Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kilimo Tanzania, leo ni miaka 57 baada ya uhuru bado Tanzania kilimo kimekuwa cha kusuasua na kimejaa siasa na misamiati kibao. Kwa kifupi bado nchi yetu haijawa serious na kilimo kwa kuwa bado wakulima asilimia 70 wanategemea jembe la mkono na asilimia tatu wanatumia wanyama kazi na asilimia tatu ndiyo wanaotumia zana za kisasa za kilimo kama matrekta na mitambo mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo chetu tumekiingiza kwenye siasa na misamiati ya maneno badala ya vitendo. Yapo maneno siasa ni kilimo, kilimo cha bega kwa bega, kilimo cha kufa na kupona, kilimo cha ushirika, kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu, kilimo ni uhai na kilimo kwanza. Je, nchi jirani wanayo hii misamiati katika kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kudharauliwa kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, pungufu asilimia 23. Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilipelekwa asilimia 18 na bila shaka itapungua hadi asilimia tatu, hii ni hatari, hatujui kipaumbele ni kipi na kipi kisubiri, kuna mambo namna tatu, moja umuhimu haraka sana, mbili muhimu lakini siyo haraka, tatu muhimu kawaida. Bajeti ya Kilimo ni asilimia 0.52 ya Bajeti Kuu, namtaka Waziri atakapokuja katika winding up atueleze vipaumbele katika Wizara yake. Bajeti haitoshi ni bado tunasema kilimo ni uti wa mgongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kizungumkuti cha mawakala, bajeti ya mwaka 2015/2016 ilikuwa shilingi 35 bilioni na deni wanalosema wanadai ni shilingi bilioni 67. Maswali ya kujiuliza Waziri uje na majibu ama shilingi halali yangu kuishika. Kwa nini shilingi bilioni 67 inatoka wapi?, kwa nini vocha zilizidi hata bajeti iliyotengwa ni vocha za thamani gani zilirudi kutoka Mikoa yote? Kwa nini zilitengenezwa vocha nyingi zaidi ya bajeti iliyotengwa, ni fedha shilingi ngapi zilitumika kutengeneza vocha hizo? Baada ya vocha kurudi deni halisi ni shilingi ngapi? Je, Serikali ipo tayari kuwasikiliza mawakala ili watoe hesabu halisi? Hakuna ofisi iliyovunjwa na vocha kuibiwa kwanini kuna tofauti ya deni ya shilingi bilioni 35 na shilingi bilioni 67? Waziri uje na majibu sahihi na uchunguzi ufanywe na Serikali ili kubaini waliohusika na hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya ushirika ni matatizo kwa wakulima. Zamani miaka ya 1950 – 1960 vyama vya ushirika kama KNCU - Kilimanjaro na KNCU - Kagera, Nyanza na Tanga - TARECU, vyama hivi viliwasaidia wakulima kwa kukata shilingi moja hadi mbili na kisha waliwalipia ada wanafunzi ambao leo ni madaktari, wachumi, maprofesa, engineers, pilots lakini pia bado vyama vya ushirika viliwasaidia wakulima katika kuendeleza kilimo, leo vyama vya ushirika kazi kubwa ni kuwaibia, kuwadhulumu na kuwatapeli wakulima mazao yao na bahati mbaya mnaihusisha Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha mbolea Tanga - Tanzania Fertilizer Company (TFC). Tanga ilikuwa ni mji wa viwanda, miongoni mwao ilikuwa ni Kiwanda cha Mbolea. Kiwanda kilifanyiwa hujuma na kikafa kwa maksudi ili pafanyike biashara ya kuagiza mbolea kama urea, sulphur/DAP bei juu, kisha eti kikajengwa Minjingu lakini vifungashio made in Kenya. Wakati Kiwanda cha Mbolea Tanga kinafanya kazi hakijauliwa kwa makusudi tatizo la mbolea halikuwepo na wala issue ya mbolea ilikuwa haijadiliwi Bungeni kwa ghadhabu na hasira kama ilivyo leo. Tujiulize tatizo nini na liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kwa