Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ambalo napenda nimuachie Waziri pamoja na Wizara yake waje watuambie nchi yenye fursa kama Tanzania ambayo tunaweza tukuwa tunauza chakula nje ya nchi kwa nini bado tunaagiza chakula kutoka nje? Baada ya hapo naanza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 19 ameelezea vipaumbele nane ambavyo Wizara yake imekuwa ikifanya utekelezaji wa haya majukumu. Cha kwanza sikigusi, nagusa cha pili kwamba kuongeza kilimo chenye tija kwa kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo kwa upande wa kilimo katika nchi yetu ya Tanzania bado ni hafifu sana. Niwapongeze kwa maamuzi ya ununuzi wa mbolea kwa pamoja (bulk procurement) lakini changamoto kubwa kwenye suala hili ni kufikisha mbolea kwa wakulima wetu kwa wakati kulingana na eneo husika na msimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Oktoba Mkoa wetu wa Katavi tunaanza kazi za kilimo. Watu wa tumbaku wanaanza kufulia mbegu Julai kuelekea wa Agosti, ikinyesha tu mvua ya kwanza Oktoba wanaanza kupanda. Mazao yote ambayo tunalima ndani ya Mkoa wa Katavi tukianzia tumbaku, mahindi na mpunga utaratibu ni huo. Sasa kama mbolea ya kupandia inachelewa na kilimo chetu tunaenda kwa kudra za Mwenyezi Mungu kwa kutegemea mvua matokeo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Wizara kwenye semina walieleza kwamba wamefanya saving nafikiri zaidi ya shilingi bilioni 9 kwenye ununuzi wa mbolea kwa pamoja (bulk procurement). Huku kwenye ununuzi wa mbolea kama Wizara mlifanya saving lakini wakulima wamepata hasara kwa sababu mbolea ilichelewa, by the time wanaweka ile mbolea mvua ikaondoka, wiki mbili hakuna mvua, kwa hiyo mazao yalidumaa, hawajaweza kuvuna ipasavyo. Mbolea waliyoweka haikuyeyuka kuingia ardhini kwa sababu mvua haikuwepo, tatizo mlichelewesha mbolea. Tuombe Wizara siyo mpaka Mkuu wa nchi aseme ndipo sasa na nyie mkimbizane mpaka na magari ya jeshi kufikisha mbolea kwa wakulima ambao sasa wanapata hasara, hili ni eneo ambalo linaajiri asilimia 70 ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zana za kilimo, tumeona kuna mifuko ya ukopeshaji lakini pia juhudi hii inabidi iongezwe. Iliwahi kutolewa kauli hapa na Serikali kwamba jembe la mkono litaenda kukaa makumbusho, sasa utekelezaji wa kauli hii umefikia wapi? Kwa hiyo, tutaomba Waziri utuambie kwenye zana za kilimo ni lini jembe la mkono litaondoka na tuingie kwenye zana ambazo tutafanya kilimo chenye tija na kuzalisha zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la viuatilifu na wadudu. Tunajua mna changamoto kubwa katika eneo hili lakini maandalizi ya kukabiliana na hawa wadudu yasiwe ya zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mbegu sasa hivi zinawachanganya wakulima wetu. Kuna nyingine zina ubora mzuri na nyingine hazina. Ukishavuna mazao yakikauka bado yanawahi kubunguliwa tofauti na zile mbegu za zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye upande wa zao la tumbaku. Makampuni ya tumbaku yamekuwa kama ndiyo wenye maamuzi katika nchi hii. Walishusha kutoka tani 60,000 mpaka tani 55,000 na bahati mbaya uzalishaji ukazidi kiwango na wakulima wetu walihangaika na bei mpaka mbolea zililowa na maji na matokeo yake waliuza mpaka Dola 0.6 kwa kilo kwa sababu ubora umeshashuka, tumbaku zilikaa muda mrefu. Tuombe Serikali watengeneze makubaliano ambayo yatakuwa yananufaisha wananchi hata kama kiwango cha uzalishaji kimezidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kwenye tumbaku kwa Wilaya yetu ya Mpanda kampuni ya TLTC imetoa barua ikisema inakusudia kusitisha ununuzi wa tumbaku kwa kisingizo kwamba go-down limejengwa ndani eneo la railway