Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa hotuba nzuri aliyoitoa leo tarehe 3 Mei, 2016. Pia, nampongeza kwa kujituma, kuwajibika vizuri katika kusimamia Wizara yake. Hii inaonesha kuwa Mheshimiwa Rais hakukosea kumteua katika Wizara hiyo. Ni matumaini yangu kuwa kupitia Waziri huyu, nchi yetu itapata mapinduzi makubwa ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa ushauri mdogo kwenye upande wa kilimo, hususan pembejeo. Serikali yetu ya Awamu ya Nne iliweka utaratibu wa kuwasaidia wakulima wetu kwa kuwapatia pembejeo za ruzuku.
Pembejeo hizi zimekuwa hazimsaidii mkulima hasa wakulima wadogo. Wafanyabiashara na makampuni yamekuwa yakiingia mikataba na Serikali ili kuwasambazia wakulima pembejeo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makampuni yamekuwa yakiwapatia pembejeo hizo kupitia mawakala kwa mtindo wa vocha. Mawakala hawa wamekuwa wakijinufaisha kwa kuwalaghai baadhi ya wakulima kwa kuwaomba wasaini vocha hizo bila kuchukua mbolea au pembejeo hizo kwa kuwalipa fedha kati ya sh. 5,000/= mpaka sh. 10,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbolea hizi zimekuwa zikipelekwa kwa wakulima kiasi kidogo au kwa kuchelewa ili ziwakute wakulima wakiwa wamepanda na kuwashawishi wasaini vocha hizo. Kupitia tabia hizi za mawakala wasio waaminifu, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwasaidia wakulima kwa kulipia baadhi ya gharama za kilimo na pembejeo, lakini zimekuwa hazizai matunda. Naishauri Serikali ione au iweke utaratibu mwingine wa kuwasaidia wakulima kwa kulipia baadhi ya gharama za mbolea au pembejeo ili wakulima wawe huru kwenda kujinunulia mbolea hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niliwahi kushuhudia wakala mmoja akielezea jinsi gani alivyonufaika na usambazaji wa mbolea hizo. Ni vizuri Serikali ifanye utafiti wa kutosha juu ya matumizi ya mbolea za chumvi chumvi kwa baadhi ya maeneo. Mbolea nyingi zinazoenda Mkoa wa Morogoro zimekuwa zikipelekwa Mkoa wa Njombe. Wakulima wengi wa Morogoro wamekuwa wakipelekewa mbolea hizo na kutochukua kwa kupewa fedha kidogo na badala yake mbolea hizi zimekuwa zikipelekwa Mkoa wa Njombe ambako mahitaji ni makubwa. Wafanyabiashara wamekuwa wakiuza mbolea hizo kwenye maduka ya kawaida na kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiajiri vijana wengi wenye taaluma ya kilimo ili kuendelea kutoa mafunzo ya kilimo kwa wakulima wetu; Mafunzo ya matumizi mazuri ya mbolea, uchaguzi wa mbegu bora na mengineyo. Lengo ni kuongeza ujuzi wa kilimo bora kwa wakulima na kuongeza kiwango na ubora katika uzalishaji. Vijana hawa wamekuwa wakikaa tu maofisini bila kufanya kazi zao kama Maafisa wa Kilimo. Ni muhimu kwa Serikali kuweka utaratibu wa kuwafanya Maafisa hawa kuwajibika ipasavyo kwa maendeleo ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Kilimo ni lazima pale wanapofanyia kazi wahakikishe kwamba, wanakuwa na kajishamba darasa (demonstration farms). Ili kuhakikisha kwamba kumekuwa na uwajibikaji wa Maafisa Kilimo, ni lazima kuwe na utaratibu wa kuweka malengo mahususi ya uzalishaji katika eneo husika na Maafisa hawa wapimwe kwa ufanisi wa malengo hayo. Kwa kuweka malengo hayo, Maafisa Kilimo wataweka utaratibu wa kushinda shambani na wakulima ili kuhakikisha kwamba malengo ya wakulima yanafikiwa na malengo yake Afisa yanafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, natoa shukrani zangu za dhati kwa kupata fursa hii ya kuchangia. Nawasilisha.