Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha hoja yangu. Nawashukuru wote waliochangia na kusema ukweli nimefarijika sana kwa sababu karibu wote waliochangia wameunga mkono juhudi zinazofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika ulinzi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipeke niwashukuru sana Wakuu wa Majeshi Wastaafu ambao wamejumuika nasi katika bajeti hii leo tokea asubuhi na mpaka sasa bado tuko nao. Nawashukuru sana kwa kazi nzuri waliyoifanyia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji waliochangia kwa maandishi walikuwa 30 na waliochangia kwa kuzungumza walikuwa 17. Hoja ni nyingi, makabrasha ninayo hapa ya majibu karibu yote lakini sina uhakika kama nitapata muda wa kujibu kila hoja iliyotolewa. Kama utaratibu wetu ulivyo, tutatayarisha majibu ya maandishi na kila Mbunge ataweza kupata majibu kwa kadri alivyouliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja za Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama. Wao walisema Serikali iongeze ukomo wa bajeti ya Wizara kulingana na mahitaji halisi. Ushauri umepokelewa, Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina ili ukomo wa bajeti uweze kuongezwa na kuiwezesha kukidhi mahitaji halisi ya fedha kwa Mafungu yote matatu yaani Fungu 38, 39 na 57. Namshukuru Waziri wa Fedha kama alivyozungumza siyo kwamba ombi liwe kusiwe na ukomo, hapana, bali ukomo uongezwe ili uweze kukidhi mahitaji ambayo ni ya lazima kwa jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilisema Serikali itoe fedha zote za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hususani kwa Fungu 38 lililopokea asilimia 41.25 ya bajeti iliyotengwa. Ufafanuzi ni kwamba hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 Fungu 38-Ngome limepokea fedha kutoka Hazina kiasi cha asilimia 84.9 ya fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na hivyo Wizara ina imani kuwa Serikali itakamilisha kutoa fedha zilizobaki kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa kuna hoja kwamba Suma JKT katika kupunguza tatizo la madeni lijikite kwenye kazi zenye zabuni badala ya kufanya kazi ambazo hazina zabuni na hivyo kupata matatizo katika kulipwa. SuUMAJKT kama zilivyo taasisi nyingine za kibiashara, limekuwa likijikita pia katika kazi zenye zabuni ingawa changamoto kubwa imekuwa ni madeni makubwa hususani kwa taasisi za Serikali. Shirika linatumia mikakati mbalimbali katika kudai madeni kama ifuatavyo:-

(i) Kuwatembelea wateja na kuwakumbusha kulipa madeni yao;

(ii) Kuwaandikia barua wakopaji na wadaiwa na wadhamini kulipa madeni yao;

(iii) Kuwatumia mawakala kudai madeni;

(iv) Shirika limewasilisha orodha ya watumishi wa umma wanaodaiwa madeni kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali ili wakatwe kwenye mishahara na pensheni zao;

(v) SUMAJKT limewasilisha orodha ya wadeni wanaodaiwa ili Maafisa Masuuli wawakate kwenye mishahara yao; na

(vi) Kutangaza kwenye vyombo vya habari na kuwafikisha katika vyombo vya sheria mawakala wasio waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hatua hizi, tunadhani kwamba tutaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza madeni ambayo Suma JKT inaidai taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa kuna hoja kwamba Serikali ihakikishe wadaiwa sugu waliokopa matrekta kutoka Suma JKT wanarejesha madeni ya mikopo hiyo inayofikia shilingi bilioni 40. Suma JKT katika kuhakikisha wateja wanalipa madeni yao ya matrekta wamechukua hatua zifuatazo:-

(i) Kuwajulisha wakopaji kulipa madeni yao kwa kuwatembelea;

(ii) Kuwaandikia barua na kutumia vyombo vya habari;

(iii) Kutumia mawakala wa kudai madeni;

(iv) Kuondoa walinzi kwa wadaiwa sugu na kunyang’anya matrekta yaliyo katika hali nzuri kutoka kwa wadaiwa sugu; na


(v) Inaposhindikana wakopaji kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hili tatizo la madeni ya matrekta limekuwa sugu, fedha ni nyingi lakini kila hatua itachukuliwa ili wanaodaiwa waweze kulipa madeni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi ya walinzi SUMA Guard kwamba yaboreshwe, kampuni ya ulinzi binafsi ya SUMAJKT Guard imezingatia viwango vya mishahara ya makampuni ya binafsi ya ulinzi wa ndani. Aidha, inalipa mishahara na marupurupu kwa kiwango kilicho juu ya kima cha chini cha Serikali. Mishahara ya walinzi imepandishwa kwa asilimia 14 kutoka Sh.170,000/= hadi Sh.193,000/= kwa kima cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mishahara na marupurupu yameboreshwa kulingana na mazingira ya ngazi na cheo. Hivyo mishahara ya walinzi inaanzia Sh.193,000/= hadi Sh.622,000/=. Aidha, kampuni inakabiliwa na changamoto ya kutolipwa madeni na washitiri wao ambao wengi wao ni taasisi za Serikali hivyo kukwamisha juhudi za kuboresha maslahi kwa watendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni Serikali itoe fedha shilingi bilioni mbili za maendeleo ambazo hazijatolewa kuwezesha ukarabati wa miundombinu ya kambi za JKT na ujenzi wa kambi mpya ili JKT iweze kuchukua vijana wengi wa mujibu wa sheria kwa mwaka 2018/2019. JKT kwa mwaka 2017/2018 ilitengewa jumla ya shilingi bilioni sita za maendeleo na hadi sasa Serikali imeshatoa shilingi bilioni tano za fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizo zimeleekezwa katika kukarabati na kujenga miundombinu iliyopo katika vikosi na makambi ya JKT kwa lengo la kuliongezea uwezo wa kuchukua vijana wengi kwa mujibu wa sheria na kujitolea. Aidha, JKT kupitia Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina ili kupatiwa kiasi cha shilingi bilioni moja iliyobaki kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha ili kukamilisha miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni Serikali itoe fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Mashirika ya Nyumbu na Mzinga. Ufafanuzi ni kwamba katika mwaka huu wa fedha Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya Mashirika ya Mzinga na Nyumbu, ambapo Shirika la Nyumbu limepokea shilingi bilioni 2.5 na Shirika la Mzinga limepokea shilingi bilioni 3.5. Tunatarajia kiasi kilichobaki kitapatikana kabla ya mwaka wa fedha kumalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine Serikali itoe fedha shilingi bilioni 19.8 kwa ajili ya kulipa fidia maeneo ambayo yametwaliwa na jeshi na kipaumbele kutolewa kwa eneo la Rasi Mshind, Kilwa. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewasiliana na Hazina na ahadi ya Hazina ni kutoa kipaumbele katika kulipa fidia ya eneo la Rasi Mshindo, Kilwa pamoja na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikamilishe mchakato wa Sera ya Ulinzi wa Taifa. Serikali imepokea ushauri huu na itaufanyia kazi haraka iwezekanavyo. Jambo hili ni kweli limechukua muda mrefu lakini kama taarifa ilivyotolewa hapa na Mheshimiwa Mbunge mmoja ni kwamba jambo hili limeshakaliwa katika ngazi moja ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na linasubiri hatua zilizobaki kufikia Baraza la Mapinduzi ili hatma ya jambo hili iweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipe stahili za Majenerali Wastaafu kama zilivyoidhinishwa. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Majenerali Wastaafu ni shilingi bilioni 3.9 mpaka sasa Wizara imeshapokea kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kama Waziri wa Fedha alivyoeleza. Ni matumaini ya Wizara kuwa Hazina itatoa kiasi kilichosalia itakapofika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ndizo zilikuwa hoja zilizotolewa na Kamati, nataka kuishukuru Kamati kwa kazi nzuri wanayofanya za kushirikiana nasi katika kuhakikisha kwamba bajeti yetu inapatikana ili tuweze kutimiza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa nitazungumza baadhi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanajeshi wastaafu kukatiwa bima ya afya. Wizara ya Ulinzi kwa kushirikiana na Serikali Kuu inaendelea kukamilisha taratibu stahiki za bima ya afya kwa wanajeshi wote wakiwemo wastaafu pamoja na familia zao. Mpaka sasa tunavyozungumza wanajeshi wanapata huduma za afya katika kambi zao. Kuna zahanati na vituo vya afya katika kambi mbalimbali, kuna hospitali kuu Lugalo na hospitali za kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kwa sababu za changamoto za kibajeti huduma si vile ambavyo tunataka iwe. Ndiyo maana sasa tumebuni kwamba pengine tuanzishe bima ya afya kwa wanajeshi, tupate pesa ya kutosha, tuboreshe huduma zetu katika vituo vyetu, lakini vilevile tuweze kuwasaidia waliostaafu. Kwa kweli watu waliolitumikia jeshi na nchi yao kwa miaka yote baada ya kustaafu kukosa huduma za afya si jambo la busara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba mfuko huu wa bima ukipita, tutakuwa na uwezo wa kutosha kabisa wa