jina la Mwenyezi Mungu bila ya kuimarisha na kuboresha kilimo kinachotoa raw materials za viwanda tutabaki na hadithi za paukwa pakawa hapo zamani za kale, bajeti ya kilimo ni asilimia 18 kwa mwaka 2018, nashauri Serikali iongeze bajeti kwa mwaka 2018/2019 angalau ifikie asilimia 35 kwa kuwa kilimo kinaajiri Watanzania asilimia 75 angalau kilimo kitaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wakulima kukosa masoko; Tanga ni wazalishaji wakubwa wa zao la muhogo katika Kata za Kirare, Mzizima, Tongoni, Pongwe na Kiomoni lakini tatizo kubwa ni soko la uhakika kiasi kikubwa cha muhogo hutegemea soko la Tanga Mjini na Dar es Salaam. Masoko hayatoshelezi na kusababisha muhogo kuporomoka bei, zimekuwepo tetesi kuwa Wachina wanahitaji muhogo, Tanzania Chamber of Commerce iko katika mazungumzo ili kujua kwa mwaka China itahitaji tani ngapi kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, Waziri wa Kilimo wakati wa majibu ni vyema akaeleza ukweli na uthibitisho wa taarifa hii ili kuweza kuwatoa shaka wakulima wa muhogo wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Masoko ya mazao mengi yamekuwa mashakani na mazao hayo ni mbaazi, mtama, miwa, machungwa, mahindi, ufuta na kadhalika. Serikali iwe na mipango ya muda mrefu ya utafutaji wa masoko, Serikali ifuate mfano wa nchi za India, Brazil, Rwanda, Burundi na Uganda kutafuta masoko ya mazao ya wakulima wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo kwa wakulima katika mabenki; mikopo katika mabenki ya nchi yetu ni haki kwa kila Mtanzania atakayekamilisha taratibu zilizopo. Serikali ilianzisha hatimiliki za kimila na moja ya manufaa ya hati hizi ni wakulima kuweza kuzitumia katika mabenki na kuweza kupata mikopo, kitu cha kushangaza wananchi wengi waliotaka kuzitumia hatimiliki za kimila kutaka mikopo katika benki za NMB, NBC na CRDB. Hati hizi hazitambuliki na wakulima wanashindwa kuelewa kati ya mabenki na Serikali nani ni mkweli au nani ni muongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kwa Serikali, isiwadanganye wakulima inawakatisha tamaa, wakulima wamejitahidi kupata hatimiliki za kimila lakini hazina maana yoyote. Serikali itafute njia mbadala kuwawezesha wakulima wa Tanzania kuweza kupata mikopo katika mabenki yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha Mkonge Tanga. Tanga imefahamika na kupata umaarufu katika Afrika Mashariki, Afrika na dunia kutokana na zao la mkonge kuanzia katika miaka 1886, zao hili lililetwa na Wagiriki na Wajerumani, Serikali ya United Kingdom, walikuja kuliboresha na kuliimarisha kwa kuwa walipata kodi kubwa katika mkonge. Mkonge katika Tanzania upo katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Lindi. Mkoa wa Tanga pekee ulikuwa na mashamba 72 yaliyoajiri wafanyakazi 40,000 na vibarua 32,000. Serikali baada ya kuimarisha mashamba ya mkonge iliamua kuzibinafsisha Mamlaka ya Mkonge (Tanzania Sisal Authority) na hapo ndipo mkonge ulipoanza kufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati njema sana dunia imeamua kutumia bidhaa za mikonge kwa kuwa mkonge hauchafui mazingira, lakini mkonge katika Tanzania haupo mikononi mwa Serikali, mamlaka na udhibiti ipo kwenye taasisi na watu binafsi ambao hawawezi kuendesha mkonge. Nashauri Serikali iamue kwa makusudi kulifanyia kazi na kulithamini zao la mkonge kama inavyofanya kwa mazao ya korosho na pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho Maafisa Ugani wasikae ofisini waende mashambani.