na ni kweli ni eneo la railway na wanatakiwa waliondoe na pili, ni masuala ya kiuongozi kutotimiza matakwa yanatotakiwa. Bodi ya Tumbaku inayo barua, huu wasiwasi wa wakulima wetu kwenye ununuzi wa tumbaku tutaomba kauli ya Waziri ni kweli TLTC mnakubali wasitishe ununuzi? Kama mnakubali ni kampuni gani mbadala itaenda kununua tumbaku katika Wilaya ya Mpanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana pia Waziri alikuja na mapendekezo ya kushusha produce cess kutoka 5% - 3% lakini haijamfaidisha mkulima kwenye haya mazao ya kibiashara kama tumbaku. Punguzo hili limeenda kutupunguzia mapato kwenye Halmashauri zetu na haijamgusa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri aje atuambie ni utafiti upi wa kina ambao wameufanya na kwa nini wasirudishe kwa upande wa wanunuzi kuwa 5% kwa sababu mkulima haijamfaidisha. Zile za leseni na kadhalika ambazo mliwapunguzia zibaki kama zilivyo lakini hii ya ununuzi wa haya mazao ya biashara kama tumbaku warudi kwenye 5%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Benki ya Maendeleo ya Wakulima. Chanzo cha CRDB kinafanana na hii TADB. CRDB ilivyoanzishwa ilikuwa kwa ajili ya kusaidia kilimo na vyama vya ushirika lakini imeenda imekuwa benki ya kibiashara. Kwa mfano, wakulima wa tumbaku wanakopa kutoka kwenye mabenki kwa riba ambayo ipo juu na kuanzishwa kwa benki hii ni chachu kwenye kutoa mikopo upande wa kilimo. Ni kwa kiwango gani mpaka sasa wameshatoa mikopo kwenye mazao ya aina mbalimbali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la SAGCOT. Nimeona kwenye hotuba wanataka waitanue pia ukanda mwingine lakini huu Ukanda wa Kusini SAGCOT imekamilika na kufanya kazi kwa kiasi gani? Hebu njooni Mkoa wa Katavi, ile mikoa ilikuwa ni big four sasa hivi ni big six kwa sababu imegawanyika Njombe na Iringa, Katavi na Rukwa. Kwa hiyo, SAGCOT ikamilishe kwanza Nyanda za Juu Kusini ndipo waende kwenye ukanda mwingine na tuweze kuongeza tija na uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kufanya utafiti. Baadhi ya Wabunge wamelalamika kwamba mazao yanaanzishwa sehemu zingine, kama korosho imeanzishwa nchi nzima, maeneo mengi wamechukua wamepanda na haijakua na pamba inatanuliwa maeneo mengine. Mwaka juzi tulipitisha sheria ya mambo ya utafiti na kwenye bajeti nimeona mmetenga shilingi bilioni 1.4, utekelezaji wa fedha hizi za kufanya utafiti uko kwa namna gani ili tunapotawanya haya mazao tuwe na uhakika kwamba yataenda kukua na kuongeza uzalishaji? Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha tutaomba majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Jimbo la Nsimbo tumeanzisha zao la pamba na tupo kwenye mikakati ya kwenda kulikuza. Kwa hiyo, tunaomba ile Bodi husika ipitie pia maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii Kampuni yetu ya Mbolea TFC. TFC ipo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lakini kazi kubwa za mbolea wanazofanya zinahusiana na Wizara ya Kilimo. Kwa nini Serikali kiutawala na kiutendaji, japokuwa ni kampuni, basi iwe chini ya Wizara ya Kilimo? Kama tunalaumu kwamba kuna upungufu kwenye utendaji basi anayehusika na usimamizi na usambazaji wa mbolea ambaye ni Wizara ya Kilimo aisimamie hii Kampuni ya Mbolea (TFC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kwenye kuwa nchi ya viwanda na mikakati iliyopo sasa hivi vile viwanda ambavyo tunaenda kuvilisha malighafi kwa kupitia shughuli zetu za kilimo, je, tunazi-link vipi hizi sekta zote ili tuwe na tija na kufanikisha malengo kwa wakati? Naomba Waziri atuambie katika mazao ya aina mbili tu, mafuta ya kula ambayo yamekuwa na mgogoro…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)