Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo ya kuchangia sekta muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa. Kwanza kabisa, niwapongeze Wizara na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusimamia vizuri sana sekta hii ya viwanda na biashara kiasi kwamba wadau tunapata matumaini kwamba tunaweza kuifikia Tanzania ya viwanda ndani ya kipindi chake cha miaka 10 ya uongozi wake mahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kupata Tanzania ya viwanda kama tutaendelea kupuuza mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, nataka nitumie nafasi hii nieleze vizuri, ulianza kuzungumziwa na Mbunge mtangulizi wa Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mheshimiwa Prof. Simon Mbilinyi, lakini imekuja kuongelewa kwa zaidi ya miaka 10 na Mheshimiwa Jenista Mhagama (Waziri) na mimi ni Mbunge wa tatu kulizungumza hili lakini mpaka leo commitment ya Serikali imekuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Liganga kuna chuma, tathmini inaonesha chuma iliyopo Liganga inaweza kuchimbwa kwa kiwango cha tani milioni moja kwa mwaka, hiyo ni tani ya chuma. Chuma hii pamoja na kuzalisha chuma, inazalisha mazao mengine yanayoambatana na chuma. Kuna madini ya vanadium pentoxide na kuna titanium dioxide, haya nayo ni madini yanayoambatana na chuma. Watanzania wote tunajua chuma ni malighafi ya msingi ya viwanda. Ujenzi wa viwanda unatumia sehemu kubwa chuma, mashine zote za viwandani kwa asilimia kubwa zinahitaji chuma, unaipataje Tanzania ya viwanda bila kuchimba chuma ya Liganga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda jikoni utakuta kijiko, kisu, na uma, hivi vyote vinatengenezwa na chuma. Ukienda shambani utakuta jembe, panga, nyundo, vinatengenezwa na chuma. Ukipanda gari, asilimia 80 ya gari ni chuma, ni utajiri mkubwa sana Watanzania tumeauacha pale Liganga. Ipo mifano mingi, tukienda kwenye nyumba zetu tunazozijenga, bati ni product ya chuma, madirisha yetu, nondo na grill zote hizi ni product ya chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni viwanda vingapi vinaweza kuanzishwa kutokana na chuma ya Liganga? Tunaweza kutengeneza viwanda vya bati, viwanda vya nondo, viwanda vya magari na kila aina ya kiwanda tunachokitaka tutatengeneza na sisi wenyewe tutakuwa wateja namba moja wa hivyo viwanda. Hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda kama hatuweki makusudi kwenda kuchimba chuma ya Liganga.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1864, nchi ya Marekani iliahirisha ujenzi wa reli kwa sababu walitaka watumie chuma yao kujenga reli kwa sababu waliamini kiwango cha chuma ambacho kitahitajika kujenga reli iwapo kitachimbwa ndani ya nchi husika, kwanza kitaokoa pesa kubwa ya Serikali lakini kitachangia sana kwenye pato la Taifa. Mwaka ule 1864 wakati Marekani wanajenga reli chuma cha ndani kilikuwa na bei mara mbili ya chuma kilichokuwa kinatoka nje ya nchi ya Marekani, hata hivi kwa sababu ya uzalendo waliamua kutumia chuma iliyozalishwa ndani. Kwenye hili niombe sana Wizara iamue sasa kwenda kuchimba chuma cha Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chuma cha Liganga pamoja na kutoa malighafi ya tani milioni moja ya chuma kwa mwaka itatoa ajira takriban 4,000. Ajira 4,000 ni mchango mkubwa sana kwenye idadi ya ajira. Tumesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ni nzuri. Hata hivyo, ukifanya uchambuzi, ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2015 mpaka 2017 ni 26,113, ajira 4,000 zina mchango gani katika hiyo maana yake ni zaidi ya robo ya ajira zilizozalishwa katika kipindi hicho.

TAARIFA . . .

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili taarifa hii. Nikibaki hapo, ajira zitakazozalishwa kwenye mgodi huu wa chuma pamoja na spillover effect, maana yake ni zaidi ya ajira zilizozalishwa katika kipindi hiki chote cha utawala huu, kwa hiyo, si jambo la kulifanyia dhihaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nabaki hapo hapo kwenye Liganga na Mchuchuma, mradi wa Mchuchuma utakaozalisha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, umeme ambao utazalishia chuma cha Liganga, mtambo huu utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme megawatts 600, hiyo ni faida nyingine. Sasa megawatts 600 ni sawasawa na nusu ya umeme wote tuliokuwa nao mwaka 2015. Mheshimiwa Rais amekabidhiwa nchi hii ilikuwa na umeme wa megawatts 1,308 sasa Mchuchuma peke yake itazalisha umeme megawatts 600, si kitu kidogo wala siyo cha kukidharau. Umeme huu sawa na robo ya umeme wote utakaozalishwa kwenye Stiegler’s Gorge. Stiegler’s Gorge watazalisha umeme megawatts 2,100 na megawatts 600 ni robo ya huo umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisisitize kwa kusema umeme huu wa megawatts 600 utakaozalishwa Mchuchuma ni asilimia
12.2 ya malengo tuliyojiwekea ya umeme tunaohitaji mpaka ifikapo mwaka 2020. Sasa unajua huwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila umeme. Katika michango yangu iliyotangulia nilisema, umeme tulionao Tanzania hauwezi kutupa Tanzania ya viwanda. Afrika Kusini mwaka 1970 walikuwa na megawatts 14,000, sisi leo tuna megawatts 1,500 mpaka 2,500, tunahitaji uzalishaji mkubwa wa umeme. Mradi wa Stiegler’s Gorge ni mradi muhimu sana kwa Taifa letu, lazima tuupe nguvu, lazima tuunge mkono lakini lazima tuongeze vyanzo, chanzo kingine ni huu wa Mchuchuma, megawatts 600, kwa kutumia makaa ya mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeongea kwa msisitizo mkubwa kwa sababu ninaamini hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila umeme wa kutosha na hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila kwenda Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, niongezee tu hapo, kwenye hili suala la umeme. Wenzetu nchi nyingine wanaongea megawatts 84,000 sisi tunaitafuta Tanzania ya viwanda bila kwenda kuchimba chuma, bila kwenda kushughulika na Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nichangie tu kwamba, Tanzania tuna bahati, tumeendelea kuvutia wawekezaji na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri amefanya sana kazi tumeona wawekezaji toka nchi mbalimbali wanakuja kutoka Ujerumani, Ufaransa, ni initiative kubwa sana hii, watu wamebeza lakini wanabeza kwa sababu hawajui misingi ya uchumi. Hawa wanapokuja watatuongezea teknolojia na mtaji, tutahakikisha kwa kuwatumia hao tunavuka, tunafikia haya malengo yetu lakini eneo muhimu ni kulinda viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu muda haujanitosha, nichukue nafasi hii kukushukuru sana na naunga mkono hoja.