kuwahudumia wanajeshi walio kazini pamoja na wale waliostaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya maduka ya bidhaa kufungwa, wanajeshi wapewe exemption ili wapate unafuu katika bidhaa na vifaa mbalimbali. Yupo Mheshimiwa Mbunge nadhani ni Mheshimiwa Selasini alisema kwamba hakuna fidia yoyote iliyotolewa baada ya maduka haya kufungwa. Ukweli ni kama ufuatavyo Mheshimiwa Selasini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maduka ya duty free ya jeshi yalikuwa yana kasoro nyingi. Kasoro moja kubwa ilikuwa ni wale ambao walikuwa wakiyaendesha kuuza bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru nje ya makambi. Hiyo kama vile haitoshi, mimi nimefanya ziara katika kambi nyingi za jeshi, malalamiko makubwa yalikuwa maduka hayo pamoja na kupata exemption ya ushuru bado bei zao zilikuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imeamua kujipanga ili maduka haya ikiwezekana yaendeshwe na jeshi lenyewe ili tuondokane na kasoro hizo. Wakati huu tuliokuwa nao ambapo bado hatujatengeneza huo uwezo inatolewa fidia kwa kila mwanajeshi ya Sh.100,000/= kila mwezi, kwa hiyo, fidia hiyo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya usalama wa mipaka ya nchi, Tanzania na Kenya, Tanzania na Uganda, nadhani alikuwa Mheshimiwa Masoud anazungumzia juu ya uwekaji wa mipaka sawasawa. Nakupongeza sana Mheshimiwa Masoud umekuwa ukilifuatilia jambo hili miaka yote lakini nataka kusema kwamba sasa ufumbuzi umeanza kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizokuwa kwenye mipaka ya Tanzania na Kenya, nchi hizi zimekubaliana kuimarisha alama yaani beacon za mipaka kuanzia Ziwa Viktoria hadi Ziwa Natron na hatimaye kufikia Vanga katika Mkoa wa Tanga. Kazi hii imeanza rasmi tarehe 2 Machi, 2018 ambapo timu ya pamoja ya wataalam imeendelea na kazi kwa awamu ya kwanza kilometa 238. Kazi hii inahusisha pia kuweka beacon za kati ya kila mita 100 na hivyo kufanya mpaka uonekana kwa uwazi na kuondoa utata. Zoezi hili litakamilika kabla ya tarehe 30 Juni 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kuimarisha beacons za mpaka wa Tanzania na Uganda, nayo imeanza ambapo timu ya wataalam wako Mtukula wakiendelea na kazi. Kama ilivyo kwa mpaka wa Kenya beacons za ziada kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda zitaongezwa kwenye mstari wa mpaka ili uweze kuonekana kwa urahisi na uwazi. Kwa maana hiyo, kuna mafanikio katika kurudishia mipaka ya nchi zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine kwamba Wizara ya Ulinzi na JKT ihakikishe wanakuwa na usafiri wa kutosha kubeba maafisa na maaskari kwenda kazini na kurejea majumbani. Nadhani hii ilikuwa hoja ya Mheshimiwa Lubeleje, Wizara ya Ulinzi na JKT ina utaratibu wa kuwasafirisha maafisa na maaskari kwenda na kurudi kazini nchi nzima. Maafisa na askari hao hupanda magari hayo katika vituo maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baadhi ya maafisa na askari ambao hutoka mapema kazini kama wanaotoka zamu hukutwa njiani wakisubiri usafiri mwingine. Hata hivyo, juhudi zinafanywa kuongeza magari hayo ili kukidhi hitaji la usafiri kwa asilimia mia katika mikoa na wilaya zote zenye makambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilikuwa askari iliyepotea baada ya shambulio la tarehe 7 Desemba, 2017. Hii hoja nadhani ni ya Mheshimiwa Yussuf, Umoja wa Mataifa na Serikali kupitia JWTZ wanaendelea na juhudi za kumtafuta askari huyo. Endapo itatimia miezi sita bila askari huyo kupatikana kwa mujibu wa sheria za Tanzania Serikali kupitia JWTZ itaitisha Baraza la Uchunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tukio hili, tayari Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ameshaunda Baraza la Uchunguzi ili hatua stahiki zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kutoa tangazo la kifo yaani presumed death ili mchakato wa kuandaa taratibu za malipo ufanywe na Umoja wa Mataifa na JWTZ. Huyu kijana amepotea wakati wa shambulio na mpaka sasa hivi anatafutwa, hatuwezi kusema kwa uhakika kama yuko hai au ameshafariki, lakini taratibu ni kama nilivyozieleza hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupate utaratibu wa malipo ya stahiki kwa wanajeshi wanaofariki au kuumia wakiwa katika operesheni za ulinzi wa amani. Wanajeshi wanapoumia au kufariki wakati wakiwa katika majukumu ya ulinzi wa amani malipo yake