Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu na pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Wanging’ombe kwa kufiwa na watu mashuhuri, makada wa Chama cha Mapinduzi. Tumefiwa na Diwani na Katibu Kata wa Kata ya Igima. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu hawa mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu. Waziri na Katibu Mkuu wote ni ma-engineer, nategemea kabisa ma-engineer hawatatuangusha katika kulifikisha Taifa hili kwenye uchumi wa kati. Tutafanikiwa kufikia uchumi wa kati kama Wizara hii imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba hii, kwa kweli sijaridhika nayo. Kwa jinsi sekta hii ilivyo kubwa lakini hoja iliyoletwa ni kidogo sana na mambo mengi ya msingi yameachwa. Tukumbuke tulio wengi hapa ni watoto wa wakulima na kama Wabunge wote tulioko humu hatujawazungumzia wakulima inavyotakiwa kuhusu matatizo wanayopata kuanzia kupanda mbegu, hawana mbegu bora na hawapati kwa wakati; ukija kwenye kukuza mmea hawapati huduma ya ugani na viuatilifu; ukija kwenye soko ndiyo kabisa. Kwa hiyo, unakuta maeneo yote haya ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia mazao ambayo Mheshimiwa Waziri amewasilisha hapa, sijaona mkakati wowote wa kusaidia wakulima wa mahindi na kuna mikoa karibu kumi inayolima mahindi. Kama alivyosema mwenzangu aliyetangulia kwamba sasa hivi hatusemi mambo ya subsistence farming, yaani kilimo cha mahindi siyo kwa chakula tu, ni pamoja na biashara. Tunategemea Serikali imuwezeshe mkulima wa mahindi ambaye hana zao lingine aweze kujikomboa kwenye uchumi. Kama kuanzia kulima hajasaidiwa, inapofika kuuza ndiyo Serikali inasema tunataka food security, unazuia asiuze mahindi yake, tutakuwa tumemsaidia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana NFRA iliweza kununua mahindi Mkoa wa Njombe lakini mwaka huu hawakuonekana kabisa. Wananchi wanauza debe moja Sh.2,000 mpaka Sh.3,000, kiasi ambacho hataweza kununua mbolea na kupeleka mtoto shule yaani maisha ni magumu kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Serikali hii ni ya wananchi lazima tuweke kipaumbele katika kuwasaidia wananchi hawa waweze kujikomboa na kuona faida ya kuwa na Serikali yao ambayo inasikia. Naamini kabisa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imesikia hili na najua tutafanya marekebisho. Mheshimiwa Waziri wakati atakapohitimisha bajeti yake alete kitu ili wakulima wa mahindi wampigie makofi. Mambo ya kuzuia mpakani watu wasiuze mahindi, hii haitusaidii, hatuwezi kutoka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua Waziri ni mkulima na mwaka jana nilimfuata kulima mtama, tumelima mtama pamoja nawe lakini mpaka leo hatujauza. Hapa nimeona kuna mkakati wa kuongeza zao la mtama, hivi tutalima mtama halafu iwe nini kama hatuwezi kuuza, magunia yamekaa yanaharibiwa na wadudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye eneo hili, pamoja na kwamba wewe ni rafiki yangu lakini tusifanye ngonjera, tunasema tunazalisha mtama kutoka tani 2,000 mpaka 3,000 halafu zitafanya kitu gani? Wanasema watahamasisha sekta binafsi waje wawekeze viwanda, lakini jambo hili ni long process, huwezi kulifanya katika msimu wa mwaka mmoja, kwa sababu watu tayari wamelima. Kwa hiyo, nafikiri tuwe na mkakati fulani ambao unamsaidia mkulima kuanzia ku-plan alime zao gani na asaidiwe vipi. Kama alivyosema mwenzangu pale, mnaleta mikorosho Dodoma inakauka, hivi kwa nini Serikali tusiwe na strategy kama tunawasaidia wakulima wa Mtwara na Lindi basi tungeweka nguvu yetu kule, huku kwingine tuweke nguvu