Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imebarikiwa sana kuwa na maeneo mazuri yenye uwezo wa kuifanya mifugo ikaneemeka na maziwa makubwa na bahari yenye uwezo wa kutuletea samaki wa kutosha. Baraka hizi zisipotumika vizuri hazitofautiani na mwanafunzi mwenye akili darasani halafu hana jitihada, mwisho wa siku lazima atafeli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 36 ya familia za Kitanzania zinajihusisha na ufugaji. Nchi yetu ni nchi ya pili Barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe, inazidiwa na Ethiopia tu. Nchi yetu kwa sasa ina ng’ombe zaidi ya milioni 30. Takwimu zinatuonyesha kila mwaka kwa wastani wanaongezeka ng’ombe milioni moja. Kwa hiyo, ng’ombe milioni 30 ni fursa. Naiomba Wizara isitazame mifugo na uvuvi kama tatizo na kinachotupatia shida ni kuitazama kama tatizo, tunajinyima fursa ya kuitazama kama fursa na kuifanya ikaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwa utaratibu ukachanganua, kama nchi yetu ina ng’ombe milioni 30, tuchukulie ng’ombe wanaoweza wakauzika, yaani tukafanya strategic farming tunavuna ng’ombe kimkakati, tuwavune kimkakati ng’ombe milioni tano kwa mwaka, tafsiri yake, tutapata shilingi bilioni tano. Ukipata shilingi bilioni tano ukaenda kwenye upande wa maziwa, kila ng’ombe walete lita moja moja, katika hii hesabu utakuwa na lita bilioni sita. Ukizidisha kwa lita moja kwa shilingi 1,000 kwa upande wa maziwa tu nchi yetu inao uwezo wa kupata trilioni1.8 kwa mwaka. Kwa upande wa kuuza ng’ombe hujagusa ngozi, hujagusa kitu chochote, unaweza ukapata trilioni 2.8 kwa mwaka. Kwa hiyo, sekta ya ng’ombe peke yake tukiitengenezea mkakati mzuri tunaweza kupata kwa mwaka trilioni nne.

Mheshimiwa Spika, tatizo ninaloliona, ni kwamba hatujatazama hii fursa na tukaangalia zile changamoto zake vizuri tukaziweka pembeni. Tukienda hivi tutafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, nina mfano mmoja. Kulikuwa na DC mmoja kama sikosei alikuwa wa Iramba, alipofika Iramba akatengeneza programu ya kuku mmoja, nyumba moja, familia za Iramba zikazalisha Kuku wa kienyeji wengi sana, ndani ya muda mfupi watu walijenga, mpaka kuku tunaokula hapa ni mchango wa Nawanda alipokuwa DC wa Iramba. Kwa nini tusifanye hivi kimkakati kwenye ng’ombe?

Mheshimiwa Spika, ng’ombe wengi siyo tatizo, uchache siyo tatizo; tatizo, tunawavuna vipi? Tukitengeneza utaratibu wa kuwavuna ng’ombe kimkakati, kila mwaka mnaondoa ng’ombe milioni tano, wanazaliwa milioni moja; automatic echo system itaji-set. Ni jinsi tu ya kupanga. Kupanga ni kuchagua, tukiacha kama inavyokwenda, hatutaweza. Ng’ombe watakuwa tatizo, kilimo kitakuwa tatizo na samaki watakuwa tatizo.

Mheshimiwa Waziri Mpina, hoja hapa ni ndogo tu. Mifugo kweli kuna maeneo ni matatizo. Kuna maeneo wanaingia kwenye hifadhi, kuna maeneo kule wanashambulia mahindi, kuna maeneo wanasababisha soil erosion, lakini lazima tutengeneze utaratibu. Mifugo imeshakuwa utamaduni. Kitu kikishakuwa utamaduni, jinsi ya kukiondoa lazima kitaleta resistance. Njia pekee ni kwenda nacho sambamba, automatic kitakuja kitapotea. Kama ng’ombe wanakulete trilioni nne kwa mwaka hakuna mtu ambaye ataacha kuuza ng’ombe wake, atauza tu kwa sababu wanamletea faida. Ni kutengeneza tu modality nzuri ya kuuza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni huu utaratibu wa kupiga chapa. Utaratibu wa kupiga chapa huu umepitwa na wakati. Sijui unamgonga ng’ombe kiunoni, anatoka na muhuri mkubwa, tunapoteza thamani ya ngozi. Wenzetu wana hereni (pin). Pin ina serial number anagongwa sikioni hapa anakuwa na data, anajua joshoni atakwenda lini, leo atapigwa sindano sijui ya kifaduro, yaani kila kitu, chanjo, wenzetu wanafanya hivi. Kumpiga ng’ombe muhuri, ngozi automatic inapoteza thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ijaribu kwenda kwenye teknolojia, tuweke serial number, anagongwa, inakwenda kwenye database ya Wizara, unajua kabisa ng’ombe “x” alipata chanjo siku fulani, data zinakuja. Hata ng’ombe aliyekufa unajua kabisa alitoka kwenye familia ya mtu fulani kwa sababu tayari tuna-database.