yanatolewa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza hutolewa na Umoja wa Mataifa na sehemu ya pili hutolewa na Serikali yetu kwa kuzingatia kanuni za pensheni katika majeshi ya ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotolewa na Umoja wa Mataifa ni kwamba, mwanajeshi akiumia katika jukumu la ulinzi hulipwa baada ya kufanyiwa Bodi ya Tiba yaani Medical Board na hulipwa baada ya kujaziwa nyaraka muhimu. Malipo haya hufanyika kwa kuzingatia kiwango cha kuumia. Mwanajeshi akifariki Umoja wa Mataifa hutoa dola za Kimarekani 70,000 ikiwa ni rambirambi kwa familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Umoja wa Mataifa umetoa fedha zote kwa askari wetu waliofariki katika majukumu ya ulinzi wa amani na wote wamelipwa isipokuwa kwa wale ambao taratibu za mirathi bado hazijakamilika. Wizara inaomba kushauri kuwa familia ambazo hazijakamilisha taratibu za mirathi zikamilishe haraka iwezekanavyo ili wahusika walipwe fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanajeshi akifariki, Serikali hutoa fedha zifuatazo:-

Fedha za rambirambi ambazo hutolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ikiwa ni mshahara wa mwanajeshi wa miezi sita; kusafirisha familia na mizigo ya marehemu kwenda nyumbani na hutoa death gratuity pamoja na survivor pension. Kwa hiyo, katika suala hili hakuna utata hata kidogo, fedha hizi zinapatikana bila ya tatizo lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji mali. Jeshi lichukue hatua za kuimarisha tafiti kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia. Ushauri umepokelewa, hata hivyo, ili kuimarisha utafiti Serikali inaendelea na hatua za kuboresha utendaji wa mashirika ya Mzinga, Nyumbu na SUMA JKT kwa kuwapatia rasilimali watu, fedha na ukarabati wa miundombinu pamoja na vitendea kazi.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kutolipwa kwa madeni ya SUMAJKT yakiwemo madeni ya matrekta na SUMA Guard, hili nimeshalizungumizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SUMA JKT vifaa vyake vya ujenzi na ulinzi ni duni Serikali iwawezeshe. SUMAJKT imekuwa ikiendelea kujiimarisha kivifaa kadri ya mapato yake yanavyoruhusu. Kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, shirika limenunua mitambo nane mbalimbali ya ujenzi ili kukiwezesha kitengo chake cha ujenzi na kampuni ya ulinzi kufanya kazi kwa ufanisi. Aidha, kupitia kampuni yake ya ulinzi limenunua vifaa vifuatavyo:-

Gari la zimamoto na uokoaji kwa ajili ya shughuli za zimamoto; magari matano kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria katika malindo yake; mitambo ya kisasa ya CCTV Camera na kujenga control room. SUMA JKT Guard litaendelea kuboresha zana, mitambo na vifaa vya utendaji kadri mapato yake yatakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu operesheni za jeshi na mahusiano na mamlaka ya kiraia. Kulikuwa na hoja kwamba wanasiasa wasilitumie JWTZ kwa shughuli za kisiasa ndani ya nchi. JWTZ halijawahi kutumiwa kisiasa na wanasiasa. JWTZ linatumika kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nadhani Mheshimiwa Waitara kwamba jeshi lilitumika wakati wa uchaguzi Zanzibar. Hili nililijibu mwaka jana na naomba nilirudie, tutofautishe kati ya jeshi kutumika wakati wa uchaguzi na jeshi kulinda major installations wakati wa uchaguzi. Wakati wa uchaguzi kwa taarifa zenu Waheshimiwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinakuwa standby. Jeshi wakati mwingine linatumika katika kulinda major installation isitokee uhujumu. Zanzibar jeshi lilinda airport, bandari na maeneo ya kuzalisha umeme. Huko siyo kuingilia uchaguzi, kwa hiyo, jeshi halitumiki kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, JWTZ itoe msaada wa kiutendaji polisi. Jibu ni kwamba kulingana na mgawanyo majukumu ya ulinzi na usalama wa nchi yetu jukumu la usalama wa raia na mali zao ni jukumu la polisi. Hata hivyo, endapo kutatokea hitaji la kushirikisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama, JWTZ hutoa msaada huo kwa kuzingatia Sheria ya Ulinzi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhusiano huo mzuri, nchi yetu imeendelea kuwa salama. Tunachosema hapa ni kwamba jeshi lina jukumu la kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanapohitajika kufanya hivyo. Kwa hiyo, pale ambapo polisi wanahitaji msaada wa jeshi zipo taratibu za kufuata na jeshi huwa wanatoa msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matishio ya ugaidi. Kumekuwepo na viashiria vya ugaidi nchini Tanzania na hitajio la military intelligence kusaidia jeshi la polisi. Yapo matukio yenye viashiria vya ugaidi ambayo yamekuwa yakijitokeza nchini. Jeshi la Polisi limekuwa likikabiliana matukio hayo kwa mafanikio makubwa na kuweza kuyadhibiti. Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama vina utaratibu wa kubadilishana taarifa ya kiutambuzi kuhusiana na matishio mbalimbali ikiwemo ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo kikubwa cha Kupambana na Ugaidi (National Counterterrorism Center) kinachojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama kinakusanya taarifa za utambuzi kuhusiana na ugaidi na kuzifanyia kazi kwa pamoja. Matishio ya hivi sasa yanavifanya vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa ukaribu sana na kwa kweli mafanikio makubwa yamepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Abdallah Bulembo kwamba Serikali iwaajiri vijana wa JKT walioshiriki ujenzi wa ukuta Mererani. Nadhani jibu lake limeshatolewa na Mheshimiwa wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya vijana wa mujibu wa sheria iongezwe ili ichukue vijana wengi. Hili linafanyiwa kazi, sasa hivi tumeongeza kambi za JKT katika maeneo kadhaa lengo ni kuongeza vijana wanaochukuliwa kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea ili wale wote wanaomaliza form six kabla ya kujiunga na vyuo vikuu waweze kujiunga na jeshi angalau kwa kipindi kifupi waweze kupata yale ambayo yamekusudiwa katika jukumu hili la kujiunga na JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo kuhusu vijana wa JKT na malalamiko yao kuhusu ajira. Hapa ni vyema nikalieleza hili kwa kina kidogo ili lieleweke. Vijana wanaokwenda JKT kwa kujitolea sasa hivi wamezidi kuongeza sana na sababu ni kwamba wanadhani ndiyo njia ya kupata ajira. JKT imekuwa ikitoa ufafanuzi na mimi napenda niurudie hapa, kwamba kujiunga na JKT kwa kujitolea hakukupi uhakika wa kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaobahatika wachache, wataajiriwa na wale ambao hawapati nafasi za ajira watapewa stadi za kazi ili wanapotoka JKT waweze kujiajiri wao wenyewe. Hili ndilo lengo na miezi sita ya kwanza wanafundishwa mafunzo ya kijeshi na baada ya hapo wanafundishwa stadi za kazi ili hatimaye wale wanaokosa ajira waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vyema Waheshimiwa Wabunge wakati wa usaili wa vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika wilaya zetu watambue hilo. Maana wao wanadhani watu 5,000 wote wataingia katika jeshi hili sio jambo ambalo linawezekana kwa sababu inategemea na idadi ya nafasi za ajira zinazotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwamba sasa hivi tunafarijika sana kwamba vyombo vyote vya ulinzi na usalama kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ajira zinafanyika kupitia JKT. Polisi, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi lenyewe na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama wanachukua vijana kutoka JKT kwa ajili ya ajira katika vyombo hivyo. Bado vijana wanaojiunga na JKT ni wengi mno kuweza wote kupata ajira. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba vijana hawa wawe tayari kujifunza stadi zile wanazopewa ili hatimaye waweze kwenda kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro mingi ya ardhi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumzia kati ya jeshi na wananchi. Nitaizungumzia baadhi, kwanza, Serikali ishughulikie mgogoro wa ardhi kati ya Kambi ya JKT Itaka na vijiji jirani. Kambi hii ilirithi eneo lililokuwa shamba lililokuwa Maganga Estate ambalo lilikuwa limepimwa kwa muda mrefu na kukabidhiwa kwa JKT. Hii ni hoja ya Mheshimiwa Haonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuonekana dhahiri kuwa wananchi wamevamia eneo kubwa la kikosi kulifanyika upimaji upya na kupunguza eneo la shamba la JKT kwa wananchi. Kwa mgogoro huu uliotajwa na Mheshimiwa ni dhahiri kuwa wananchi wamezidi kuvamia maeneo ya kikosi. Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ulinzi na JKT, itaenda kufanya tathmini ya hali ya uvamizi na kushauri nini kifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengine ya migogoro ya ardhi kwa mfano katika eneo lile la Mheshimiwa Esther Matiko, anataka kwamba JWTZ ilipe fidia ya ardhi iliyotwaliwa la sivyo irudishe ardhi kwa wananchi. Tunasema kwamba eneo linalotumiwa na JWTZ la Nyamisangura lilitwaliwa kwa kufuata taratibu za Sheria ya Ardhi ikiwa ni pamoja na kufanya upimaji na uthamini kwa ajili ya fidia. Eneo hili lina ukubwa wa hekta 123.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uthamini wa mali za wananchi ulifanywa mwaka 2015 na kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zilitakiwa kulipwa kwa wananchi 204 kama fidia. Ahadi ya Serikali ni kulipa fidia kwa mujibu wa Sheria za Ardhi zilizopo kwa kuzingatia thamani ya sasa ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Rasi Mshindo kule Kilwa, hili nilishalizungumzia kwamba tunajipanga ili fedha za fidia zitakazopatikana ziweze kulipa fidia katika eneo hili ili iundwe ile base ya navy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Jeshi Mtoni Zanzibar siyo nzuri kiusalama, imevamiwa na shughuli za kibiashara kama vile maduka, bar na sehemu za kuoshea magari. Je, shughuli hizi ni za Jeshi? Eneo hili la Kambi ya Jeshi Kikosi cha 111 Mtoni kabla ya ujenzi wa uzio na vibanda vya biashara lilikuwa likitumiwa na watu ambao ni waovu. Hivyo uwepo wa shughuli hizo za kibiashara unasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo. Shughuli hizo zinaratibiwa kikamilifu na jeshi lenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja ya Mzinga kwamba shirika lijikite zaidi katika maeneo ambayo wanaweza kufanya kwa ufanisi mfano shirika lilipewe kazi ya ujenzi wa barabara katika Wilaya ya Malinyi, Morogoro na walishindwa kufanya kazi hiyo kwa ubora na kwa muda uliopangwa. Miradi ya barabara ya Malinyi ilisainiwa Machi, 2016 na ilitakiwa kukamilika Juni, 2016. Kazi ilipoanza ilikumbwa na kipindi cha masika ikabidi zisimame kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika ulipoombwa muda wa ziada mteja ambaye ni Halmashauri ya Malinyi aliamua kusimamisha kazi, vifaa vyote vinavyotakiwa kwa barabara ya kiwango cha moramu vilikuwepo eneo la kazi. Kampuni ya Mzinga Holding imetekeleza miradi mingi vizuri kama Halmashauri ya Mkalama, Ikungi na Hospitali ya Manispaa ya Morogoro. Hiyo ni mifano michache kati ya miradi mingi iliyotekelezwa vizuri kwa ubora na ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuhakikisha karakana ya Nyumbu inaimarishwa hadi kuunda magari yake ukiacha matengenezo ya kawaida na uchongaji wa vyuma. Ushauri huu umezingatiwa, shirika kwa kushirikiana na wadau limeandaa mpango wa maendeeleo wa miaka 10 wenye azma ya kuliimarisha. Mpango umelenga kulirejesha shirika kwenye lengo la kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa gari la Nyumbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine ya mradi ya matrekta ambayo nadhani nilishauzungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hii hoja ya wanajeshi 19 waliouwawa Congo DRC na wengine kujeruhiwa, je, ni lini watarejeshwa? Nadhani hoja hapa Mheshimiwa Mbunge alisema kuna uzembe mkubwa; hawana zana zinazotakiwa na hawakupata msaada kwa sababu ya uzembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii nimwarifu Mheshimiwa Mbunge pengine ni vyema kabla hajatoa hoja zake Bungeni angekuja kuonana na mimi nikampa taarifa. Mimi mwenyewe nilikwenda Congo baada ya ajali hii, niliona na niipata maelezo ya kina na najua mambo yote yaliyotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya Mheshimiwa Mbunge, kule kuna Brigedi inayoitwa Force Intervention Brigade (FIB) inaundwa na nchi tatu: Tanzania, Malawi na Afrika ya Kusini. Kila kikundi kati ya vikundi hivi vya nchi tatu kina uwezo wake tofauti. Wenzetu wa South Africa wana uwezo wa mapigano ya ndege, kwa hiyo helkopta ni za South Africa, Watanzania na Malawi wana zana za aina nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipotokea ambush hii kwa sababu eneo hilo ni mbali ililazimika ndege zitumike jambo ambalo halikufanyika. Kwa hiyo, kusema uzembe wa Watanzania au kwa sababu kikosi chetu hakina silaha za kutosha ni makosa. Ningependa Mheshimiwa Mbunge wakati mwingine anione ili nimpe taarifa kwa sababu kauli kama hizi hazifai kutolewa ndani ya Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze vilevile Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeunda Tume ya Uchunguzi na imeshatoa taarifa yake. Kama nilivyosema katika hotuba yangu leo asubuhi, wadau