Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na nianze kwa kuunga mkono hoja. Naomba pia nitumie nafasi hii kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Viongozi wa Wizara nikianza na Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na Wasaidizi wake wote pia Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wote kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa Wizara hii na vyombo vyake vinafanya kazi nzuri sana, wote tunajua nchi yetu iko salama na huu ndiyo msingi wa uchumi katika Taifa lolote, kama Taifa haliko salama basi hata jitihada zote za kujenga uchumi wa Taifa inakuwa ni matataizo. Tunajua pia jinsi ambavyo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikitusaidia kama Taifa pale tunapopata dharura na majanga mbalimbali, ku-rehabilitate miundombinu mbalimbali. Pia Jeshi letu limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za afya na elimu, kwa hiyo kwa kweli tunawapongeza kwa dhati kwa kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwapa pole Jeshi letu kwa kupoteza Askari ambao walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi na usalama ndani ya Taifa letu, lakini pia hata huko nje ya nchi. Serikali na Wizara tunayoiongoza, Serikali itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa Jeshi letu na Wizara hii katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya naomba nitolee ufafanuzi mambo machache. Kwanza kama nilivyosema Serikali itaendelea kuwezesha Jeshi kwa kuwapatia rasilimali kadri ya mapato ya Taifa letu yanavyoruhusu. Mathalani Fungu 38 - Ngome kwa mwaka huu wa fedha mpaka mwezi Aprili, upande wa matumizi ya kawaida tuliwapatia shilingi bilioni 307.9 ambayo ni asilimia 132 ya bajeti kwa kipindi hicho, kadhalika upande wa maendeleo Ngome walipata bilioni 13.4 ambayo ni takribani asilimia 202 ya bajeti ya kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu Namba 39 - JKT kwa upande wa matumizi ya kawaida tuliwapatia bilioni 194.1 ambayo ni sawa na asilimia 201 ya bajeti ya kipindi hicho. Kwa upande wa maendeleo hapa ndiyo tulikuwa na changamoto ambapo tuliwapatia shilingi bilioni moja JKT ambayo ni asilimia 20, kwa kipindi kinachoishia Aprili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu Namba 57 ambayo ni Wizara yenyewe, mpaka mwezi Aprili tuliwapatia shilingi bilioni 4.1 ambayo ni sawa na asilimi 81 ya bajeti ambayo ilipangwa kwa kipindi hicho na kwa upande wa maendeleo tuliwapatia bilioni 169.7 ambayo ni asilimia 99 ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli kwa upande wa Serikali tunajitahidi sana kuhakikisha kwamba Wizara hii na vyombo vyake vyote vinapewa priority katika utoaji wa fedha kadri makusanyo yanavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme ni kweli kabisa chombo hiki ni muhimu sana lakini ushauri kwamba Jeshi letu lisiwekewe ukomo wa bajeti ili kwa kweli naomba niwe mkweli siyo rahisi. Naowaomba Ndugu zangu Waheshimiwa tuelewane tusiwaambie Watanzania visivyo, kwa sababu rasilimali fedha hazitoshelezi mahitaji yetu mengi, lakini pili, yako mahitaji mengi, mengine ambayo nayo ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge walisema kwa nguvu kabisa juu ya mahitaji yetu ya maji katika Taifa, wamesema kwa nguvu juu ya mahitaji ya dawa na vifaatiba katika hospitali zetu, wamesema kwa nguvu sana juu ya umuhimu wa Serikali kuwezesha kilimo kukua, haya yote kama unachukua kwenye mtungi mmoja nayo lazima yapate kidogo. Haiwezekani ukasema Wizara yetu hii basi yenyewe isiwekewe ukomo, hili nitakuwa nadanganya na mimi ni msema ukweli daima ni vizuri nikasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kulikuwa na suala la utoaji wa posho ya chakula kwa ajili ya askari wetu. Naomba niseme tena kwamba tunajitahidi sana kadiri bajeti inavyoruhusu. Mpaka mwezi Aprili, Ngome peke yake tumewapatia zaidi ya shilingi bilioni 155.5 lakini upande wa JKT posho ilifikia shilingi bilioni 64.7. Kwa hiyo, kwa kweli tunajitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa na suala la madeni. Serikali inalipa madeni baada ya kuyahakiki na ni muhimu tufanye hivyo ili tujiridhishe kwamba kuna value for money kwa haya madeni ambayo vyombo vyetu hivi vimeingia. Mpaka kufikia Aprili kwa mwaka huu wa fedha peke yake, upande wa Ngome tumelipa shilingi bilioni 46.2, upande wa JKT tumelipa madeni ya shilingi bilioni 41.1. Kwa hiyo, unaona kabisa vyombo hivi viwili peke yake ni shilingi bilioni 87.5. Kwa hiyo, tunajitahidi kadri tunavyoweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palikuwepo pia hoja kwamba tulifuta misamaha ya kodi kwenye maduka ambayo yalikuwa yanawasaidia sana askari wetu. Waheshimiwa Wabunge, hatua hii ilichukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba ule motisha ambao ulikuwa unatolewa unawanufaisha walengwa na siyo baadhi tu ya askari na badala yake tuliweka utaratibu wa kuyapatia majeshi yetu posho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa upande wa Ngome mpaka kufikia Machi, posho ya fidia kwa misamaha ya kodi tumelipa shilingi bilioni 63.39 na upande wa JKT tumelipa shilingi bilioni 5.7. Kwa hiyo, siyo kwamba hatuwapi motisha askari wetu, hapana, hata kidogo, tunawathamini sana. (Makofi)

Mheshimwia Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa madeni, nayo tunajitahidi kulipa baada ya kuyafanyia uhakiki. Mpaka mwezi Aprili, upande wa Ngome tumelipa madeni yaliyohakikiwa ya shilingi bilioni 46.2 na JKT tumelipa madeni ya shilingi bilioni 41.1

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala kwamba Serikali itoe shilingi bilioni mbili ambazo hazijatolewa kwa ajili ya kukarabati miundombinu na ujenzi wa makambi mapya ya JKT. Hadi mwezi Aprili, tumetoa shilingi bilioni moja wa ajili ya ukarabati wa miundombinu na ujenzi wa makambi mapya ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika ilishauriwa hapa kwamba tutoe fedha kwa ajili ya ukarabati wa Kituo chetu cha Nyumbu na Mzinga. Napenda niliarifu Bunge lako kwamba shilingi bilioni mbili zimetolewa kwa Mashirika ya Nyumbu na Mzinga kwa ajili ya shughuli za utafiti na uzalishaji wa bidhaa ambayo ni sawa na takribani asilimia 40 ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la kulipa stahili za Majenerali Wastaafu. Viongozi hawa wamefanya kazi nzuri sana walipokuwa kazini, tunathamini sana kazi yao na kamwe Wizara yangu na Serikali kwa ujumla hatuwezi kuwaacha. Hadi Aprili, Fungu 57 lilipelekewa shilingi bilioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 63 ya bajeti ambayo iliidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya stahili za Majenerali Wastaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme la mwisho, kulikuwa na ushauri hapa kwamba kwa kweli fidia katika maeneo yaliyotwaliwa kwa ajili ya matumizi ya majeshi yetu ilipwe haraka iwezekanavyo. Ni kweli kabisa madai ya fidia haya ni makubwa lakini napenda nitoe commitment ya Serikali kwamba tutatoa kipaumbele kuyalipa yale ambayo yamehakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo machache, nirudie tena kuipongeza Wizara na vyombo vyake kwa kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.