Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kwa maandishi tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro katika Kijiji cha Kambala. Serikali imeshindwa kutatua mgogoro huu. Serikali imejenga korongo la kuwagawa wakulima na wafugaji kufuatia migogoro ya mara kwa mara. Korongo hili limetumia zaidi ya shilingi milioni 147, fedha za mapato ya halmashauri ilizokuwa inadai Kiwanda cha Mtibwa Sugar.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zingeweza kusaidia kujenga zahanati na majosho ya mifugo badala ya kujenga korongo la kuwatenganisha wakulima na wafugaji, tunatengeneza Taifa la namna gani? Tunahubiri amani na ushirikiano lakini tunakuja na maamuzi ya kuwagawa Watanzania kwa kutenganisha jamii hizi. Nashauri Serikali itumie busara kupitia maamuzi haya ili kurudisha mahusiano kwa jamii hizi. Tatizo la wakulima na wafugaji lingeweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia nguvu. Serikali iangalie mashamba yaliyohodhiwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu pamoja na ranchi zikiwemo za Wami Dakawa zitumiwe na wananchi baada ya Serikali kufanya utaifishaji na kugawa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliyopita iliagiza zaidi hekari 5,000 zigawanywe kwa wananchi ili kuondoa kero ya upungufu wa maeneo ya kilimo na ufugaji. Eneo hilo limechukuliwa na vigogo wamegawana badala ya kutolewa kwa wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ichukue hatua kama ilivyoagizwa wananchi wapate ardhi hii badala ya vigogo kujinufaisha na maamuzi ambayo yameshatolewa na Serikali. Ni wakati wa Serikali kusimamia maamuzi yake yaliyokwishatolewa na si kuyabatilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA - stakabadhi ghalani. Ukopaji wa mazao kwa wakulima mwaka jana umesababisha usumbufu mkubwa na wakulima walikopwa mazao kwa muda mrefu lakini walicheleweshewa malipo yao. Wengine wamelazimika kutumia nguvu kudai jasho lao. Tumeshuhudia wakulima wa maeneo ya Kibaigwa, Mbeya, Morogoro waliandamana kudai malipo yao. Zoezi la kuwalipa wakulima hao limechukua muda mrefu huku wakulima wengi wakipata hasara katika taasisi za fedha walizokopa kwa ajili ya kilimo na walitegemea kurejesha baada ya msimu wa kilimo badala yake iliwachukua miezi na miaka kudai malipo pasipo kupata jibu.
Nashauri Serikali iwalipe fidia wakulima kwa kuwa mazao waliuza kwa shilingi 500 na kuuza kwa 800, Serikali ilitengeneza faida kwa nini Serikali isingetoa fidia/kifuta jasho kwa wakulima hao? Mfumo huu wa NFRA unapaswa kuangaliwa upya na kwa mwaka huu Serikali ije na mpango/mfumo mpya wa kuwalipa wakulima mara baada ya kuuza mazao yao. Pia ikiwezekana NFRA iwe na mfumo wa kuwakopesha pembejeo na mbegu wakulima ili walipie baada ya kuvuna mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mazao, hii imekuwa kero ya muda mrefu kwa wakulima na ni ukandamizaji wa wakulima ambapo kuna milolongo ya ushuru wa mazao kutoka shambani kwenda sokoni, sokoni kwenda stoo za soko na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri huu unaendelea kuwakandamizi, wakulima wanakata tamaa badala ya kuuza mazao yao sokoni mfano soko la mazao Kibaigwa sasa wanakwepa ushuru na wanauza mazao mashambani kama lumbesa na kuendelea kupata hasara. Imefikia wakati sasa Serikali kuangalia upya viwango vya ushuru wa mazao, kuondoa mageti ya ushuru kwenye vijiji ili kuwezesha wakulima kuwa na ushuru mmoja tu usiowaumiza na pengine ushuru mwingine wapewe wafanyabiashara wanaonunua mazao toka kwa wakulima au kwenye masoko.