wote wakiwemo Umoja wa Mataifa, nchi hizi ambazo zinaundwa Brigade hiyo ya FIB pamoja na ule uongozi wa MONUSCO, kila mtu atachukua hatua stahili kuhakikisha kwamba matukio kama haya hayatokei tena. Kwa hiyo, wanapokwenda watu katika operesheni ajali huwa zinatokea, hili tulielewe. Kwa hiyo, kusema kwamba ni uzembe kwa kweli hii siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu stahili za wanajeshi, juhudi za Wizara za kuwapatia wanajeshi wetu makazi bora ziendelee kwa lengo la kuwapatia wanajeshi makazi bora na yenye utulivu. Ukweli ni kwamba kweli bado wanajeshi wengi wako uraiani, lakini Serikali imefanya juhudi kwani tumejenga nyumba 6,064 ambazo lengo lake lilikuwa ni kupunguza wanajeshi wanaokaa uraiani warudi makambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kila sababu ya wanajeshi kurudi makambini kwa sababu pamoja na mambo mengine nidhamu lakini vilevile wanapohitajika waweze kupatikana haraka. Kwa hiyo, Serikali itaendeleza juhudi hizi za kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga makazi ya wanajeshi kwenye makambi ili hatimaye wanajeshi wote warudi katika makambi, lakini hii itategemea sana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya stahili kwa wanajeshi walioshiriki Operesheni Kibiti kama wamelipwa stahili zao zote na kiwango walicholipwa kama kinafanana na kile walicholipwa wenzao wa TISS na Polisi. Askari walioshiriki katika Operesheni Kibiti wote wameshalipwa stahili zao kwa mujibu wa taratibu za JWTZ. Aidha, kila taasisi ina utaratibu wake wa malipo inapokuwa kwenye jukumu fulani. Hivyo ni vyema ieleweke kwamba jeshi limelipa kwa taratibu zake na kwa maana hiyo halipaswi kulinganishwa na taasisi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mishahara ya wanajeshi kuongezwa na posho zao pia zipatikane, ninachoweza kusema ni kwamba mishahara ya wanajeshi inaongezwa mwaka hadi mwaka kwa kadri fedha za bajeti zinavyoruhusu. Napenda pia niseme kwamba posho zao zinapatikana, wanajeshi wanapata posho zao, ni kweli kwamba wangependa ziongezeke na sisi sote tunapenda iwe hivyo, lakini hili linategemea sana uwezo wa Serikali. Nataka niwahakikishie kwamba uwezo wa Serikali utakapoongezeka basi kila mara posho zao zitakuwa zinaongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya kwamba matukio mengi yanayoashiria vitendo vya ugaidi yanaongezeka nchini na kwamba sasa litumike jeshi kudhibiti vitendo hivyo. Kama nilivyosema awali ni kwamba kumekuwepo na matukio kadhaa yenye viashiria vya ugaidi nchini na matukio haya yamesababisha vifo, majeruhi na hofu kwa wananchi. Hata hivyo, matukio haya yamekuwa yakidhibitiwa na Jeshi la Polisi, JWTZ limeendelea kujizatiti kukabiliana na matukio yote ya kigaidi endapo litahitajika kushiriki kama ilivyofanya katika Operesheni iliyotokea pale Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira, Mheshimiwa Halima Mdee kwa ufupi anachojaribu kusema ni kwamba hawa vijana wanaojiunga na JKT wapate ajira. Kama nilivyosema awali tutaweza kuchukua baadhi yao, haiwezekani wachukuliwe wote kwa sababu idadi ya wanaojiunga ni wengi mno na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitafanya hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iongeze muda wa mafunzo kwa mujibu wa sheria ili kuwajengea vijana uwezo wa kujifunza zaidi stadi za kazi. Mabadiliko ya muda wa mafunzo kwa vijana kwa mujibu wa sheria ni suala mtambuka kwani limechangiwa na mabadiliko ya mihula ya masomo ya kujiunga na elimu ya juu. Hata hivyo, wadau wa pande zote wanaendelea kukutana ili kuona namna nzuri itakayopelekea vijana kupata mafunzo kwa muda stahiki na kunufaika na mafunzo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana nyingine ni kwamba sasa hivi vijana wanaomaliza form six wanachukuliwa kwa awamu kwa muda wa miezi mitatu tu ambayo na sisi tunakiri kwamba pengine haikidhi haja. Ni vyema muda huu ukaongezeka lakini utaingiliana na muda wa kujiunga na vyuo vikuu. Ndiyo maana wadau wameanza kukaa na wataendelea kukaa ili kuweza kupata ufumbuzi wa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makambi ya JKT kuwa machakavu na kwamba Serikali iongeze juhudi za kuyaboresha, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kuboresha makambi haya. Kama tulivyosema kwamba fedha za mwaka huu wa bajeti tayari shilingi bilioni tano zimekwishapatikana na kazi hiyo inaendelea kwa kuboresha na kuanzisha makambi mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa vijana kusailiwa kujiunga na JKT, Wabunge wanatoa hoja kwamba pengine utaratibu siyo mzuri na wanaiomba Makao Makuu ya JKT waende hadi ngazi ya wilaya ili kuepusha upendeleo. Malalamiko haya tumeshayapata mara nyingi na tutautazama upya utaratibu huu lakini lazima niseme hapa na hili ni pamoja na Zanzibar, kulikuwa kuna hoja kutoka Zanzibar kwamba utaratibu tunaotumia wa kuchukua vijana kwenda JKT siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema ni kwamba jukumu la utaratibu gani utumike kwa Zanzibar ni la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Sisi tunapelekea nafasi hizo katika Serikali ya Mapinduzi na wao kwa mujibu wa taarifa nilizokuwa nazo mimi wanazigawa katika wilaya zao ili tuweze kupata vijana katika wilaya zote. Sasa kama kuna kasoro, basi nitawaomba Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kufikisha taarifa hizi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili wao wapange vizuri zaidi jinsi ya kuchukua vijana kutoka kule lakini hatuwezi kuliingilia sisi kwa sababu tukishawafikishia nafasi zao hilo ni jukumu la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupanga mchakato huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Bara, nimepata malalamiko vilevile kwamba kuna upendeleo. Baadhi ya wilaya vijana wa wilaya zile hawapati wanapata kutoka nje ya wilaya. Taarifa nilizokuwa nazo mimi ni kwamba jambo hili halifanywi na mtu mmoja linafanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama. Ni vyema basi tukahakikisha kwamba Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya zinahakikisha kwamba nafasi zinazotolewa kwa kila wilaya ni vijana wa wilaya husika tu ndiyo wanapata nafasi hizo. Tutapeleka wawakilishi wa Makao Makuu ya JKT ili tuweze kuhakikisha kwamba utaratibu huo unafuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele ya kwanza imeshapigwa, sasa nimalizie tu, kuna hoja ilitolewa kwamba wanajeshi wanakatwa fedha za chakula wanapokuwa katika mafunzo na pia wanalipia huduma za umeme, nadhani lilitolewa na Mheshimiwa Maryam Msabaha. Nadhani hii taarifa aliyokuwa nayo Mheshimiwa Maryam siyo sahihi. Wanajeshi wanapewa ration allowance na wanapokwenda kwenye mafunzo kwa sababu ration allowance zao wanazo wanatakiwa kujilipia chakula, lakini ni si kweli kwamba wanalipa umeme, umeme bado unalipwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pengine hoja hapa ilikuwa ni kwamba watu wapate ration allowance zao na wanapokuwa kwenye mafunzo walishwe. Hili tunasema kutokana na tatizo la kibajeti tumeona ni vyema kwa kuwa ration wanapata basi waweze kujilipia wao wenyewe na Serikali itaendelea kuwalipia wale ambao wako kwenye operesheni. Ukiwa kwenye operesheni kwa sababu hakuna mzabuni kule lazima Serikali ikulishe wakati huo huo fedha zako za ration zinaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa hoja ya Mheshimiwa Yussuf ambayo anasema hakuna amani katika nchi yetu. Naomba nimsihi sana, mimi nadhani tuko hapa leo tunazungumza na Watanzania katika nchi hii tunajivuna kwamba katika nchi zinazotuzunguka yenye amani peke yake ni Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kusema kwamba Tanzania haina amani siyo sahihi hata kidogo. Mipaka yetu yote iko shwari kama nilivyosema katika hotuba yangu na ndiyo maana Tanzania tuna amani na watu wanafanya kazi na maendeleo yanaonekana. Ndugu yangu ukienda nchi za jirani zetu Burundi, Congo, Somalia kote huku kuna matatizo makubwa sisi hatupaswi kusema hatuna amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesema katika hotuba yangu vilevile kwamba changamoto hazikosi, wapo wahalifu, wapo wanaoingia kwetu na silaha kutoka katika nchi zao, changamoto zipo. Wapo wanaowabughudhi wavuvi wetu katika mito na bahari, changamoto hizo zipo, lakini tuzichukulie kama changamoto ambazo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kuhakikisha kwamba tunaziondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla nchi yetu ina amani na mimi nataka nichukue fursa hii nilipongeze Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kuilinda nchi yetu. Nawaomba waendelee na moyo, uzalendo na weledi wao huo ili nchi yetu iendelee kuwa na amani tuweze kusonga mbele katika maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja.