Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Mheshimiwa Mwijage na Naibu wake wanafanya kazi nzuri sana. Naomba tukiri hilo kwamba wanafanya kazi nzuri isipokuwa tu ni kwamba uwezeshwaji wa kufanya kazi ndiyo kuna matatizo. Hii nadhani sisi kama Bunge tufikie mahali tutafute namna ya kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni mtambuka, ina mambo mengi sana. Bila kusaidiwa na kuwezeshwa kufanya kazi, itakuwa ni hadithi. Ndiyo maana anajiita ni Mzee wa Sound, ni kweli anapiga sound tu, anazunguka huku na huku, anapiga sound. Nadhani tafsiri halisi ya Mheshimiwa Mwijage mimi ninavyofikiri ilikuwa ni kwamba kauli ya Watanzania katika uchumi wa viwanda iweze kushamiri. Mheshimiwa Mwijage, umefanya kazi nzuri, lakini bado kuna wingu kubwa sana la tafsiri ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali kama nchi tuweze kuwa na tafsiri pana na iliyo sahihi. Unaposema viwanda, cherehani tano ni kiwanda, kwa baadhi ya watu tunashindwa kukuelewa vizuri zaidi, kuna vitu vinaitwa factory na industry, sasa ni lazima kuwe na utofauti wa namna hiyo. Tukitofautisha hivyo, tukisema kwamba tumekuwa na viwanda 3,000 na kitu Watanzania wataelewa ni kitu gani. Nadhani tamaa kubwa ya Watanzania ni kuona kwamba mnapozungumzia viwanda ni vya kati na vile vikubwa zaidi ili viweze kuchochea zaidi katika kuleta uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii pamoja na yote inayofanya, kuna vitu ambavyo ni lazima mvisimamie kwa uhakika zaidi. Ni namna gani ya kumsaidia mwananchi huyu na hasa mkulima maana zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima kuongeza thamani ya mazao yao, tukishafaulu pale hiyo ndiyo Tanzania ya viwanda tunayoitaka. Bila hivyo, itakuwa tunaongea kama ngonjera tu. Haiwezekani leo hii tunazidi ku-import vitu kutoka nje ambavyo tunaweza kuzalisha hapa nchini na tukapunguza kutumia fedha zetu za kigeni kununua bidhaa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu mkulima wa pamba. Mkulima wa Pamba ana mateso makubwa sana. Mwaka 2017 alilima pamba na akapata bei nzuri ya Sh.1,200 ikamhamasisha kulima zaidi mwaka huu, lakini utaratibu uliopo mwaka huu unamvunja moyo mkulima wa pamba. Ni vema kuangalia namna ya kuweza kumsaidia, vivyo hivyo hata kwa wakulima wa mazao mengine, tuangalie namna ya kuweza kufufua vinu vya kuchambua pamba ambavyo vitaongeza thamani ya mazao ya mkulima. Namna ya kuanza kuwa na viwanda vya kuweza ku-process bidhaa ya mkulima kama ni pamba, tuweze kupata nguo hapa nchini. Bila ya kufanya hivyo, haiwezekani na lazima tuwe na sera ya kulinda viwanda vyetu. Bila kulinda viwanda haitawezekana. Haiwezekani tunaacha soko letu, tunaingiza tu bidhaa kutoka nje bila kuangalia viwanda vya ndani. Bila ya kuwa na hiyo sera, hatutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba sana Mheshimiwa Mwijage pamoja na Wizara yako, hili jambo mliangalie kwa makini, linamgusa Waziri wa Fedha. Lazima tuwe na sera za fedha na za kodi za makusudi kabisa za kulinda viwanda vya ndani. Kama ni kodi, basi tutoze kodi kubwa kwa bidhaa kutoka nje na tufanye zero rating kwa bidhaa za ndani. Tukifanya hivyo itasaidia kuchochea mkulima huyu aweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mkulima wa korosho amepata bei nzuri, wamehamasika zaidi na korosho inaendelea vizuri lakini mazao mengine yanaanguka. Mazao kama chai, kahawa, mbaazi na kadhalika, sina haja ya kuyarudia sana, lakini leo hii Tanzania miaka 57 ya uhuru bado tuna-import mafuta ya kula kutoka nje, hii ni aibu. Tufike mahali tuangalie namna gani nzuri zaidi ya kuwezesha kuzalisha bidhaa hapa hapa nchini ambazo zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuweza kupata uzalishaji wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, Wizara hii, Mheshimiwa Waziri acha tu kutembea mikoani, toka nje kaone, fanya economic diplomacy. Zunguka, tembea, unganisha nchi hii na mataifa mengine ili biashara ziweze kwenda. Haiwezekani kuna maonyesho mbalimbali ya kidunia, sijaona Waziri wa Viwanda na Biashara au Naibu wake nao wanafunga safari kwenda kuiunganisha Tanzania na dunia nyingine. Bila kufanya hivyo hatutakwenda tunapotaka. Mheshimiwa Waziri, wewe sio Waziri wa kwenda kijijini kwangu, kwenye kata, wewe Wizara yako ni muhimu sana. Tumwache Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI azunguke na kata na vijiji lakini wewe zunguka nje, tafutia Tanzania masoko na namna ya kuiunganisha kibiashara. Kama huwezi kushona suti, tukusaidie kutafuta suti nzuri uweze kuzunguka. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana Mheshimiwa Mwijage kwa sababu anafahamu na upeo wake ni mkubwa sana na toka amekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, tunaona anavyohangaika, sasa hiyo sound ipige mpaka nje, isiishie hapa peke yake. Msaidie Mheshimiwa Rais, kila siku anazungumza, ninyi wasaidizi wake msipomsaidia itakuwa ni mbio ya mtu mmoja. Hawezi kupiga ngoma mwenyewe akacheza mwenyewe, lazima Mawaziri mumsaidie Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ifike mahali Watanzania sasa tumsaidie Mheshimiwa Rais zaidi. Kila wakati unaona anavyolia, anavyohangaika, ninyi mnasema kama mlivyoagizwa, sasa mjiongeze zaidi ya hapo. Nami naomba sana kupitia hotuba hii ya bajeti, kwa kweli ningependa sana fungu la bajeti ya Wizara hii tuliongeze. Tufanye kila namna na Mheshimiwa Mpango najua wewe ndiyo unajaribu kumgawa huyu sungura mdogo, lakini tuwe na priority sectors na ministries kwamba tukiweka hela hapa itazaa na kusaidia Watanzania zaidi. Tufike mahali tufikirie zaidi, let’s think big, tusifikirie kidogo kidogo, tufikirie zaidi kwa mustakabali wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Fedha, najua kuna changamoto kubwa sana za kimapato, lakini tujaribu kugawa resources kulingana na mahitaji halisi ya kila Wizara. Wizara hii inatakiwa ipate fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Cotton to Cloth lazima ndiyo iwe wimbo wa Mheshimiwa Mwijage wa siku zote. Naomba katika sounds zake tutamuelewa tu kama kweli atatimiza azma hii. Hii inakuwa record yake kama Waziri ambaye ameanzisha mbio za Cotton to Cloth. Naomba sana viwanda vyetu hapa ndani tuzidi kuvilinda na wanaowekeza hapa ndani tuwasaidie, tuondoe urasimu wa uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIC iwasaidie. Siku hizi hakuna tax holiday, kuna tax incentives, lakini kuna conflicts. Mtu anakuwa na cheti cha TIC lakini watu wa TRA baadhi ya vitu hawavikubali, tufike mahali tu-harmonize. Haiwezekani mwekezaji anakuja hapa anazungushwa. Tunapata wawekezaji wanakuja hapa Tanzania kupata kibali tu hapa cha kujenga kiwanda au kufanya shughuli hapa, anazungushwa, wengine wanahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kuna watu walikuja hapa tukawazungusha wakaenda nchi jirani, wameanzisha viwanda vikubwa vya magari na vingine. Naomba tuache urasimu. Kama tunataka tuisaidie nchi hii Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na wadau wengine wanaohusika tuondoe urasimu kwa watu wanaokuja kuwekeza hapa Tanzania. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumeisaidia nchi yetu kuweza kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mikoa ya Kanda ya Ziwa inategemea sana kilimo, uvuvi na mifugo. Sasa wakulima wanalia, wavuvi wanalia na wafugaji wanalia. Sasa naomba tutoke kule, mtusaidie namna ya kufanya coordination na hasa viwanda hivi viweze kufanikiwa zaidi. Tukifufua viwanda itasaidia kuweka ajira hata kwa vijana. Vijana wengi wako mtaani hawana kazi, tuwasaidie kupitia viwanda. Naomba kuwe na sera mahsusi ya kuwawezesha Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu South Africa walikuwa wana sera inayosema ‘Black Economic Empowerment’ na sisi Watanzania tuwe na Tanzania Economic Empowerment, tuwawezeshe Watanzania. Leo hii Mtanzania ukienda hata kukopa hela unaonekana kama nyanya chungu au pilipili hoho, unaonekana kama mtu wa ajabu tu. Naomba Watanzania wapewe nafasi. Kama mtu anawekeza, apewe nafasi kadri anavyoweza kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Watanzania tuachane na mawazo ambayo ni ya kizamani, tuangalie dunia inavyokwenda sasa hivi. Wawekezaji wanabembelezwa, akishaondoka kuja kumpata inakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba Mheshimiwa Mwijage kaza buti. Punguza maneno kidogo tuone kazi zaidi na vitendo. Maana yake tukikutana mtaani hapo, unauliza unataka kiwanda? Kama unacho mfukoni, Mheshimiwa Mwijage acha style za namna hiyo, hebu kuwa serious kidogo. Maneno yako yaakisi kile unakifanya, nina imani una wasaidizi wazuri kwenye Wizara yako, fanyeni kazi kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.