Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na utukufu ambaye amenijalia uzima hatimaye niweze kusimama hapa kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya. Pia nimpongeze Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu pamoja na Waziri wa Wizara ya Kilimo, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, nimpongeze sana Waziri Mkuu namna ambavyo amekuwa akifanya kazi nchi nzima. Kimsingi hamna asiyejua namna anavyotimka kufuatilia sekta ya kilimo na kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanatendewa haki katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi kuishukuru sana Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo wametutengea ujenzi wa ghala kubwa katika Mkoa wa Ruvuma. Pale Songea Mjini kunaenda kujengwa ghala kubwa ambalo lina uwezo wa kuchukua tani 81,000 za mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili la ujenzi wa ghala kubwa liende sambamba na hoja kubwa ambayo nimekuwa nikiisema mara nyingi hapa inayohusu pembejeo za kilimo. Kwa Serikali yangu kuona umuhimu wa kujenga ghala kubwa katika Mkoa wa Ruvuma ina maana inatambua wazi namna gani Mkoa wa Ruvuma umekuwa ukizalisha mazao ya mahindi kwa wingi. Katika Tanzania hili ni ghala ambalo linaongoza, hakuna ghala lenye kuchukua tani nyingi kiasi hicho. Kwa hiyo, ujenzi huu wa ghala uende sambamba na suala la pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kwenye suala la pembejeo za kilimo iongezwe ruzuku hapa kwenye mbolea. Nashauri mbolea ya ujazo wa kilo 50 ikiongezewa ruzuku iende ikauzwe Sh.10,000 kwa kila mfuko. Hii itawasaidia sana wakulima lakini pia itaongeza tija ya uzalishaji katika eneo hili kwa sababu kupeleka tu ghala haitoshi, ni lazima kuwe na mkakati mzuri ambao utapelekea uzalishaji wa haya mahindi kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nadhani ni vizuri Wizara ya Kilimo pia ikafanya jitihada za makusudi za kupeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wetu wa Ruvuma ili wananchi wale waweze kukopa na kuongeza tija kwenye mazao yao kwa maana ya kuongeza mtaji. Nimekuwa nikiuliza hili swali mara nyingi ni lini Benki ya Kilimo itapelekwa katika Mkoa wa Ruvuma lakini majibu yake hayana afya, najibiwa juu-juu tu, ni majibu ambayo hayakidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kulikuwa na umuhimu sana wa kupeleka hii Benki ya Kilimo tofauti na sasa hivi Benki ya Kilimo imewekwa pale Dar es Salaam, kuna mashamba gani pale Dar es Salaam? Watu wamekaa kwenye viyoyozi, wapo maofisini wakitoka wanaingia kwenye magari wanaenda nyumbani, kwa hiyo, haileti tija kuweka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Peleka Benki ya Kilimo katika Nyanda za Juu Kusini ili wakulima wale waweze kuzalisha mazao kwa wingi kwa sababu ni wakulima haswa wanaofanya kazi za kilimo zinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye suala la masoko. Nimesoma kitabu hiki cha hotuba ya Waziri wa Kilimo, nimekwenda ukurasa wa 75, nilichokiona wanazungumzia kuzalisha katika kilimo lakini pia amezungumzia suala la uhifadhi sijaona akizungumzia suala la masoko ya mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona kama Nyanda za Juu Kusini tumetengwa kwa maana ya kwamba suala la mahindi halijawekewa mkakati madhubuti ambao utamnyanyua mkulima wa Tanzania ambaye kimsingi amekuwa akizalisha kwa kutumia nguvu nyingi lakini uzalishaji wake hauna tija. Hivi sasa ni mpaka mtu auze madebe matatu ya mahindi ndiyo apate kilo moja ya sukari, ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niombe Wizara ya Kilimo ije na mkakati mzuri. Siku moja Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea katika Mkoa wetu wa Ruvuma, alizungumzia suala hili la kuongeza thamani kwenye zao la mahindi. Akasema kwamba ataangalia namna ya Serikali kuweka mkakati ambao utafanya zao hili la mahindi kuuzwa katika mtindo wa minada kama ilivyo korosho na mazao mengine ambayo kimsingi yamekuwa yakileta tija kwa wananchi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, anafanya kazi vizuri pamoja na wasaidizi wake hasa huyo anayeongea naye hapo, wanafanya kazi vizuri sana, hebu jaribuni kuona namna ya kuongeza thamani ya zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, sasa naomba niende kwa mawakala wa pembejeo za kilimo. Rais wetu anafanya kazi nzuri na amekuwa akisema kwamba yeye ni Rais wa wanyonge na wasaidizi wake wamekuwa wakisimamia hivyo. Mimi nashangaa sana inakuwaje mawakala hawa wa pembejeo wana miaka minne wanadai pesa zao walizohudumia Serikali katika sekta hii ya kilimo? Mawakala hawa walikwenda kukopa fedha kwenye taasisi za fedha, wakajikusuru na wakaenda kuwekeza kwenye pembejeo za kilimo lakini Serikali haioni umuhimu wa kuwalipa, inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijificha kwenye kichaka cha uhakiki miaka minne. Ni kwa nini Serikali haiendi kuwalipa hawa mawakala wa pembejeo? Wapo mawakala ambao wengine walichukua mbolea TFC inaeleweka walikwenda kuchukua kule walichukua kiasi gani lakini wengine wanapoteza maisha yao wakisubiri kupata haki yao, Wizara mmekaa lakini Serikali pia imejificha nyuma ya suala la uhakiki. Ni uhakiki wa aina gani miaka minne, inatia huzuni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia wakala mmoja nilipokwenda ziara kule analia. Nimekuta pale dukani kwake kuna makampuni manne yote yanamdai na kila kampuni imeleta dalali, inasikitisha na yule bwana ametoka pale. Nitoe tu mfano kwa mawakala wachache ambao mnaweza mkafuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dada anaitwa Rose Minjingu, nendeni mkafuatilie pale, amekopa na taasisi zinamdai lakini pia kule alikokopa kwenye kampuni mbalimbali mpaka TFC anadaiwa. Imefika mahali amezungukwa na watu wale kama wanne wanadai, kila mmoja kaja na dalali. Pia yupo kijana anaitwa Cosmas Haule, naye pia amezingirwa, imefika mahali ndugu zake wamekaa chini kumshawishi maana alikuwa anataka kuchukua hatua ya kujinyonga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi hii ambayo watu wanatafuta haki zao na inafika mahali wanashindwa kupata haki zao, hivi kwa nini kama hawa watu kweli wameiba wasipelekwe Mahakamani? Haki zao zinapotea, wengine wanapoteza maisha, inatia uchungu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi hii wako watu ambao haki zao zinapotea, tunakwenda wapi? Wale mawakala walipwe pesa zao, wale ambao wamefanya vizuri walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyuma yake kunakuwa na suala la uhakiki, uhakiki gani? Mbona tumeona hawa watumishi wamehakikiwa siku mbili suala limekwenda, wenye vyeti feki wamehakikiwa siku mbili wamekwenda, ni kwa nini huku kwenye Wizara ya Kilimo hawalipwi pesa zao hawa mawakala? Siyo vizuri, msiwadhulumu haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kwa uchungu kwa sababu yuko mtu ambaye alikuwa anataka kujinyonga lakini ndugu zake wamekaa wamemshawishi, inatia huzuni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wale mawakala, wako mawakala saba ambao tayari wameshapoteza maisha, wako Wabunge ambao ni mashahidi hapa kwenye maeneo yao. Mzee wa Makambako yule pale atasema, kuna watu wamekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.