Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi leo nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitaanza na Mradi wa Maji Kibiti, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba sasa hali ya ulinzi Kibiti imeanza kuimarika, Kibiti shwari, sasa shida yetu maji, wale watu waliokuwa wanatuua tumewamaliza sasa hivi shida yetu imekuwa maji, tatizo Kibiti ni maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mradi wa maji Kibiti. Huu mradi wa maji wa Kibiti umekamilika na unatoa huduma, lakini bado unasuasua kwa sababu huu mradi ni mkubwa na haupatiwi fedha ya aina yoyote ya ruzuku ili kuweza kuendesha mradi ule. Tuna gharama kubwa ya kulipa bili ya umeme, vibarua, hata na baadhi ya vioski, tunaomba sasa Wizara iangalie kwa jicho la huruma mradi huu wa maji Kibiti ingeweza kuwapatia fedha kidogo ili kuweza kuendesha mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko miradi saba ambayo haifanyi kazi kutokana na miradi hii kuchakaa. Miradi hiyo ni kama Kijiji cha Luaruke, Jaribu Mpakani, Mtawanya, Muyuyu, Mkenda na Kibiti. Wizara iangalie jinsi gani ya kuweza kupeleka fedha za ukarabati wa miradi hii ili iweze kutoa huduma, miradi hii ipo kwa muda mrefu imekosa fedha ya kufanyia ukarabati kwa hiyo, inashindwa kutoa huduma iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kule Jimboni kwangu nimechoka kusuluhisha ndoa kwa sababu muda mwingi wanandoa wanakwenda kutafuta maji visimani na baba anashindwa kuwa na imani mkewe kweli amekwenda kisimani au amekwenda kwenye mchepuko. Kwa sababu maji yanatoka mbali na huko kisimani ukienda maji yenyewe yanakuwa ya kulindia, kwa hiyo, baba anakosa imani kwa hiyo, tumekuwa na migogoro mikubwa ya wanandoa kule Jimboni kwangu Kibiti. Ningeomba Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi gani ataangalia Kibiti kwa jicho la huruma utupatie maji katika vijiji vyetu vya Kibiti vilivyobakia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mwaka jana tulipata fedha, zile fedha tumeziona kwenye makaratasi tu, lakini uhalisia maji yenyewe Kibiti hakuna. Sasa hapa Waziri hebu angalia ilionekana kama kuna mgomo baridi baina ya Wizara na Halmashauri zetu kwamba fedha zinakaa Wizarani lakini mradi unatekelezwa Wilayani, kule Wilayani hampeleki fedha kwa ajili ya ufuatiliaji, ukiangalia ni kama kuna mgomo baridi, mnasema ninyi huko Wilayani mtangaze tender halafu muandae certificate mlete huku Wizarani, kule Wilayani kwenyewe kazi hazifanyiki kwa wakati, sasa hilo nalo mliangalie kwamba mgomo baridi huu upo wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana kwamba watu sasa wameamua kugoma kuwaangalia ninyi Wizara mtafanikiwa au hamtafanikiwa. Kwa hiyo, ningeomba ili muangalie kama mnaweza mkafanya hii miradi ya maji kwa kutumia force account basi fanyeni kwamba hizi fedha ingizeni kwenye kijiji husika wao wenyewe wasimamie maana ndiyo wenye uchungu na ndiyo wenye shida ya maji, tunaweza tukafanikiwa kwa jitihada zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unavyoizungumzia Kibiti lazima uzungumzie maeneo ya Delta kwamba Kibiti zipi kata tano ambazo ni Delta ambayo ina vijiji 17, vitongoji 42, huko kote hatuna maji safi na salama. Unapokosa maji safi na salama hata shughuli za uzalishaji zinashindwa kufanyika kwa wakati. Maeneo hayo kama ya Nyamisati, Kiomboni, Saninga na Simbaulanga, kote huku hatuna maji ya uhakika, ningeomba Wizara angalieni jinsi gani ya kutufikishia maji katika maeneo hayo ya Delta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hivyo hatuna watumishi wa kutosha katika Idara hii ya Maji Wilayani kwetu Kibiti. Wilaya hii inaelekea tunaweza tukakosa ufanisi wa kazi wenye tija kutokana na upungufu wa watumishi na vitendeakazi. Mpaka leo Kibiti hatuna gari idara ya maji, unapokosa vietendeakazi utashindwa kufanya kazi yao kwa ufanisi. Kwa hiyo, ningeomba sana Wizara muiangalie kwa jicho la huruma Kibiti. Kwanza tumeathirika kwa yale mauaji tu Kibiti tumeathirika. Kwa hiyo, Wizara lazima uiangalie Kibiti kwa jicho la huruma mtusaidie Kibiti tumeathirika tatizo maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hiyo viko baadhi ya vijiji kama vile Makima, huu Mji unakua kwa kasi lakini pana tatizo la maji na ndiyo maana ukiangalia kila Mbunge humu akisimama analia na maji na ukiangalia mwaka 2015 katika ahadi zetu tulisema tunakabidhi maji kila kijiji, sasa leo usiku wa deni mfupi, Wandengereko kule tunasema hakuna shughuli ndogo kwamba mwaka 2020 tukifika tutaongea nini majukwaani? Maji yenyewe mpaka leo tumeishia kuyaona kwenye makaratasi tu? Ukiangalia kwenye makaratasi kweli maji unayaona, lakini ukienda uhalisia kule vijijini maji hakuna, sasa nashindwa kujua kwamba hawa wataalam wetu wanatufanyia mawele au wanatufanyia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tatizo la maji hili ni janga la kitaifa, muangalie jinsi gani ya kutusaidia katika Wilaya yangu mpya ya Kibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja.