Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Haji Khatib Kai

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Micheweni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameweza kuniamsha salama siku ya leo nikiwa na afya tele na kuweza kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ambayo Rais John Pombe Magufuli akilihutubia Bunge na kulifungua, aliwajengea wananchi wa kawaida matumaini makubwa kwa kule kusema kila alipokuwa akizungumza kwamba anawaomba wananchi na kuwataka wamuunge mkono kwa
kazi kubwa ambayo ataifanya ya kutumbua majipu ili nchi yetu iweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya game ilizunguka, majipu yaliyotumbuliwa yaliwagusa wananchi hawa kwa kuvunjiwa makazi yao, wananchi hawa wanyonge hawajui kwa kwenda hadi sasa, hawajui la kufanya na vilevile kusababisha maafa na kusababisha vifo
kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niseme kwamba Mheshimiwa Rais amewatelekeza wananchi ambao alisisitiza kila alipokuwa akizungumza kwa kutaka wamuunge mkono na kwa kutaka wamwamini kwa kazi kubwa ambayo amekusudia kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie hali ya kisiasa Zanzibar. Wakati Rais John Pombe Magufuli siku ya tarehe 20/11/2015 akilifungua Bunge hili alimtanguliza Mungu mbele kwa kusema kwamba atautatua mgogoro wa Zanzibar kwa utulivu na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kusema kwamba baada ya yote hayo, Mheshimiwa Rais kumtanguliza Mungu mbele na wakati Mheshimiwa Rais akienda kwenye maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 2016 Mheshimiwa Rais alikwenda kutangaza
kurudia Uchaguzi wa Zanzibar. Nimeamua kusema hili kwa sababu kiongozi yeyote wa chini kiprotocol anapozungumza jambo mbele ya Kiongozi Mkuu, basi kauli ile inakuwa siyo ya kiongozi wa chini bali ni ya kiongozi wa juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar siku zote tumekuwa tukisikia kauli aina mbili ambazo zikitolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kauli zinazosema kwamba Serikali ya Mapinduzi haiwezi kutolewa kwa makaratasi, hatutoi, hatuitoi, hatuitoi labda wapindue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya pili ambayo imekuwa ikitolewa na Chama cha Mapinduzi inasema kwamba Serikali ya Mapinduzi haiwezi kutolewa kwa kura, hilo wasahau.
Masuala ya kujiuliza ni kwamba, kwa nini Zanzibar iendelee kufanya chaguzi ikiwemo hiyo ya marudio. La pili, milioni ngapi zinatumika kugharamia chaguzi ambazo majibu yake yanajulikana? Nini tija ya kufanya hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, chaguzi ngapi zimefanyika huko nyuma ambazo zimekuwa zikilalamikiwa lakini hazijawahi kurudiwa? Seuze chaguzi huu wa mwaka huu ambao matatizo yake yamekuwa madogo na yangeweza kushughuhulikiwa kwa gharama ndogo sana. Yote haya ya kulazimisha kurudia uchaguzi ni kwa sababu ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali ya CCM na viongozi wa CCM hawawezi kujifunza kwa yanayotokea duniani kama vile Somalia, Afghanistan, Misri, Libya na kwingineko. Raia wa nchi hizi hawakutaka kufikia hapa walipo, lakini walisababishwa kufikia
hapo walipo na uongozi dhalimu wa nchi zao kama vile uongozi dhalimu wa CCM na viongozi wao ambao wamekusudia na wamepanga sasa kutupeleka ambako siko, kule Zanzibar.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM na viongozi wa CCM wamekuwa wakitudhulumu kule Zanzibar; mwaka 1995 walitudhulumu, mwaka 2000 walitudhulumu, mwaka 2010 walitudhulumu na mwaka 2015 wanapanga kutudhulumu!
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nakizungumza hapa ni hali ya kisiasa Zanzibar, kwa hivyo sioni sababu kusema kwamba kuzungumzia chaguzi zilizopita ili tujue nini tufanye.
Nilichokuwa nasema, Serikali hii ya CCM na viongozi wake ambao wamekuwa wakituonea, wakitudhulumu, siku zote haikubaliki. Serikali ya CCM na viongozi wake walitudhulumu 1995, wakatudhulumu 2000, wakatudhulumu 2005, wakatudhulumu 2010, na 2015 mmepanga kutudhulumu! Haikubaliki, inauma sana, Mheshimiwa Waziri mkuu inauma sana hii. (Makofi)
MHE. HAJI K. KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimalizie kwa kusema, endapo suala la Zanzibar halitapatiwa ufumbuzi wa haraka, nchi inakokwenda siko. Tumevumilia Wazanzibar vya kutosha vya kutosha na sasa mazungumzo yanakwenda, mazungumzo mnatudanganya, mnamdhalilisha kiongozi wetu, mnampeleka huku na kule, kumbe hamna nia njema na mazungumzo.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, hili limeonekana kwamba linagusa hisia za watu…
MBUNGE FULANI: Wewe mbishi.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Basi niseme tu kwamba kwa hapo nilipofikia, nasema ahsante.