Mheshimiwa Spika, lingine, kama nilivyosema awali, zaidi ya asilimia 36 ya Watanzania wanajihusisha na ufugaji, ama mbuzi, au ng’ombe au kuku na kitu kingine chochote kile. Mazingira hutofautiana, kwa maeneo ya kwetu sisi kule Mbinga hatuwezi kuwa na ng’ombe tukawachunga, maeneo hayako. Lazima maeneo yetu sisi, twende kwenye mkakati sasa ninaousema ndugu yangu Keissy namuunga mkono kuhusu kufuga kisasa. Kwamba utafuga ng’ombe wachache, eneo dogo, tija kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo mengine ukienda kufuga ng’ombe wachache, eneo kubwa unapata hasara. Haya mambo lazima tuyaangalie. Hii Dunia haifanani, Tanzania siyo kisiwa, lazima tui-map hii nchi yetu kiufugaji. zone zile zenye ardhi ndogo, mfumo wa ufugaji lazima utakuwa tofauti.

Mheshimiwa Spika, mimi hapa nina hekari 2,000 zinanitazama mbele yangu, nina ng’ombe 300, nifuge ng’ombe wanne kwa ajili ya nini wakati ardhi ninayo? Tunatofautiana. Kuna maeneo lazima tubane, ardhi haitoshi, lakini kuna maeneo tunaweza tukafuga tu, haina tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, mifugo ina thamani kubwa sana na kuna muda nadhani tunakosea. Mimi ni mkulima wa mahindi, sisi wakulima wa mahindi adui yetu namba moja ni mfugo kwa sababu akiingia ng’ombe anamaliza.

Mheshimiwa Spika, kule kwenye familia zetu, mtu mwenye ng’ombe mmoja, mwenye mbuzi wawili, mwenye kuku ni biashara ambayo inatusaidia sana. Thamani ya ng’ombe mmoja inakuwa kubwa kuliko magunia 20 ya mahindi. Ukitaka sasa hivi kumpeleka mtoto shuleni, magunia 20 ya mahindi hayauziki, lakini ng’ombe mmoja, uchu wa nyama haujawahi kwisha, ng’ombe anauzika, mbuzi anauzika. Kwa nini tusiitazame hii kama fursa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja la mwisho niseme kidogo kwenye kusafirisha samaki. Mheshimiwa Mpina tusijisahau kuwajua Watanzania. Hulka ya Mtanzania akitoka kwenda kumtembelea jirani, kama ametoka shambani ana kawaida ya kubeba unga, akitoka ziwani ana kawaida ya kubeba dagaa na samaki ili anakokwenda asiende kumtia mzigo anayemtembelea. Mtu kabeba kwenye gari samaki wawili, anakwenda kumwona jirani yake, tatizo liko wapi? Sasa hivi kwenye mabasi huwezi ukabeba hata samaki wa mboga. Nikikaa hapa sasa hivi nikitaka samaki kutoka Mwanza, nitafute cooler box, nitaweza?

Mheshimiwa Spika, haya mambo hebu tuya- moderate, tuyaweke katika hali ambayo tunajua kabisa kusafirisha samaki wawili, dagaa ni utamaduni wa Mtanzania ili anakokwenda kule asiwe mzigo. Anatoka anakwenda Dar es Salaam, hakuna mboga; anabeba dagaa zake kutoka Mwanza au samaki wake watatu, unaweka kwenye basi, unamtoza mtu fine. Why? Kwa nini tunajisahau kuwa sisi hatujafika hiyo stage ya kuwa na cooler box na kuwa na yale malori yana-pack samaki yanasafirisha? Hata yakiwepo, yatakuwa mangapi? Watakula wangapi hao samaki watakaosafirishwa kwenye hayo magari? Tuwe wa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.