Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. John Tizeba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri. Nampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara zake nyingi zilizoleta tija kwa ajili ya kilimo chetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 75 ya wananchi wanaishi vijijini na asilimia 65 ni wakulima na wanategemea kilimo, lakini bado Serikali haijaweza kuwa na mkakati wa kumsaidia mkulima. Yapo mambo ambayo ningeomba kupata ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo ilianzishwa ili kuweza kumsaidia mkulima mtaji kwa sababu wakulima hawakopesheki. Pamoja na benki hii kuwa Dar es Salaam, bado Serikali haijaweza kuweka pesa ya kutosha kwa ajili ya kukopeshwa wakulima. Kwa ushauri wangu benki hii makao makuu yahamie Dodoma, lakini kuwepo na matawi kila kanda ili wananchi waweze kuwafikia kwa urahisi. Ushauri wangu ni kwamba Serikali iongeze mtaji katika benki hiyo ili ibebe jukumu la kutoa mikopo kwa wakulima wengi na yenye riba nafuu ili kilimo kiwe na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pesa ya utafiti 1% ya bajeti, ni lini Serikali itatenga pesa ya kutosha kwa ajili ya watafiti ili wataalam wetu waweze kufanya tafiti mbalimbali hasa za mbegu, mbolea hata waweze kupima udongo wa maeneo mbalimbali ili wakulima wetu walime kilimo chenye tija na cha uhakika kuliko sasa hivi ambapo mkulima analima kilimo cha kubahatisha, hana uhakika na kilimo chake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo huu unadhihirisha kukosekana kwa dhamira ya dhati ya uwekezaji katika miradi ya kilimo na kikwazo katika ukuaji wa kilimo na kupunguza umasikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani wanafanya kazi gani katika maeneo yao? Mbona wakulima wetu hawana elimu ya kutosha ya kilimo ya kueleweshwa kuhusu mbegu bora, utumiaji wa mbolea na matumizi ya ardhi kwa ujumla? Ni kwa nini yasianzishwe mashamba darasa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kuwapatia elimu wakulima wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alipofanya ziara Iringa alitueleza kuwa NSSF wameamua kufufua kinu cha kusaga mahindi cha Iringa (National Milling) kwa ajili ya kuleta tija kwa wakulima wetu wa Mkoa wa Iringa. Sasa je, huo mpango bado upo? Sababu kinu hiki kilikuwa kinaleta ajira, pia ni soko hata kwa wakulima wetu la mahindi. Wakulima nchini hasa wa Mkoa wa Iringa wanapata shida sana kwa sababu upatikanaji wa mbolea katika maeneo mbalimbali haukidhi mahitaji ya wakulima nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo changamoto nyingi sana zikiwemo za wasambazaji mbolea kwamba hawazingatii kabisa bei elekezi za Serikali na kusababisha bei ya mbolea kuwa kubwa sana, mbolea haifiki kwa wakati, hawazingatii msimu unaanza lini na kadhalika. Ni kwa nini Serikali isiangalie uwezekano wa kuondoa tozo katika mbolea ili bei ya mbolea ipungue?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali izingatie ushauri wa Kamati. Kamati imeshauri mambo mengi sana ambayo kama yakizingatiwa yanaweza kusaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania tumekuwa na kilimo cha kubahatisha na wakulima wengi wanategemea kilimo cha mvua na msimu wake hautabiriki, ni lini Serikali itaanzisha Bima ya Kilimo ili wakulima waweze kukopesheka kuliko ilivyo sasa mkulima hakopesheki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.