Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja na kabla ya kuzungumza lolote napongeza jitihada ya Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na baadhi ya wataalamu kwa kazi nzuri waifanyayo kwa wananchi wa Tanzania na jinsi wanavyomuunga mkono Rais mpendwa kwa jitihada zake za kumtua ndoo mwanamke kichwani na kwa kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya mita 400. Mola awape wepesi na nguvu ya kufikia azma ya Rais wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni kati ya mikoa ambayo inakumbwa na magonjwa ya mlipuko kila mara kutokana na kutokuwa na visima virefu vya maji safi na salama hasa vijijini. Wananchi hutumia maji ya visima vifupi, madimbwi, mito na Ziwa Rukwa ambayo ni maeneo yasiyo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia ukurasa wa 267 hadi 279 kuna orodha ya visima 225 lakini hakuna kisima hata kimoja kwa Mkoa wa Rukwa. Tunaomba hawa Mawakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) wafike na Mkoa wa Rukwa kwa zoezi hili la uchimbaji wa visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu wa maji nchi nzima na kuwa na miradi kadhaa ya maji ambayo bado haijakamilika na iliyokamilika hakuna maji na wakati pesa ya Serikali inakuwa imetolewa na huku haitoshelezi mahitaji, tunaomba miradi ambayo haijakamilika itambulike na kuandaliwa mpango mkakati maalum wa kuikamilisha. Kwa ile miradi iliyokamilika na haina maji na pesa ya Serikali imetolewa ni vema wahusika wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kuona namna ya kuvuna maji ya mvua kwani mafuriko yamekithiri hapa nchini. Tutafute namna ya kuyavuna kuliko kupotea bure na kuyatumia kwa matumizi ya majumbani, mabwawa ya mifugo na hata umwagiliaji. Kwa matumizi ya maji safi na salama, kwa matumizi ya majumbani kwa wananchi wetu, ni vema Serikali kukubaliana na mapendekezo ya kuongeza shilingi 50 kwenye mafuta ya dizeli na petroli ili Mfuko wa Maji uwe na fedha za kutosha. Fedha za Mfuko wa Maji kwa Mkoa wa Rukwa shilingi 4,101,400,911 hazitoshelezi mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tufanye ukaguzi wa miradi kabla ya kuiendeleza. Aidha, uwepo ukaguzi wa kila hatua ya miradi kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali kuwa tete ya upatikanaji wa maji kutolingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali na mahitaji halisi ya wananchi wetu, nashauri wataalam waliopo ni vema wakatathminiwa kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa dhamira ya Rais kuwatua akina mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.