Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nikushukuru kwa kunipa fursa hii, jioni hii kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Hata Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akihimiza sana viwanda na kasi yake. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, maneno mazuri sisi Waislam tunasema ni sadaka au maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, uongozi ni dhamana, ni jambo la kupita, leo lipo kesho halipo na baada ya siasa kuna maisha nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, biashara ni nini? Biashara haifanywi na mtu mmoja, biashara lazima iwe na monopoly. Biashara haiwezi kufanywa na mtu mmoja hata kidogo. Uzuri wa Wizara ya Biashara haiwezi kwenda bila ya fedha. Fedha ndiyo biashara, biashara ndiyo fedha, kwa hiyo, hivi vitu kidogo vinaoana. Hapa kidogo Mheshimiwa Waziri nataka unisikilize kwa makini, hasa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, nikuombe sana, kuomba siyo kosa, kuiba ndiyo kosa, kama kuna watu wanateseka, Benki ya FBMEwatu wanateseka, nimepiga kelele, nitaendelea kupiga kelele mpaka pumzi yangu ya mwisho. Watu wanaweka haki zao kule, wananyanyasika, wengine wameshaanza kutangulia mbele ya haki, hakuna harufu yoyote na Benki Kuu ndiyo dhamana na kama nilivyosema cheo ni dhamana na tutaenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu au mbele ya haki, tumetumia vipi dhamana zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanataka kusomesha, fedha zao zimekwama benki. Mnawaambia nini? Benki Kuu iko chini ya Wizara ya Fedha, Bureau de Change zote mna-control ninyi. Tumeona Greenland Bank imefungwa na wakati huohuo mnasema fedha za wateja ziko salama, salama iko wapi? Au Salama jina la mtu? Maana kuna jina la mtu Salama. Kuna wawekezaji Zanzibar pesa zao zimekwama, wafanyakazi wa benki pesa zao zimekwama, mishahara yao haipatikani.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa huruma na unyenyekevu, sijawahi kukuambia hivi Mheshimiwa Dkt. Mpango. Wewe binadamu na mimi binadamu, tuwe na jicho la huruma. Je, ungefanyiwa wewe au mimi tungekubali? Tuwaonee huruma wananchi. Wananchi ndiyo walioweka Serikali hii madarakani. Mtu ana shilingi milioni 200, unampa milioni moja na laki tano ni sawasawa na kumpa peremende baadaye ukamnyang’anya, haifai hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika kero za Muungano, biashara ndogondogo bandarini. Hii tuliambiwa moja kati ya kero ya Muungano. Msijali mtu wa mbali, jirani yako ndiyo mtu wa karibu. Tumetimiza miaka 54 ya Muungano huu na tuombe uendelee kudumu. Wafanyabiashara bandarini Mheshimiwa Mwijage wanateseka na hesabu inaanza moja ndipo ije mbili na tatu. Hawa wote wafanyabiashara wameanzia biashara ndogondogo wakafika kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa Zanzibar amechukua TV moja, amechukua mashati yake matatu, amechukua kilo zake sita za sukari akafika pale ananyanyaswa. Imefika wakati watu wakathubutu kuvunja TV zao, huu siyo ubinadamu wala siyo uungwana. Nikuombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Waziri wa Biashara mliangalie hili suala. Leo imekuwa mali inayotoka Zambia, Uganda, Burundi na Kenya inaingia hapa iko salama, inayotoka kwa ndugu zetu upande wa pili utafikiri umeleta bangi au unga, kwa nini tunafanya hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema na nitaendelea kusema, baada ya siasa kuna maisha nje, haya mambo ni ya kupita na cheo ni dhamana lakini hatuwatendei haki. Zanzibar inategemea zao la karafuu, uchumi wake wa pili ni biashara. Leo bandari imezuiwa usajili wa meli, kuna matatizo hatujui kinachoendelea, lakini tusiwanyanyase wafanyabiashara. Mtu ana TV moja, mbili, atakula nini? Anakuja na boti yake asubuhi, jioni apate kuuza aondoke lakini anakuja mzigo unaoza ndani mle, ndiyo lengo hilo? Katika moja ya kero kubwa ya Muungano hili ni moja, tuwe wakweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, hapa nisikilizeni vizuri. Kiwanda hiki kipo Tanzania, Tanzania hii imeitwa na Zanzibar ikiwemo. Tunalinda viwanda vya Tanzania, je, Zanzibar haipo Tanzania? That is my question. Tunalinda viwanda vya Tanzania, Zanzibar haiko Tanzania? This is my question au hailindwi Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalinda viwanda vya Tanzania Bara kwa hiyo Zanzibar haipo? Pombe, nondo, saruji, unga wa ngano unaingia Zanzibar lakini bidhaa kutoka kule kuleta huku imekuwa mtihani, tuwe wakweli. Ndiyo yale nimemwambia Mheshimiwa Keissy, moja iwe moja, mbili iwe mbili, mbichi iwe mbichi, kavu iwe kavu. Kama tunalinda tuseme tunalinda viwanda vya Tanzania Bara siyo Tanzania, tuwe na vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. au Prof. Mwijage maana cheo chao kikubwa, juzi ulijibu swali la 205. Mheshimiwa Spika aliona udhaifu wa swali hili, ningesema mimi ingekuwa mtihani, huku unakataa Tanzania hakuna uhaba wa sukari, huku unasema baada ya miaka mitano sukari itakuwa ya kutosha, tukamate wapi? Huku unakataa, uhaba wa sukari haupo, baada ya miaka mitano unasema uhaba wa sukari utakuwa umekwisha. Sasa tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Waziri toka kaangalie bandarini, hiyo sukari imeshafika usije ukauziwa mbuzi kwenye gunia. Uende ukapate ushahidi, usije ukapata ushahidi wa Kinyamwezi. Nenda kaangalie hii sukari uliyowapa vibali imefika? Isije kufika Ramadhan hapa tukawasumbua au kuwatesa wananchi. Narudia tena, Serikali hii isingekuwa madarakani bila wananchi. Hata Uwaziri wako huu,Mheshimiwa Waziri ungekuwa mtihani tungetawala nini, miti au barabara? Wananchi ni kitu muhimu. Hata Mheshimiwa Rais mwenyewe anawajali wananchi, tumpongeze kwa dhati kabisa hasa wananchi wa chini, credit yake kubwa iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isiogope kula hasara kwa mambo madogo madogo kama haya na wewe mshauri Mheshimiwa Rais usiogope kuwa hiki kiko hivi, hiki kiko hivi, mueleze tuna upungufu huu. Tuliwapa vibali vya sukari, mimi na ninyi, twende mguu kwa mguu kama sukari mliyotumbia imeshaingia tani 135,000, twende tukaiangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijamaliza lakini itabidi nishukuru hivyo hivyo kwa muda ulionipa.