Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naungana na wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, kipekee naomba nimpongeze Mkuu wa Majeshi kwa kutambua umuhimu wa Wakuu wa Majeshi wastaafu ambao amewaalika. Hii inaonesha jinsi gani wapo tayari kushirikiana na kuendeleza amani iliyopo nchini mwetu na inatoa faraja sana kwa kuona ushirikiano uliopo inaonesha kwamba Tanzania bado tupo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana kadhaa wa JKT waliopo katika kambi mbalimbali nchini mwetu, vijana hao wamefanya kazi ya kujitolea kwa muda mrefu. Naiomba Serikali ajira zinapotokea basi wale wawe wa kwanza kuajiriwa kwa sababu wamefanya kazi ya kujitolea kwa muda mrefu. Hii itawasaidia kujenga uzalendo na hivyo kuendelea kuitetea nchi yao badala ya kuendelea kuwaweka pale muda mrefu na kuwakatisha tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuwapongeza SUMA JKT kwa kazi nzuri wanayoifanya. SUMA JKT wanafanya kazi nzuri na kwa bei nafuu sana. Nimeweza kuona majengo yao katika Zahanati ya Kiboga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala, lakini pia nimeweza kuona majengo waliyojenga katika Shule ya Sekondari Nyakato Mkoani Kagera na gharama yao ni ndogo na majengo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali isiwe inawakopa SUMA JKT, wawe wanawalipa pesa zao zote na kwa wakati muafaka, hasa ukizingatia kwamba katika malipo yao wanaondoa faida na pia wanaondoa ile gharama ya vibarua, badala ya kuleta labour charge wao wanaleta labour force. Kwa hiyo, ni vizuri walipwe mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuishauri Serikali yangu sikivu kuhusiana na suala hilo hilo la SUMA. Vifaa vingi kwa kuwa SUMA JKT wanajitolea na wanafanya kazi nzuri basi hata maofisini kwetu tuwe tunachukua vifaa kutoka SUMA na majengo yetu yawe yanajengwa na SUMA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie katika suala la utumiaji wa silaha za moto vibaya, limekuwa ni tatizo kubwa nchini. Wakati huo huo niipongeze Serikali kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali wameweza kulimaliza tatizo hili katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono suala zima la kununua silaha za kisasa zaidi, kutoa mafunzo zaidi na kuwawezesha wapiganaji wetu kiuchumi ili tuendelee kuwatia moyo na pia kuwapa fursa ya kutumia ujasiri wao katika kulinda nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala zima la mavazi yanayofanana na jeshi, wapo baadhi ya wananchi ambao wanatumia mavazi haya lakini kuna wananchi ambao wamenunua kihalali dukani wanayavaa, lakini wanapata bughudha na saa nyingine kudhalilishwa kutokana na mavazi yale. Niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa basi atueleze ni kwa nini basi nguo zile zisipigwe marufuku ili wafanyabiashara wasipate hasara na wananchi wasiendelee kubughudhiwa kwa kuvaa mavazi yanayofanana na mavazi ya jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la malalamiko katika maeneo mbalimbali ambayo yamechukuliwa na jeshi. Nikitolea mfano katika eneo la Mapinga Wilayani Bagamoyo, kuna maeneo ambayo Wanajeshi wamechukua, lakini hawajalipa fidia hadi sasa na wengine tathmini yao haikuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu ana heka nne lakini anaandikiwa ana heka mbili, lakini mwingine anapiga tathmini bila kuangalia mazao yaliyopo ndani ya shamba lile. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa na hilo pia analifahamu atakapokuja tunaomba tupate maelezo ni lini wananchi wa Mapinga Bagamoyo na maeneo mengine yenye tatizo kama hilo watalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje pia na jibu ni lini Kambi za Jeshi zilizopo Mjini zitaondoka ili kuondoa bughudha kwa wananchi. Kumekuwa na changamoto nyingi katika maeneo ambayo Kambi za Jeshi zipo Mjini, nikitolea mfano katika Kata ya Majohe, Jimbo la Ukonga Mkoa wa Dar es Salaam ambapo Wanajeshi mara kwa mara wanavurugana na wananchi kwa sababu binafsi zikiwepo mambo ya mapenzi na ulevi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Wanajeshi wetu wale wenye nidhamu nzuri wanaendelea kuonesha nidhamu nzuri na wanashiriki vya kutosha katika shughuli mbalimbali za dharura zinazojitokeza hapa nchini, yakiwepo mafuriko, matetemeko ya ardhi, lakini pia na ajali mbalimbali wanajeshi wamekuwa wa kwanza kujitokeza na kutoa msaada kwa wananchi, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi pia kutaka maelezo ya kina kuhusiana na maendeleo ya michezo ya Majeshi hapa nchini. Siku za nyuma Wanajeshi wengi walikuwa wanatupa sifa nchini katika michezo mbalimbali na hivyo kuitangaza Tanzania, lakini sasa hivi tumeona kimya. Je michezo Jeshini imekwisha au Wanajeshi sasa hivi hadhi yao kwenye michezo imeshuka? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze maendeleo ya michezo katika Jeshi yakoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwapongeze wanajeshi hao na timu nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza mila na desturi za Watanzania kupitia ngoma, michezo, sarakani na maigizo. Tumewaona kwenye shughuli mbalimbali za Kiserikali Wanajeshi hawa unawasahau kama hawa ni Wanajeshi jinsi wanavyoweza kuweka burudani na kudumisha mila na desturi za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa katika ajira tuangalie wilaya na mikao yote wapate ajira ili zile mila na desturi zinazolindwa jeshini ziwe za makabila yote, zisionekane ni za makabila mawili au matatu tu ndiyo yenye uwezo wa kutunza mila hizo kupitia jeshini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika suala la amani, wenzangu wengine walichangia lakini kuna mchangiaji mmoja ambaye alisema Tanzania sasa hivi haiko salama. Nataka kusema kwamba, Tanzania ipo salama ndiyo maana mpaka sasa hivi tupo hapa Bungeni. Wanajeshi hawa wamefanya kazi nzuri sana ya kulinda nchi yetu, kuna nchi wanalala saa tisa alasiri kwa sababu hakuna amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuonesha kwamba Tanzania amani ipo, bado tuna wimbi la watu wanaomba uraia wa Tanzania, kuna wimbi la watu ambao wanatoroka kwao wanataka kuja Tanzania, kuna maharamia haramu wamenga’ang’ania kuja Tanzania. Sisi tupo hapa unatoka Biharamulo mpaka Pemba, unatoka Mtwara mpaka Chato, unatoka Mbeya mpaka Chanjamjawiri, hakuna anayekuuliza hamna nini, halafu unasema Tanzania haina amani. Kipindi hiki ni kipindi cha kuwapa nguvu Wanajeshi wetu, kuwapongeza na kuthamini kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii bajeti yake isipunguzwe, wapewe kama walivyoomba na naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza.