Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufufua viwanda vyetu hasa viwanda hivi vidogo vidogo ni lazima suala la kuwa na mashine au vitendea kazi na wataalam kutazamwa kwa macho mawili. Taasisi hii ya SIDO ndiyo taasisi yenye uwezo na taaluma ya kutengeneza mashine ndogo ndogo ambazo zinawasaidia wananchi wetu wenye kipato cha hali ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ni lazima Serikali iimarishe na kufanya shughuli zake za kuhakikisha SIDO inaweza kuimarishwa kwa kupatiwa mtaji. Mara nyingi pesa zimekuwa zikitengwa kupelekwa SIDO, lakini zikawa haziendi. Kwa hiyo, naomba kabisa SIDO iweze kutizamwa kwa macho mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa SIDO haifanyi vizuri kwa sababu baadhi ya vitendea kazi kama mashine, zimepitwa na wakati. Haziwezi kufanya ushindani na mashine zinazotoka nchi za nje kwa sababu mashine zetu zilizopo sasa hivi ni zile za muda mrefu. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweze kutoa pesa kusudi SIDO iweze kwenda sambamba na mashine zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Hivyo basi, naomba Serikali iweze kuhudumia SIDO na kuipa wataalamu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuiimarisha SIDO. Katika ukurasa wa 143 wameandika ni jinsi gani watakavyohakikisha SIDO inaweza kuimarika na wamesema; “Kutumia SIDO kama nyenzo ya kujenga viwanda vidogo vidogo na vya kati kwa kuendelea kulifanyia maboresho shirika hilo la SIDO na kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia.” Kwa hiyo, ninaomba sana kazi hiyo ya kuhakikisha SIDO inaimarishwa iweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka ni lazima maonesho yanakuwepo. Mara nyingi wananchi wa kutoka vijijini wanakuja kuonesha biashara zao kwenye maonesho lakini tatizo ni masoko. Kwa hiyo, naiomba Serikali ihakikishe inawaruhusu wanafanya maonesho, lakini itafute masoko

kwa sababu wanapokuwa wamepeleka kwenye maonesho wanakaguliwa halafu wanakosa maeneo ya kupeleka kuuza bidhaa zao, wanakata tamaa. Kwa hiyo, naiomba Serikali, sambamba na kufanya shughuli ile ya maonesho, lakini iweze kutafuta masoko kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Zainab na Mheshimiwa Zitto Kabwe, katika Mkoa wa Kigoma tunalima zao la michikichi. Tunaiomba Serikali iweze kuja kuwekeza Kigoma ili tuweze kuanzisha viwanda vya mafuta na vilevile viwanda vya kutengeneza dawa kwa sababu zao la michikichi linatoa mafuta, lakini vilevile linaweza likasaidia kuanzishwa viwanda vya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa nataka kuzungumzia uwekezaji wa kiwanda katika Wilaya ya Kasulu, Kijiji cha Kitanga. Aliwahi kuja mwekezaji, karibu miaka 10 iliyopita, akaja akaoneshwa eneo, tangu ameondoka hajaweza kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naiomba Serikali mpaka sasa hivi eneo hilo lililoko katika Kijiji cha Kitanga, bonde ambalo ni la Mto Malagarasi bado lipo, kwa hiyo, bado tunaihitaji Serikali iweze kututafutia mwekezaji katika bonde hilo ili aweze kulima kilimo cha miwa, lakini vilevile aweze kujenga kiwanda cha sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutaweza kuimarisha uchumi wetu na viwanda vitaweza kuongezeka. Ni lazima tuhakikishe tunawekeza katika kilimo ili viwanda viweze kupatikana kutokana na mazao ya kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamekuwa wakiogopa kuja Kigoma kwa sababu ya miundombinu, lakini naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri, kwa sasa hivi miundombinu Kigoma inaenda kuimarika, barabara zinajengwa, uwanja wa ndege wa Kigoma umetengenezwa na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake, ndege za bombardier zinakuja. Kwa hiyo, wawekezaji watakapokuwa wanakuja Kigoma, hawatapata shida kwa ajili ya kuja Kigoma kwa ajili ya kufanya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante.