Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpongeza Waziri wa Maji, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watenddji wote walioshiriki katika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kwa kueleza changamoto zilizoko katika sekta ya maji na umwagiliaji. Kumekuwa na matukio mengi ya maafa yanayosababishwa na mafuriko ya mvua nyingi hali ambayo husababisha uharibifu wa mali na hata vifo vingi kwa wananchi wetu vilivyotokana na mafuriko ya mvua hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Idara hii ya Umwagiliaji inakuwepo kipindi chote cha awamu zote na utawala na kumekuwa na matamko na ahadi mbalimbali kwa kuahidi kujenga mabwawa na miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji hapa nchini, lakini hakuna matokeo ya kuridhisha katika sekta hii ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua kwamba jiografia ya nchi yetu ya Tanzania imejaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na mabonde mengi ya kuvuna maji, mito, maziwa, milima mingi na rasilimali ya mvua, vyote hivi vikitumika ipasavyo tunaweza kutatua changamoto kadhaa kama za kilimo cha umwagiliaji na kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na upotevu mkubwa wa maji ya mvua ambayo hutiririka mabondeni kuelekea kwenye makazi na mashamba ya watu, hali hiyo husababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali na hata vifo vingi kutokana na mafuriko na mvua nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokanana maafa hayo mara nyingi Serikali hulazimika kutoa misaada mbalimbali kwa dharura kwa ajili ya wahanga hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ingewekeza kwenye kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji na kujenga miundombinu kwa ajili ya malisho ya wafugaji. Kwa kuwekeza katika sekta hii ya umwagiliaji kutasaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana na akinamama. Vilevile kutasaidia kupunguza mafuriko ya mara kwa mara kwa kuwa maji mengi ya mvua yatavunwa kwa ajili ya umwagiliaji na malisho, hivyo ugomvi baina ya wakulima na wafugaji utakuwa umekwisha. Maana mapigano yanasababishwa na ukosefu wa malisho kwa mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ihamasishe wananchi jinsi ya kuvuna maji ya mvua na hasa katika taasisi za umma kama shule, taasisi za kiserikali na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuwekeza katika kujenga miradi mikubwa ya mabwawa kwa ajili ya malisho ya mifugo yote hapa nchini. Awamu ya Tano inasthili sifa kubwa kwa mageuzi makubwa katika sekta ya maji, kazi kubwa inaendelea na inaonekana.