Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, vilevile nichukue fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Makatibu wote Wakuu.

Wizara hii ya Maji ni Wizara muhimu kama ilivyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, binafsi ninapongeza shughuli ambazo zinaendelea kwenye Taifa letu na kwenye Jimbo langu la Kalenga. Binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kufika Jimboni kwangu. Siyo tu Waziri Kiongozi lakini Naibu Waziri pia amefanya kazi kubwa sana kuweza kuhakikisha kwamba Jimbo la Kalenga linakaa vizuri. Pongezi zangu zifike kwako kwa sababu hata ile fedha uliyonipa shilingi 500,000 kuwapelekea wananchi wangu ninakushukuru sana, Mheshimiwa Waziri naamini ni mwanzo mzuri. Ilikuwa ni fedha binafsi kutoka kwenye mfuko wake na mimi nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba kuna miradi mbalimbali ambayo inaendelea, lakini nizungumzie mradi mahsusi ambao sasa hivi una takribani miaka sita tokea uanze. Mradi wa Itengulinyi, Isupilo kuelekea Magunga. Huu ni mradi mkubwa sana ambao Serikali iliingia mkataba na Mkandarasi RJR kwa zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 2.4. Leo hii tunavyozungumza, nimeshaongea mara kwa mara Bungeni kukumbusha umuhimu wa mradi huu wa maji. Mpaka leo fedha ambazo zimetolewa ni zaidi ya shilingi bilioni 1.2 na mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yangu ya Iringa Vijijini leo hii tunavyoongea imepelekwa mahakamani kwa ajili ya mradi huu, mradi haujakamilika na mkandarasi ameipeleka Halmashauri mahakamani na tunaendelea kusubiri nini kitatokea kwa sababu mkandarasi huyu anadai Serikali fedha ya riba ziadi ya shilingi milioni 250, nashindwa kufahamu tumeshapeleka fedha za mradi zaidi ya shilingi bilioni 1.2 lakini utaratibu unavyokwenda mpaka leo ni muda mrefu sasa Serikali imeshindwa kuingia makubaliano na Mkandarasi huyu ili mradi huu ukamilike na wananchi wangu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mradi ambao ungeweza kutatua tatizo la maji kwa zaidi ya vijiji vinne na ni mradi ambao binafsi ungekamilika ningeshukuru sana na wananchi wangu ambao katika bajeti hii iliyoelezwa kwa kweli hatujatengewa fedha za kutosha kwenye suala la maji, na kama tunavyofahamu maji ni uhai na wananchi wa Jimbo la Kalenga wanahitaji maji kama majimbo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona utaratibu ambao umeoneshwa kwenye Wizara kuhusu suala la maji, lakini kwanza fedha ambazo tumekopa kutoka India jumla ya dola za Kimarekani milioni 500 ningependa kujua, je, ni utaratibu gani umetumika kwa Serikali kupeleka hizi fedha katika yale maeneo ambayo tumeyatenga 17, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tufahamu kwamba kuna maeneo mengine mengi ambayo yameshaelezwa na yameoneshwa kwenye kitabu cha hotuba, mengine yamepata miradi ya maendeleo, mengine fedha kutoka Serikali, mengine miradi ya umwagiliaji, lakini kuna maeneo kama Jimbo langu la Kalenga hatujapata hata senti moja kutokana na maeneo haya ambayo yametengwa. Kwa sababu inaonesha kabisa kwamba fedha zimetolewa na kuna fedha zingine kutoka Serikali Kuu, fedha kutoka miradi mbalimbali kwa ajili ya mwaka huu wa fedha na mambo mengine chungu nzima, lakini Jimbo langu la Kalenga bado halijapata au halijatengewa fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba tumetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya bajeti hii ya 2018/2019 lakini Serikali lazima itambue kwamba kuna maeneo au kuna Wilaya ambazo zina majimbo mawili, fedha hizi bilioni 1.3 zikitenganishwa katika majimbo mawili bado zinakuwa hazitoshi. Jimbo langu la Kalenga peke yake bajeti yake ni jumla ya shilingi za Kitanzania milioni 735, sasa sina uhakika kama fedha hizi zitafika kwa wakati au hazitafika kwa wakati lakini ninachoomba Wizara ni kwamba hebu tujitahidi kupeleka fedha katika maeneo ambayo matatizo ya maji ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo ambayo tulipitisha mwaka jana ya shilingi 50, sasa hivi ningependa tu kuishauri Serikali kwamba kama tukakubaliana zikawa shilingi 100 zikaenda katika kwenye maji basi nina uhakika kabisa tatizo la maji linaweza likawa limepungua. Shilingi 50 ambayo tumeitenga mwaka jana imeweza kukusanywa na tukapata jumla ya shilingi bilioni 158, ina maana kama tungefanya kwa shilingi 100 tungepata zaidi ya shilingi bilioni 300 ambazo tungegawanya katika Wilaya au katika Majimbo tungepata fedha nyingi sana. Hili ningependa Wizara iweze kuliangalia sana na kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo dogo kuhusu miradi ya umwagiliaji, pale Jimboni kwangu tuna mradi wa maji wa umwagiliaji wa Mlambalasi, ambao kwenye kitabu hiki cha hotuba inaonesha kwamba mradi umekamilika, lakini ukweli ni kwamba mradi haujakamilika na zaidi ya shilingi milioni 800 bado zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ulifika Jimboni na umezunguka mara kwa mara umeona, ninaamini hata hili ninalolizungumza unalifahamu, tunachohitaji ni shilingi milioni 800 ili mradi huu uweze kukamilika, naona kwamba umuhimu wa umwagiliaji ni mkubwa lakini tunasahau eneo hili la umwagiliaji kwa sababu tumejikita sana kwenye miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie suala la miradi mbalimbali ya maji ambayo haikamiliki katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ningeomba kuishauri Serikali kwamba sasa ifike wakati Serikali ipeleke special audit kwenye miradi yote ya maji katika nchi hii. Nilikuwa kwenye Kamati ya LAAC kwenye kipindi kilichopita nimeshuhudia miradi mbalimbali ya maji ambayo imetelekezwa na wakandarasi, imetekelezwa na Halmashauri, aidha fedha hazijakwenda au kama fedha hazikwenda basi kuna utapeli wa hali ya juu ambao umefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni suala la msingi kwa sababu tutakapoongeza hizi fedha hizi za tozo nina uhakika kabisa kwamba tunaweza kufanya special audit na tukapata miradi mbalimbali ya maji ambayo ilikuwa haijakamilika na hatimaye ikakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kuna Wasimamizi Elekezi (Consultants), katika maeneo mbalimbali ukiangalia watu hawa, ndiyo wamefanya kazi nzuri na wanaendelea kufanya kazi nzuri, lakini kuna maeneo ambayo wamekuwa kama kichaka cha kujipatia fedha bila kuangalia ufanisi wa kazi. Consultant anapewa kazi, anafanya kazi lakini baada ya muda fulani anatokomea na zile fedha ambazo alitakiwa alipwe, analipwa lakini mradi unakuwa haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotokea vijijini tunaona mengi na tunajua kuwa miradi ya maji ni mikubwa lakini kama fedha zinakuwa haziendi au zinatumiwa vibaya nina uhakika kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo lazima sasa kama Wizara iweze kuweka jicho lake na kuangalia na kwa umakini zaidi na kuona je ni wapi ambapo tumekosea? Eneo hili ni mojawapo na ninaamini kama tutaweka macho ya uhakika na tukaangalia vizuri tunaweza tukawa na uhakika wa kupata maji katika maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu na miji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia mradi mmoja wa Nyamlenge katika Jimbo langu. Design inahitaji shilingi milioni 49, ningeomba Serikali iweze kuangalia mradi huu kwa sababu unakidhi viwango vilevile utapeleka maji katika vijiji zaidi ya 15. Mheshimiwa Waziri naamini unanisikia, uko hapo pamoja na Naibu Waziri ninaomba mradi huu wa maji muweze kuangalia. Nilishapeleka proposal sijajua mpaka leo imefikia wapi na nimejaribu sana kufuatilia bado sijajua hizi milioni 49 ambazo zingeweza kukidhi mahitaji ya mradi huu kama zingepatikana zingeweza kuleta tija sana katika suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema mengi naamini kwa haya machache ambayo nimeyaeleza Serikali itayachukua itaenda kuyafanyia kazi na hatimaye Jimbo la Kalenga na Mkoa wa Iringa uweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nikushukuru sana na ninawatakia kila la kheri Wizara ya Maji. Ahsante sana.