kwenye mahindi, sehemu nyingine tuweke nguvu kwenye mpunga, nadhani kwa namna hiyo tutaweza kuwatoa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Wanging’ombe tunalima sana viazi na tunaanza kupanda Julai, mbolea inaanza kufika Oktoba wakati wameshamaliza kupanda, sasa mkulima umemsaidia hapo? Halafu tuna tatizo kubwa la ugonjwa wa ukungu wa viazi, kuna dawa ambazo zinaletwa kule hazijatatua tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hawa Maafisa Ugani wanafanya kazi gani? Sehemu nyingi nimeona Maafisa Ugani hawafiki kwa wakulima. Mimi ni mkulima lakini sijawahi kumuona Bwana Shamba anakuja kunitembelea kwenye shamba langu na nafanya hivyo kwa sababu nataka shamba langu liwe shamba darasa, wakulima waone Mbunge wao naye analima anavuna kiasi gani kwa heka, sasa huyu Afisa Ugani hafiki na mnaendelea kuwaajiri. Mimi nafikiri hawa watu kwa kweli kama ndiyo ufanyaji kazi wa namna hiyo, nimeona sehemu nyingi hawa Maafisa Ugani wanashughulika na mashamba yao, hawafiki kwa wakulima, kwa hiyo hatuwezi kutoka hapa tulipo. Tuna miaka zaidi ya 50 ya uhuru, tunataka tuone kilimo kinakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili Shirika la NFRA, nimeona kwenye kitabu kwamba mwaka huu mna mpango wa kuongeza ununuzi wa mahindi kutoka tani 18,000 mpaka tani 26,000, lakini hamjaonesha hivi mahindi yaliyopo nchini ni kiasi gani ili tuweze kupima ufanisi wa NFRA. Mimi nachojua ni kwamba bajeti mnayoweka ya ununuzi wa mahindi ni kidogo na ndiyo maana umeweka tani kidogo lakini umetuficha kujua hivi nchi nzima tunazalisha mahindi kiasi gani, ndiyo tungejua ufanisi wa mpango wa hii NFRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona kwamba kuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa pareto. Kwa miaka ya 60 Mkoa wa Njombe tulikuwa tunaongoza kwa ulimaji wa pareto lakini wananchi wale wameacha kulima kwa sababu hakuna soko. Sasa nani atalima pareto kama hakuna soko na hivi tutapataje foreign exchange kama hatulimi pareto? Pareto ni zao moja ambalo linaingiza sana mapato ya fedha za kigeni. Kwa hiyo, mngeonesha mkakati namna gani tutawahamasisha wananchi warudi kulima pareto ili tuweze kuongeza pato la nchi. Kwenye kitabu hiki ambacho nimesema hakina maelezo ya kutosha, hakielezei kabisa mkakati wowote wa kukuza mazao haya ili tuweze kuongeza uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wetu wa Njombe wenyewe tunajiongeza, tunalima kilimo cha parachichi.

Parachichi imeonekana ni zao moja ambalo kwa kweli soko linakuja, watu wanatoka Kenya nakuja kununua parachichi. Kwa hiyo, tunaomba Wizara iji-zero in kwenye zao hili la parachichi, mtusaidie masuala ya viuatilifu na namna ya kusindika zao hili. Naamini Mikoa ya Njombe na Mbeya itatusaidia kutoka hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda tunaweza tukafanikiwa tu kama utakuwa-based zaidi na mazao ya wakulima. Kama tunajenga viwanda vile ambavyo vitakuwa vina-process mazao ya wakulima, nina uhakika kwamba hata soko litajiongeza. Kama hatujaweka mkakati wa kuwasaidia wakulima katika mazao ambayo ni specific, yana watu ambao wanawekeza kwenye viwanda, ndiyo tunaweza tukawasaidia. Kwa hiyo, naomba utakapokuwa unahitimisha hoja yako ulizungumzie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masuala ya kukuza kilimo, hatuwezi kuendelea kukuza kilimo kwa kutegemea hili jembe la mkono. Ni lazima tuanze na mashamba makubwa (commercial farming). Sijaona katika kitabu hiki akiongelea kwa ufanisi commercial farming, hatuwezi kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.