Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, nashukuru na mimi kupata fursa ili niweze kuchangia machache. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika maeneo mawili matatu ambayo yalipata kuchangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni vizuri likatolewa ufafanuzi. Iliafikia hatua wengine wakasema kwamba Serikali hii haina mipango ndiyo maana Msimbazi maji yanaingia na hawaelewi nini ambacho kinaendelea, ni vizuri sana nikachukua fursa hii kuweza kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Dar es Salaam ya miaka hiyo wakati tunapata uhuru na leo kuna tofauti kubwa sana, ongezeko la watu ni kubwa. Lakini Serikali inayoongezwa na Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ina azma ya kuhakikisha kwamba, Jiji la Dar es Salaam linakuwa mahali salama kwa kuishi na hasa naomba niongelee Bonde la Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, DFID kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa ninavyoongea kimetengwa kiasi cha dola milioni 20 na tayari wameshapatikana watalaam waelekezi, kampuni kubwa mbili za kimataifa ambalo moja kazi yake ni kuweza kufanya tathmini kujua athari za mafuriko ndani ya Bonde la Msimbazi hasa Msimbazi ya Chini, na kushauri nini kifanyike, ujenzi upi ufanyike ili athari hii ambayo tunaipata; sisi sote ni mashuhuda inayptokana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo kati ya dola milioni 20 ni package kutoka katika paundi milioni 49 ambayo ina kazi nzima ya kuhakikisha kwamba kwa kupitia utaratibu wa Tanzania Urban Resilience Programme tutakabiliana na tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mshauri huyu anaitwa COWI Tanzania Limited ameshamaliza kazi yake na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuko kwenye hatua za mwisho kwa kuweza kupata mshauri mwelekezi ili feasibility study ifanyike na ujenzi uweze kuanza kufanyika. Pia katika lile Bonde la Msimbazi kuna awamu ya pili ambapo tayari package nayo imeshatolewa ambayo tunataka kuanzia Bonde la Msimbazi mto unakoanzia kule juu kabisa, kutakuwa na kazi ya kuhakikisha kwamba kuna wale watu ambao wanatakiwa wahamishwe. Vilevile ujenzi ufanyike ili eneo lile ambalo tukipata leo unaona ni sehemu isiyofaa patengenezwe namna nzuri ni ile ambayo itakuwa ni recreation areas kwa ajili ya kuvutia. Pia kuwe na shughuli za kila siku ambazo zitafanyika tukiwa tunahakikisha pia hatuwi na tatizo la mafuriko kama ambavyo tumekuwa tukikubwa na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi, kuna mradi wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi awamu ya pili, jumla ya kilometa 20.3 kuanzia Kariakoo kwenda mpaka Mbagala. Mpaka sasa hivi kandarasi imeshatangazwa na itafunguliwa tarehe 20 Mei, 2018. Kwa hiyo, akipita Mbunge anasema kwamba Serikali hii haina mipango, inawezekana labda mtu hana taarifa nini ambacho kinaendelea. Ni vizuri tukaelezana ili mkajua, kwamba tuko makini tumejipanga na tutahakikisha tunakonga nyoyo za Watanzania waliochagua Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache naomba nimpishe mwenzangu naye achangie katika yaliyojitokeza.