzania wasiokuwa na hatia. Leo yametokea, watu wamepigwa risasi. Leo pale Jimboni kwangu Mchinga, vijana wa maeneo ya Ruvu, Mchinga na Kijiweni hawana shughuli nyingine zaidi ya uvuvi. Wakienda wanakutana na askari, wanawatisha, watu wanaacha uvuvi wanarudi. Tunawaongezea umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kwenda kuchunguza kilichoendelea kwenye operation hii inayoitwa tokomeza ni jambo muhimu na isifanyike kwenye ukanda wa ziwa tu, ufanyike pia maeneo ya Mtwara, maeneo ya Lindi na maeneo ya Kilwa kwa sababu pia watu wamedhurika kwa kiwango kikubwa sana na hii operesheni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ufugaji, sisi watu wa Mkoa wa Lindi na Wilaya tatu siyo Wilaya zote. Mkoa wa Lindi kwenye maeneo mengine walikataa kupokea mifugo wakati wanahamishwa kutoka Ihefu, lakini Wilaya ya Lindi ambako mimi ndiko ninakotoka, Wilaya ya Kilwa na Liwale tulikubali. Tulikubali kwa sababu maeneo ya kuwaweka wafugaji tunayo. Kwa bahati mbaya walipoletwa ni kama tu tumewa-damp, hawajaendelezwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante.