Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii leo. Vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuwepo hapa leo nikiwa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na timu yake, naamini Kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi anafanya kazi vizuri na Mungu azidi kumpa uwezo wa kuliongoza Jeshi hili ili tuweze kufika mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie kidogo suala ambalo amezungumza Mbunge mwenzangu hapa kuhusu Sera ya Ulinzi kwa upande wa Zanzibar. Sera hii kwa sasa imeshafanyiwa kazi kwa hatua kubwa kwa upande wa Zanzibar, naona katika suala la Wizara limeshafika hatua yake ya mwisho na hivi sasa wanaelekea kwenye kikao cha Makatibu Wakuu. Nafikiri baada ya muda mfupi kitakwenda katika Baraza la Mapinduzi ili kupewa baraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niliona niliseme hili ili Waheshimiwa Wabunge kidogo wasiwe na pressure na hii sera kuhusu Zanzibar kuwa hali iko hivyo na sasa tunakwenda vizuri na ninafikiri tunaweza tukafika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sera siyo suala jepesi. Ukitaka kuitafsiri sera na ukitaka kuiandaa ili upate mafanikio, sera ndiyo inayojenga sheria, kwa hiyo ukiipata sera bora maana yake unapata sheria bora isiyokuwa na vikwazo. Kama hukuipata sera iliyokamilika, utakuwa bado hujapata sheria nzuri, baadaye tutakwenda kwenye matatizo. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, kwamba hali ya Zanzibar na hii sera iko vizuri na tunakwenda vizuri na ninafikiri tutafika mahali pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni uchukuaji wa vijana wa JKT kutoka Zanzibar. Hili suala nalizungumzia, kwa Mheshimiwa Waziri kila muda, bado mdogo. Angalau vijana 500 waweze kutoka Zanzibar kwenda JKT, tunachukua vijana kidogo sana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kupaangalia hapo ili awe na uwezo mkubwa wa kuchukua vijana kutoka Zanzibar ili waweze kwenda JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kuchukua vijana kutoka Zanzibar bado haziko vizuri. Nasema kila siku kumwambia Mheshimiwa Waziri, suala la uchukuaji kwa kule upande wa Zanzibar kupita kwenye Wilaya zetu, bado pana tatizo, hatupati vijana ambao Mheshimiwa Waziri au Jeshi wanakusudiwa kwenda. Kwa nini asibadilishe mfumo ili tukapata mfumo mzuri kwa upande wa Zanzibar ili kupata vijana wa kuweza kuja kufanya kazi vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar tuna kikosi cha JKU ambacho kinafanana katika utendaji wake na Kikosi cha JKT. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asikitumie hiki kikosi kwa awamu ya kwanza ili kuhakikisha vijana wa JKU wanakwenda JKT kutoka katika kikosi hiki? Kama haiwezekani vijana anaochukua kwenda kupata ajira basi watoke ndani ya kikosi hiki. Kama kina upungufu Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kukiendesha kile kikosi ili kiweze kujipanga vizuri ili vijana wapate ajira kutokea JKU. Tukikitumia kikosi kile basi tunaweza kupata vijana wazuri ambao waweza kufanya kazi vizuri ndani ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ni vijana waliojenga ukuta. Vijana hawa wamepewa matumaini makubwa na wanasubiri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akija apate kutoa jibu la uhakika kuhusu vijana hawa waliojenga ukuta, wameahidiwa ajira, sasa wanasubiri ajira na Mheshimiwa Waziri ndiyo mdhamini wa vijana hawa, wako ndani ya JKT wanasubiri maamuzi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Bunge wanakaa wanalisikiliza kwa kina watapewa maamuzi gani kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri vijana hawa tuweze kuwajibu vizuri ili kama kuna ajira ya kuwapeleka kabla muda wao haujakwisha basi Serikali iweze kuwachukua kwa sababu wengine muda wao unakaribia kwisha na kazi ile wameifanya, wahakikishe na wao wameshapewa matumaini wajue wanakaa vipi. Nimwombe sana Kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, hili aweze kulijibu kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la makazi. Tulimelizungumzia sana na sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu afanye utaratibu hawa Askari wetu waweze kupata makazi mazuri. Nyumba zao zimeshakuwa za muda mrefu, Wabunge wengi wanalizungumza hili suala, lina matatizo. Mheshimiwa Waziri afanye jitihada zake ili aweze kutatua kero hii ya makazi kwa Askari wetu, bado wanalitumikia Jeshi letu vizuri na hawana matatizo na Jeshi letu. Kwa hiyo, namwomba sana aweze kufanya hii kazi kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu migogoro. Bado Wabunge tunasema baina ya Wakaazi na Wanajeshi kuna migogoro ya kimipaka, tatizo hili linaendelea kuwa kubwa. Wananchi wanasubiri malipo yao, hawajui watalipwa lini, wanasubiri angalau kauli ya Mheshimiwa Waziri tujue tunafanya nini, bado wananchi wetu wana matatizo makubwa na Jeshi lao kutokana na migogoro. Majeshi yamevamia au wananchi wamevamia, kwanza Mheshimiwa Waziri, haya madeni ambayo wanadai hawa wananchi basi tufanye maarifa ili waweze kulipwa kwa wakati ili hii sintofahamu baina ya Jeshi lao pamoja na wananchi wetu, tatizo hili linatatuliwa kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kikosi chake na kazi ambayo anafanya iko vizuri, Jeshi letu liko vizuri, nchi yetu iko salama kwa sababu ya Majeshi haya. Lazima tuwaunge mkono na kitu kikubwa bajeti yao lazima iende kwa wakati, ifanye kazi vizuri. Tunalala na tunapata usingizi Tanzania kwa sababu Jeshi hili liko imara na tunaliombea dua liweze kufanya kazi zaidi ya hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tunaweza kulitumia Jeshi katika uzalishaji, tusitumie Jeshi katika ulinzi tu bali na uzalishaji pia Jeshi letu tunaweza tukalitumia kwa hatua kubwa. Suala la kiuchumi, wenzetu wanalitumia Jeshi katika ulinzi lakini vilevile katika kuimarisha uchumi wa nchi. Jeshi lina uwezo mkubwa, mambo mengi wanaweza wakafanya katika nchi yao kuhakikisha wanakuza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii.